Mahakama kutoa uamuzi pingamizi la Mbowe na wenzake

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kesho Jumatano Septemba 1, 2021 itaamua pingamizi la Mbowe na wenzake kama mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi yao ama la.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kesho Jumatano Septemba 1, 2021 itaamua pingamizi la Mbowe na wenzake kama mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi yao ama la.


Mbowe na wenzake wameipinga mahakama hiyo kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao kwa mashtaka ya ugaidi na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Ugaidi kesi yao inapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu ya kawaida na si hiyo ambayo ni Divisheni Maalum.

Serikali imepinga hoja hizo ikidai kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba 3 ya Mwaka 2016 makosa yaliyoko kwenye Sheria ya Ugaidi yaliwekwa kwenye Sheria ya Uhujumu Uchumi na kwamba kwa hali hiyo mahakama hiyo ya ufisadi ina mamlaka ya kusikiliza mashtaka yao.

Jaji Elinazer Luvanda baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumatano asubuhi atakapotoa uamuzi.