Magufuli aimba na kucheza wimbo wa Stamina na Profesa J

Magufuli aimba na kucheza wimbo wa Stamina na Profesa J

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli ameomba kupigiwa wimbo wa Baba wa msanii Stamina aliyemshirikisha mbunge wa zamani wa Mikumi (Chadema),  Joseph Haule maarufu Profesa J na kubainisha kuwa una ujumbe mzuri.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ameomba kupigiwa wimbo wa Baba wa msanii Stamina aliyemshirikisha mbunge wa zamani wa Mikumi (Chadema),  Joseph Haule maarufu Profesa J na kubainisha kuwa una ujumbe mzuri.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 25, 2021 katika uzinduzi wa studio za Channet Ten na Magic FM jijini Dar es Salaam.

Wimbo huo unamzungumzia kijana anayehangaika kutafuta maisha na kumsema baba yake kwamba hali aliyonayo inatokana na mzazi wake huyo kushindwa kutafuta fedha wakati wa ujana wake, mzazi huyo kumjibu jinsi alivyohangaika kumlea licha kuwa si mwanaye wa kumzaa lakini alihakikisha anapata mahitaji yote.

Akiwa katika studio ya Channel Ten  baada ya kuzindua kwa kubonyeza kitufe, kiongozi huyo huku akitazama televisheni kubwa ukutani alianza kuhoji kama akitaka kupigiwa muziki itawezekana, na kujibiwa na aliyekuwa akitoa maelezo ya studio hizo kuwa jambo hilo linawezekana.

“Nipigieni ule wimbo wa Profesa Jay ambao alikuwa anaongea na baba yake, naongea na wewe,” amesema Rais Magufuli akisema katika wimbo humo mzee alimpa majibu mazuri mwanaye.

Wakati akisikiliza na kuangalia video hiyo kupitia televisheni hiyo alionekana kuvutiwa na alianza kuimba kwa sauti ya chini huku akitingisha kichwa na alisikiliza wimbo huo kwa takribani dakika mbili.

 “Huu wimbo una meseji lakini hongereni sana,” amesema kiongozi mkuu huyo wa nchi.