Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madumu zaidi ya 700 ya mafuta ya kupikia yakamatwa Unguja

Mwakilishi wa Kampuni ya Sahara ambayo ni wakala wa mafuta ya kupikia ya Oki, Salum Mohamed akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamatwa madumu 747 ya mafuta yaliyokuwa yakibadilishwa stika ya kampuni nyingine na kuwekwa ya kampuni yao kinyume na utaratibu wa kisheria. Picha na Haji Matumwa.

Muktasari:

  • Mafuta hayo yamedaiwa kuwa yanatoka nchini Indonesia na yalikuwa na utambulisho wa Uturuki

Zanzibar. Madumu 747 ya mafuta ya kupikia ya lita 20 yamekamatwa na Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) mjini Unguja yakidaiwa kuwa katika hatua za mwisho za kubadilishwa stika ya Uturuki na kuwekwa stika ya Oki.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA, Dk Khamis Ali alisema jana kuwa mmiliki wa mafuta hayo ni mfanyabishara aliyekuwa na lengo la kuhakikisha bidhaa hiyo ionekane bora kwa kuweka stika za Oki ili iwe rahisi kuuza.

“Utambulisho huo wa Oki uliokuwa ukitumiwa kinyume na sheria na mfanyabiashara huyo ulikuwa wa kughushi na lengo lake kubwa ni kutafuta soko la bei ya juu katika masoko nchini jambo ambalo halikubaliki hata kidogo,” alisema Dk Ali.

Alifafanua kuwa mafuta hayo yaliyokuwa yanabadilishwa stika yamebainika kuwa yanatoka nchini Indonesia na yalizalishwa Mei 2017 na muda wa mwisho wa matumizi ni Mei 2019, hivyo yapo salama kwa ajili ya matumizi na kosa la mfanyabiashara huyo ni kubadilisha utambulisho halali wa Turkey (Uturuki) na kuweka Oki.

Alisema mfanyabiashara huyo hivi sasa anashikiliwa na vyombo vya sheria na wakati wowote atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za udanganyifu wa biashara hiyo.

Mwakilishi wa Kampuni ya Sahara ambao ni wakala wa mafuta ya Oki, Salum Mohamed alisema kitendo hicho cha udanganyifu hakikubaliki hata kidogo.

“Tunajua amefanya hivi kwa kuona kuwa mafuta yetu yanauzika sana ila siyo kitendo kizuri hata kidogo kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta madhara makubwa ya kibiashara kwa baadhi ya wateja ambao wangeweza kutumia mafuta hayo yaliyobadilishwa huenda wangetufikiria sisi vibaya kumbe wala hatuhusiki na udanganyifu kama huo,” alisema.

Alifafanua kuwa ni vyema kwa wafanyabishara kujiamini na biashara zao bila kuingiza udanganyifu ndani yake unaoweza kuleta madhara ya kibiashara kwa pande zote mbili.