Magonjwa manne ‘yachomoza’ kambi ya madaktari bingwa Mawenzi

Muktasari:
- Madaktari hao ambao wako 60 wameweka kambi ya siku tano katika hospitali ya Mawenzi, na wanatarajia kuwahudumia zaidi ya watu 2,000 wenye matatizo mbalimbali ya kiafya na kwa leo siku ya kwanza wamejitokeza watu zaidi ya 300.
Moshi. Magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo shinikizo la damu, sukari, magonjwa ya moyo na figo, yametajwa 'kuiteka' kambi ya madaktari bingwa na bobezi wa Rais Samia, ambao wanatoa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi.
Madaktari hao ambao wako 60 wameweka kambi ya siku tano katika Hospitali ya Mawenzi na wanatarajia kuwahudumia zaidi ya watu 2,000 wenye matatizo mbalimbali ya kiafya na siku ya kwanza wamejitokeza watu zaidi ya 300.
Hayo yamebainishwa Desemba 2, 2024 na Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mawenzi, Dk Edna-Joy Munisi wakati madaktari hao, wakiendelea kutoa huduma za matibabu na uchunguzi kwa wananchi waliojitokeza kwenye kambi hiyo iliyoanza Desemba 2 na kutarajiwa kuhitimishwa Ijumaa Desemba 6, 2024.
"Tunaona changamoto kubwa katika magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo shinikizo la damu, sukari na magonjwa ya figo na hiyo changamoto imekuwa ikiongezeka siku kwa siku," amesema Dk Munisi.
Amesema, "Magonjwa haya yamechukua sehemu kubwa ya watu ambao tumesha waona na ambao tumeshawasajili, kwa ajili ya kuhudumiwa na madaktari bingwa na bobezi. Hili ni eneo ambalo tunapaswa kutumia nguvu nyingi tukapeana ufahamu na kuelewa namna ya kuishi ambayo ni bora na kujikinga na magonjwa haya yasiyoambukiza," amesema.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mawenzi, Dk Edna-Joy Munisi.
Aidha Dk Munisi amesema mahitaji ya madaktari bingwa na bobezi bado ni makubwa na kutoa rai kwa wananchi mkoani Kilimanjaro, kutumia siku tano za kambi ya madaktari hao kwenda kupata huduma.
"Uhitaji wa madaktari bobezi na madaktari bingwa bado ni makubwa. Hivyo, serikali imeliona hili na tayari tunayo mikakati mbalimbali ya kuweza kuongeza madaktari hao. Lengo kubwa la kambi hii ya madaktari bingwa hapa Mawenzi ili kuhakikisha huduma za afya za kibingwa na bobezi zinasogea karibu na wananchi na watakaohitajika upasuaji watapata huduma hiyo ndani ya wiki hii,"ameeleza Dk Munisi.
"Kambi hii tuna madaktari bingwa na bobezi wa fani 19, ambazo zinajumuisha madaktari bingwa wa macho, kinywa na meno, upasuaji mkubwa na mdogo, upasuaji wa mifupa, magonjwa ya ndani, magonjwa ya watoto, magonjwa ya kina mama na uzazi, madaktari bingwa bobezi kwa upasuaji wa ubongo, moyo, njia ya mkojo, figo, ngozi na ushauri nasaha kwa maambukizi ya Ukimwi," amesema.
Akizungumza daktari bingwa bobezi wa magonjwa ya ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, Dk Happyness Rabieli amesema mwitikio wa wagonjwa ni mkubwa na wanaendelea na uchunguzi ili kubaini wale ambao wana matatizo na wanaohitaji upasuaji.
Pia, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kunufaika na huduma hizo za kibingwa na bingwa bobezi zinazotolewa ili kuepuka kuwafuata mbali.
Kwa upande wake Mwanaid Ramadhan mmoja wa wagonjwa waliofika kupata huduma katika kambi hiyo pamoja na kupongeza utolewaji wa huduma hizo, ameomba gharama kupunguzwa ili watu wengi zaidi waweze kuzimudu na kunufaika na matibabu hayo ya kibingwa.
"Huduma zinazotelewa hapa ni nzuri na muhimu kwetu, ila changamoto kubwa ni gharama, tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan awezeshe huduma hizi , zitolewe bure ili watu wengi waweze kupata matibabu kwani wengi ni wagonjwa lakini wanashindwa kuzimudu," amesema Ramadhan.
Edith Mosha amesema huduma walizozipata ni nzuri na kuomba madaktari hao kuwafikia wananchi kila mwaka ili kusogeza huduma za kubingwa karibu.
"Tumepata huduma nzuri na kubwa, tunaomba huduma hizi zitolewe mara kwa mara kwani kuna wananchi wengine hawana uwezo wa kuwafuata madaktari bingwa na bobezi na mwingine hajui tatizo linalomsumbua ila akikutana na madaktari hao, anasaidika,"amesema Mosha.
Jackiline George ambaye ni mratibu wa huduma ya madaktari wa Mama Samia Kanda ya Kaskazini amesema huduma hiyo inaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Mawenzi na kilele chake ni Desemba 6, 2024.