Mafuriko yaleta balaa Simanjiro, 100 hawana makazi

Muktasari:

  • Mvua hizo zimesababisha mafuriko makubwa ambayo yameleta madhara ya mali, mazao, huku miundombinu ya barabara ikiharibiwa vibaya.

Simanjiro. Wananchi 100 kutoka katika Kijiji cha Kandoto, Kata ya Msitu wa Tembo, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, hawana makazi baada ya nyumba 27 zenye jumla ya familia 42 kuanguka na kuzingirwa maji kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha mjini hapa.

 Mvua hizo zimesababisha mafuriko makubwa ambayo yameleta madhara ya mali, mazao na kuharibu miundombinu ya barabara.

Akizungumza leo Jumamosi Novemba 25, 2023 na wananchi wa kata hiyo mara baadaa ya kutembelea eneo lilikumbwa na maafa hayo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Suleiman Serera amewataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuondoka kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Amesema kuwa, nyumba ambazo zimepitiwa na mafuriko ni 27, huku mbili kati ya hizo zilikuwa eneo hatarishi hivyo kuwataka wananchi wa kijiji hicho kutoa msaada kwa walioathirika ikiwamo chakula wakati  Serikali ikiendelea kutafuta nanma ya kuwasaidia.

"Kuna bibi nyumba yake imesombwa na maji na anasema alikuwa maeneo haya tangu mwaka 1968 lakini hajawahi kushuhudia mafuriko makubwa kiasi hiki, hivyo tahadhari zichukuliwe haswa kwa nyumba ambazo ziko kwenye eneo oevu, wananchi waondoke," amesema Serare.

"Wananchi wanalazimika kuogelea kwenye hayo maji au kuvuka kwa kutumia mitumbwi kwa ajili ya kwenda kwenye shughuli zao na kupata huduma muhimu Moshi mjini.

Amesema tayari ameagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), kutafiti na kuona namna ya kumaliza tatizo la maji hayo, kukatika barabara hiyo kila mwaka kunapokuwa na mvua.

Mkuu huyo amesema kwa sasa hatua zinayochukuliwa ni kuangalia usalama wa wananchi hao waliohifadhiwa katika maeneo ya shule, ili waweze kupata huduma muhimu za kijamii.

Diwani wa Kata ya Simanjiro, Kaleya Mollel amesema: “Kama mlivyosikia kaya 42 hazina makazi kutokana na nyumba zao kuanguka na kuzingirwa maji.

“Zaidi ya wananchi 45, wamepatiwa hifadhi katika shule za msingi na sekondari katika kata yetu, wengine 55 wamehifadhiwa  kwa ndugu na jamaa zao. Kiukweli hali ni mbaya, maji yanazidi kuongezeka, tunaiomba Serikali kutafuta ufumbuzi wa haraka,”amesema.

Amesema maji hayo yanajaa kutokana na mvua zinazoendelea kwenye wilaya za Hai na Arumeru.

"Maji hayo yalianza kuingia kwenye makazi ya watu kuanzia saa nane usiku, wananchi waliamshana na kuokoa baadhi ya mali hivyo wakati nyumba zinaanguka hakukuwa na madhara kwa binadamu na baadhi ya mali ziliokolewa," amesema.

Ameongeza kuwa: "Wananchi ndio wanaowasaidia waathirika wa mafuriko haya kwa chakula na  malazi kwa kuchangishana hivyo naomba Serikali kupitia mfuko wa maafa kutoa msaada wa haraka kwa wananchi hawa.

Mmoja wa wananchi hao Elisia Mollel (77) ameomba Serikali kuangalia uwezekano wa kudhibiti mkondo wa maji unaosababisha yajae katika maeneo hayo na kuacha wananchi wakipata hasara ya mali, mazao na mifugo.

Amesema mvua zilizosababisha mafuriko katika kata hiyo, zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalinbali ya mkoa wa Kilimanjaro, Arusha na Manyara na kwamba kuna mkondo wa maji ambao uanayakusanya na kuyaelekeza katika kata hiyo.

Kaimu Meneja Tarura Mkoa wa Manyara, Naftali Chaula amesema Barabara ya Msitu wa Tembo - TPC iko kwenye ujenzi wa kiwango cha lami na kutokana na madhara ambayo yamesababishwa na mvua itabidi ujenzi wa lami usitishwe,  ijengwe upya kwa kuongeza karavati ambazo zitakuwa zinapitisha maji kwa urahisi

Amesema pia  watajenga kingo katika Mto Kikuletwa ambao ndiyo chanzo cha mafuriko hayo, hatua itakayomaliza tatizo la kujaa maji kwenye mashamba na makazi ya wananchi hao kwa asilimia 80.