Mafuriko yakata mawasiliano barabara kuu ya Hanang

Baadhi ya magari yakiwa yamesimama katika barabara kuu ya Hanang. Picha na Joseph Lyimo

Arusha. Mawasiliano ya barabara inayounganisha mikoa ya Kanda ya ziwa na Arusha yamekatika kwa muda kutokana na mafuriko wilayani Hanang mkoani Manyara huku mabasi zaidi ya 20 ya abiria yakishindwa kuendelea na safari zake.

Magari hayo yalianza kukwama kuanzia jana usiku Desemba 2, 2023 hadi leo mchana kutokana na mafuriko hayo ambayo yamesomba magogo, vitu mbalimbali pamoja na tope lililosababishwa na kuporomoka kwa sehemu ya Mlima Hanang.

Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja amesema leo Jumapili Desemba 3, 2023 kuwa jitihada zinaendelea kufanywa na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kurekebisha barabara ili kuruhusu magari hayo kupita.

"Mafuriko haya yameharibu miundombinu mbinu ya barabara na hivyo kusitisha usafiri wa kwenda mikoa ya Singida na Kanda ya Ziwa kutoka Manyara, Arusha na Kilimanjaro," amesema.

Shule tatu kupokea waathirika

Mkuu huyo wa wilaya amesema kutokana na mafuriko hayo ambayo yamesababishwa familia kadhaa kukosa makazi, maeneo kadhaa yameandaliwa kupokea waathirika.

Amesema maeneo hayo ni shule za Katesh, Ganana na Gedang'onyi.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kuwasaidia waathirika wa mafuriko haya.

Mmoja wa wasafiri ambaye alikuwa anatoka Arusha kwenda Mwanza, John Mashaka amesema wameshindwa kuendelea na safari kutokana na hali hiyo.

"Tunasubiri barabara itengenezwe tuweze kupita, tumekwama hapa tangu jana usiku lakini tumeelezwa hali itakuwa nzuri baadaye," amesema.


Mlima Hanang

Tatizo la maporomoko hayo yametokea katika Mlima Hanang ambao ni wa nne wa urefu nchini ukiwa na urefu wa mita 3,420 kutoka usawa wa bahari.

Chini ya Mlima huo, mamia ya watu wamejenga makazi ya kudumu na umekuwa unategemewa kwa wakazi wa Hanang kama chanzo cha maji.

Sehemu ya mlima huo ndiyo imeporomoka kutokana na mvua zinazoendelea na kusababisha maafa hayo.