Mafuta yaadimika Mbozi, Ewura yaonya

Muktasari:
- Wananchi wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe, wamelazimika kutembea mwendo mrefu baada ya baadhi ya madereva wa vyombo vya usafiri wa umma kusitisha huduma hiyo, kufuatia uhaba wa mafuta ya petrol na diesel.
Songwe. Wananchi wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe, wamelazimika kutembea mwendo mrefu baada ya baadhi ya madereva wa vyombo vya usafiri wa umma kusitisha huduma hiyo, kufuatia uhaba wa mafuta ya petrol na diesel.
Inadaiwa kuwa uhaba wa Mafuta umeanza tangu wiki iliyopita ambapo vituo vingi havina bidhaa hiyo, hali ambayo kwa upande mwingine imewafanya wache wenye nishati hiyo kuiuza kwa ya kati ya Sh4, 000 na Sh4, 500 kwa lita moja.
Aidha taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari imesema mafuta yapo ya kutosha nchini, na kuzionya kampuni zinazohodhi bidhaa hiyo malengo ya kusubiri bei ya mwezi ujao akisema ziache mara moja tabia hiyo.
Hata hivyo, mmoja wa wakazi wa Vwawa wilayani Mbozi, Magreth Halinga, ameiambia Mwananchi Digital, kwamba amelazimika kutembea kilometa mbili kwenda kazini kwake, baada ya kukosa usafiri wa bodaboda na bajaji.
"…Serikali ichukue hatua za haraka kwani shughuli za uzalishaji mali zinakwama, kama mimi leo nimechelewa kufika kazini, sababu za ukosefu wa mafuta," amesema Magreth.
Mmoja wa waendesha Bajaji katika mji wa Vwawa Yassin Mbembela amesema kutokana na kukosekana Mafuta anakusudia kusitisha huduma ya usafiri kwa kuwa hawezi kupata faida iwapo ataendelea kununua mafuta mtaani kwa bei kubwa.
Amesema ilia pate faida, atalazimika kupandisha bei ya nauli kwa wateja wake, jambo ambalo kwa upande wake amesema ni gumu.
Naye Samwel Edward, Dereva wa basi dogo linalofanya safari zake kati ya Mlowo na Tunduma, amesema mpaka jana jioni mafuta yalikuwa yakipatikana kituo kimoja cha Ihanda nje kidogo ya mji wa Vwawa na Tunduma lakini siku ya leo hayapo kabisa.
"Tunahofia kununua mafuta mtaani kwani yanaweza kuchanganywa na vitu vingine na hivyo tukaharibu magari ya watu, nasi kupotezi kazi," amesema Edward.