Mafuriko yaua saba, yavunja nyumba 43, yafyeka mazao ekari 23,501 Ifakara

Muktasari:

  • Licha ya eneo hilo kuwa kwenye mkondo wa maji, lakini Kimbunga Hidaya kinatajwa kusababisha maafa ya watu saba, kubomoa nyumba 43 zilizokuwa zikitumika kwa makazi na kuharibu ekari 23,501 za mazao mbalimbali mashambani.



Dodoma. Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na Kimbunga Hidaya ni Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro.

Kikosi Cha zimamoto na uokoaji wilaya ya Kilombero wakiokoa wananchi wa maeneo mbalimbali ya mji wa Ifakara Kwa kutumia boti baada ya mvua kubwa kunyesha kwa zaidi ya saa 72 na kusababisha mafuriko katika maeneo hayo. Picha Hamida Shariff

Licha ya eneo hilo kuwa kwenye mkondo wa maji, lakini Kimbunga Hidaya kinatajwa kusababisha maafa ya watu saba, kubomoa nyumba 43 zilizokuwa zikitumika kwa makazi na kuharibu ekari 23,501 za mazao mbalimbali mashambani.

Baadhi ya askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na wananchi, wakiwa wamebeba mwili wa Mwanaume ulioopolewa eneo la Mto Rau, Kata ya Msaranga, ambao umesombwa na mafuriko. Picha na Florah Temba

Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa maswali ya papo kwa papo bungeni jijini Dodoma, leo Mei 9, 2024.

Majaliwa amesema katika halmashauri hiyo juma la kata nne za Viwanja 60, Mbasa, Kibaoni na Katindiuka zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na athari za mvua zilizosababisha mafuriko baada mto Lumemo kujaa na kumwaga maji kwenye makazi ya watu.

Mmoja wa wananchi wa mtaa wa Kwakomba, Kata ya Mji Mpya, Manispaa ya Moshi, akijaribu kuokoa baadhi ya vyombo vyake baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kujaa maji na tope, kutokana na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia leo, Aprili 25, 2024. Picha na Florah Temba

Mbali na athari hizo, pia nyumba 512 zilizingirwa na maji na kuharibiwa kwa miundombinu ya barabara zinazounganisha wilaya kwa wilaya, barabara za vijiji na mitaa pamoja na miundombinu ya Reli ya TAZARA.

Mazao yaliyoharibiwa ni pamoja na mahindi, mpunga na mazao mengine mchanganyiko na mifugo.