Magufuli aacha maagizo matano

Magufuli aacha maagizo matano

Muktasari:

  • Akiwa kiongozi aliyetaka kuona uwajibikaji, Rais John Magufuli alikuwa akitoa maagizo na kuyafuatilia kwa karibu na kabla ya kuugua na hatimaye kufariki dunia, aliacha maagizo matano mazito.
  • Maagizo hayo pamoja na mengine yalitolewa na Rais Magufuli Februari mwaka huu, akiwa katika ziara zake za mwisho alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.

Dar es Salaam. Akiwa kiongozi aliyetaka kuona uwajibikaji, Rais John Magufuli alikuwa akitoa maagizo na kuyafuatilia kwa karibu na kabla ya kuugua na hatimaye kufariki dunia, aliacha maagizo matano mazito.

Maagizo hayo pamoja na mengine yalitolewa na Rais Magufuli Februari mwaka huu, akiwa katika ziara zake za mwisho alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.

Akiwa mkoani Morogoro Februari 11, aliwaagiza viongozi wa mkoa huo kushughulikia kero zilizopo katika soko jipya la Kingalu ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli bila bughudha yoyote.

“Wapo watu wamepewa vizimba hapa kwa kukodishiwa na madalali na baadhi yao ni wafanyakazi wa manispaa. Yupo mmoja wamenitajia anaitwa Aika, kama huyo Aika na hao watumishi wengine wa manispaa wanapenda kazi zao, wazitapike mara moja hizo fedha walizochukua kwa wananchi.

“Nataka uozo uliomo humu kwenye soko, kuanzia leo ukome. Waziri wa Tamisemi, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa wilaya, mkurugenzi na mbunge, mkalishughulikie hili, sitaki kusikia tena mambo ya ovyo hapa,” alisema.

Siku hiyo pia aliwataka Watanzania kuondoa hofu dhidi ya ugonjwa wa corona na kuendelea kutumia njia mbadala za kujikinga na ugonjwa huo kama kujifukizia, huku wakiendelea kuchapa kazi.

Februari 24 baada ya kuzindua daraja la juu la Kijazi na stendi ya mabasi ya Magufuli alitangaza kulivunja jiji la Dar es Salaam kwa sababu halina miradi ya maendeleo linayoitekeleza badala yake madiwani wanachangiwa fedha za kulipana posho.

Alisema haiwezekani kuwa na halmashauri ambayo haina maeneo ya miradi ikaendelea kuwepo na kutengewa bajeti, badala yake alitaka halmashauri moja kati ya tano zilizopo ndiyo ipandishwe hadhi na kuwa jiji.

Jioni ya siku hiyo akaipandisha hadhi halmashauri ya Ilala kuwa jiji, kisha kumteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji, Spora Liana kuwa mkurugenzi wa halmashauri ya Kinondoni.

Kiongozi huyu alikuwa mtetezi wa wamachinga na wafanyabiashara ndogondogo, alidhihirisha hilo hata siku alipozindua stendi ya Magufuli.

Alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo kuhakikisha machinga wanafanya biashara zao bila kubughudhiwa. Februari 25 kiongozi huyo alizindua soko la Kisutu na ofisi za African Media Group na kuelekeza waliokuwa viongozi wa halmashauri ya Ilala kushika hatamu ya kuongoza jiji.

Siku hiyo aliitaka pia Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuacha kuwakadiria wafanyabiashara kodi kubwa na kueleza miradi ya ujenzi wa masoko na vituo vya mabasi ni mikakati ya Serikali kubadilisha mazingira ya Tanzania.

Ziara yake ya mwisho Rais Magufuli ilikuwa wilayani Temeke alikozindua majengo ya Chuo cha Taaluma ya Polisi na kiwanda cha ushonaji sare za jeshi hilo. Hapo alimuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene kuhakikisha wastaafu wa jeshi la polisi wanalipwa stahiki zao ndani ya wiki moja.

Alitoa agizo hilo baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro kumuomba kusaidia wastaafu wa jeshi la polisi kulipwa stahiki zao baada ya kustaafu. Siku hiyo pia aliiagiza Takukuru kuchunguza njia zilizotumika kutolewa kwa mkopo wa Sh19 bilioni kwa halmashauri ya manispaa ya Temeke uliotumika kulipa fidia wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya DMDP.

Maelekezo hayo yalikuja kutokana na kutoridhishwa na ombi la mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave aliyeiomba Serikali kusaidia kulipa deni hilo ambalo limekuwa mzigo kwao.

Kilave alieleza wanalazimika kutumia fedha za makusanyo ya ndani takribani Sh4.8 bilioni kila mwaka kulipa deni hilo, jambo linalokwamisha utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo kwenye halmashauri hiyo.