Ulanga ateuliwa Mkurugenzi mpya TPSF
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), John Ulanga.
Muktasari:
- Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imemteua John Ulanga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo kuanzia leo Agosti 7, 2023 akichukua nafasi ya Raphael Maganga aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo.
Des Salaam. Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) imemteua John Ulanga kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo kuanzia leo Agosti 7, 2023.
Ulanga anachukua nafasi ya Raphael Maganga ambae alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Taarifa kwa vyombo vya hanari iliyotolewa na TPSF inaeleza kuwa Kabla ya kujiunga TPSF, Ulanga alikuwa akifanya kazi kama Mkurugenzi wa Kikanda wa Trade Mark East Africa (TMEA) ambayo kwa sasa inatambulika kama Trade Mark Africa (TMA), shirika lililojikita kusaidia ukuaji wa biashara Afrika Mashariki.
"Anajiunga TPSF akiwa amesheheni uzoefu na utaalamu mkubwa. Vile vile amefanya kazi kama Makamu wa Rais, Mambo ya nje na Endelevu wa BG Group ambayo ni kampuni kubwa ya mafuta na gesi ukanda wa Afrika Mashariki," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Ulanga ana shahada ya Uhasibu kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam na shahada ya uzamili ya Sera za Maendeleo kutoka chuo cha the Graduate Institute of International and Development Studies, Geneva, nchini Uswisi.
Vile vile ni Mhasibu anaetambulika na bodi ya NBAA na pia ana kibali cha kujihusisha na mambo ya akili bandia.
Moja ya sababu zilizochochea uteuzi wake imetajwa kuwa ari ya kujidhatiti katika mambo mbalimbali ambayo imezaa matunda ya uwepo wake kwenye bodi mbalimbali za kiutendaji.
"Kwa sasa, ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni ya bia ya Serengeti, benki ya KCB Tanzania pamoja na Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki.
Pia Ulanga Ulanga ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAFSUS, mpango uliozingatia kuboresha makazi duni nchini Tanzania.
Ulanga pia ni mjumbe wa bodi ya Wakurugenzu katika kampuni ya Mwananchi Communications Limited.
Akizungumzia uteuzi huo, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula amesema, wana imani na uwezo wa Ulanga katika uongozi na wanatarahia kushuhudia ukuaji zaidi wa taasisi hiyo chini ya uongozi wake.
Kwa upande wake Ulanga anatarajia kutumia ujuzi na uzoefu wake katika kushirikiana na sekta binafsi ili kukuza zaidi taasisi hiyo
"Hii itasaidia kujidhatiti kwenye nafasi yetu kama mwamvuli wa sekta binafsi, yenye nia ya kukuza maendeleo ya sekta binafsi na urahisi wa kufanya biashara Tanzania,” amesema Ulanga.