Wafanyabiashara 18 nguvuni kukiuka bei elekezi ya sukari Katavi

Mawakala wa sukari wakiendelea kushusha bidhaa hiyo mkaoni Katavi.

Muktasari:

  • Wafanyabiashara hao wanadaiwa kuuza Sh3500 hadi Sh4000 kilo moja ya sukari na kujipatia faida ya Sh51,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50 badala ya Sh11,000 hali inayowaumiza wananchi.

Katavi. Wafanyabiashara 18 mkoani hapa, wamekamatwa wakiuza sukari  Sh3500 hadi 4000 kwa kilo moja, kinyume na bei elekezi ya Serikali ya Sh3200.

Uuzaji holela huo usiofuata bei elekezi ya Serikali umetokea baada ya mkoa kupokea tani 244 sawa na mifuko 5,780 ya sukari.

Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi Februari 29,2024 ofisini kwake Mkuu wa mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema wafanyabiashara hao wamekamatwa wakikiuka utaratibu.

“Tumewakamata Februari 28,2024,hatua mbalimbali za kisheria zinaendelea kuchukuliwa, hatutasita kuwakamata wote wanaokiuka bei elekezi ya bidhaa hiyo tunawasaka iwe usiku au mchana.”

“Serikali imelipia kodi hivyo bei elekezi  kupitia waraka wa GN namba 40A na 40B kwa Mkoa wa Katavi ni Sh2900 hadi Sh3200,”

Aidha amewaelekeza Wakuu wa wilaya kufuatilia na kuwadhibiti wafanyabiashara wanaokaidi utaratibu na  wananchi wakibaini tatizo hilo watoe taarifa.

Mashala Jilasi miongoni mwa mawakala wanaosambaza  sukari mkoani hapa,  amesema wao wanafuata bei elekezi ya Serikali changamoto ni  kwa wafanyabiashara wa rejareja.

“Tunatekeleza agizo la Serikali niwashauri wateja wetu wasipandishe bei, warudi kwenye utaratibu unaotakiwa,”amesema Mashala.

Lidya Ramso ambaye ni mama lishe wa Manispaa ya Mpanda amesema mfumuko huo wa bei ya sukari umesababisha kupandisha bei ya kikombe cha  chai kutoka Sh200 hadi 300.

“Wateja hakuna na waliopo wanalalamika, awali tulikuwa tunanunua kilo moja Sh5,000 hadi 4,500 ya sukari,  kwa sasa imeshuka imefikia Sh4,000 nilikuwa sifahamu bei elekezi ya Serikali,”amesema Lidya.