Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maganga Mkurugenzi Mkuu mpya TPSF

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania  (TPSF), Raphael Maganga. Picha na mtandao

Muktasari:

  • Kwa vipindi viwili tofauti Raphael Maganga amewahi kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu ndani ya TPSF.

Dar es Salaam. Baada ya bodi ya wakurugenzi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kumteua Raphael Maganga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo kuanzia Februari mosi, 2024 ameahidi kujenga sekta binafsi shindani na himilivu.

Maganga anachukua nafasi iliyoachwa wazi na John Ulanga, ambaye aliteuliwa kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Biashara za Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Septemba 26, 2023.

Taarifa ya TPSF iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Angelina Ngalula imeeleza Maganga alikuwa akikaimu nafasi hiyo tangu ulipofanyika uteuzi wa Balozi Ulanga.

Maganga mwenye uzoefu na utaalamu katika maendeleo ya sekta binafsi, diplomasia ya uchumi, uwekezaji na biashara, amefanya kazi katika baadhi ya mataifa kama vile Australia, Kenya, China.

Kabla ya kujiunga na TPSF mwaka 2021 akiwa mshauri wa sekta binafsi, amewahi kuwa mwakilishi wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) kwa Tanzania na Burundi.

EABC inajishughulisha na utengenezaji mazingira ya biashara katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumzia uteuzi huo, Maganga amesema sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa Taifa, hivyo anatambua kuwa ana jukumu la kuhakikisha inaendelea kuwa shindani na himilivu.

“Ninalo jukumu kubwa la kuhakikisha sekta binafsi inaendelea kuwa shindani na himilivu, na Tanzania iongoze katika kuwapo kwa mazingira ya biashara kupitia sera bora,” amesema.

Maganga ameahidi kuhakikisha vyama vya biashara vinaratibiwa na vinawezeshwa ipasavyo kuwa chachu ya kuleta maendeleo ya sekta binafsi katika Taifa.




Kabla ya TPSF, Maganga alianzia kazi katika Benki ya AMP Capital kama mshauri wa fedha na uwekezaji kabla ya kuhamia Domain Wealth Services chini ya Westpac Bank, moja ya Benki kubwa nchini Australia.

Pia amewahi kufanya kazi kama mshauri wa uwekezaji katika ofisi binafsi ya Makamu wa Rais mstaafu nchini Kenya, Kalonzo Musyoka mwaka 2015-16 kabla ya kurejea Tanzania na kuwa Mtendaji Mkuu wa Rakestar Group.

Baada ya kutoka Rakestar Group alijiunga na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC).

Maganga, ana Shahada ya Biashara (Uhasibu na Fedha) kutoka Chuo Kikuu cha Monash nchini Australia na Stashahada ya Uzamili ya Ushirikiano wa Kimataifa kutoka Kituo cha Mahusiano ya Kigeni na ni miongoni mwa wahitimu wa kozi fupi ya Capstone 13 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi cha Tanzania (NDC).

Hadi alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa TPSF, Maganga amewahi kuhudumu kama kaimu mkurugenzi kwa vipindi tofauti ndani ya TPSF ikiwemo mwaka 2022 baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Francis Nanai kuachia ngazi.

Nanai aliachia ngazi ndani ya TPSF, Februari 8 mwaka 2022 na hapo Maganga aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo kuanzia Februari 9, 2022.

Baadaye Agosti 7, 2023 Bodi ya Wakurugenzi TPSF ilimteua John Ulanga kuwa mkurugenzi wa taasisi hiyo, akipokea kijiti kutoka kwa Maganga hadi alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Bodi ya wakurugenzi ina imani na maono na uongozi wake katika kuhakikisha kunakuwa na ushindani wa sekta binafsi nchini Tanzania na itaendelea kushirikiana na Maganga. Tunamtakia mafanikio katika majukumu yake mapya,” imeeleza taarifa ya TPSF iliyosainiwa na Ngalula.