Prime
Mahakama ya Rufani ilivyohitimisha miaka 13 ya kesi ya bomu Kanisa Katoliki Olasiti
Muktasari:
- Mahakama ya Rufani nchini imehitimisha moja ya kesi zilizotikisa nchi kwa kuthibitisha hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa kwa watu sita kwa makosa ya mauaji na ugaidi kufuatia shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti jijini Arusha mwaka 2013.
Arusha. Safari ya miaka 13 ya kutafuta haki kufuatia shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki jijini Arusha, lililosababisha vifo vya waumini watatu na wengine zaidi ya 50 wakijeruhiwa, imehitimishwa na Mahakama ya Rufani nchini baada ya kuthibitisha hukumu dhidi ya watu sita waliokuwa wakisaka nafuu kupitia rufaa.
Katika tukio hilo lililotokea Mei 5, 2013 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti jijini Arusha, Balozi wa Papa hapa Tanzania, Askofu Francisco Padilla na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Josephat Lebulu walinusurika.
Wakati mamia ya waumini waliokuwa wamekusanyika katika Kanisa hilo, bomu lililopuka katikati ya umati huo na kubadili ghafla hali ya shangwe na kuwa majonzi. Ilielezwa kuwa utepe ulipokuwa ukikatwa na viongozi hao wakuu, bomu hilo lilirushwa.
Katika hukumu yake, Mahakama ya Rufani imeeleza Mahakama Kuu haikukosea ilipowatia hatiani Abashari Omary, Yusuph Hutta, Ramadhani Waziri, Abdul Juma, Kassim Ramadhan na Japhari Lema kwa makosa ya mauaji, kutenda vitendo vya kigaidi na matumizi ya mali kwa kutenda vitendo vya kigaidi.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo ambao wametoa hukumu hiyo jana Jumatatu Julai 27, 2026 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao ni Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Lameck Mlacha.
Majaji hao wamesema ushahidi uliowasilishwa ulithibitisha makosa hayo bila kuacha shaka yoyote ya msingi hivyo hakuna sababu ya kuingilia hukumu ya Mahakama Kuu.
Jaji Mwandambo amesema Mahakama imefuta hatia ya kosa la kula njama ya kutenda vitendo vya kigaidi, ikieleza kuwa kisheria kosa hilo haliwezi kusimama pale ambapo kosa la ugaidi lililokusudiwa tayari limethibitika na kutekelezwa.
“Katika mambo yote yaliyobaki, rufaa inakataliwa na hukumu za mauaji, kutendo vitendo vya kigaidi na matumizi ya mali kwa kutenda vitendo vya kigaidi zinathibitishwa,” imeeleza hukumu hiyo.
Rufaa hiyo ya jinai namba 93, 2024 ilikatwa warufani hao na dhidi ya Jamhuri, waliokuwa wakipinga hukumu iliyotolewa Disemba 12, 2023 katika kesi ya jinai namba 32 ya mwaka 2023 iliyotolewa na Jaji John Nkwabi.
Jaji Mwandambo amesema baada ya Mahakama kuchambua sababu zote saba za rufaa zilizowasilishwa na warufani, Mahakama imebaini hazikuwa na msingi wa kubatilisha hukumu ya Mahakama Kuu.
Msingi wa rufaa
Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi, Mei 5, 2013 waumini walikuwa wamekusanyika katika kanisa hilo kwa ajili ya uzinduzi wa parokia hiyo mpya ambapo baada ya kutokea tukio hilo, uchunguzi ulifanywa na watu 10 walikamatwa na kushtakiwa mwaka 2014 ambapo mmoja kati yao alifariki kabla ya kuanza kwa kesi na wengine watatu waliachiwa huru wakati wa hukumu.
Katika kesi hiyo walishtakiwa kwa makosa mbalimbali ambayo ni ya kula njama ya kutenda vitendo vya ugaidi, kutenda vitendo vya ugaidi, mauaji na kutumia mali kuwezesha kutendeka kwa vitendo vya kigaidi.
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa kabla ya shambulio hilo kulifanyika mkutano wa kupanga tukio nyumbani kwa mmoja wa washtakiwa (Ramadhani) huku taarifa kuhusu ratiba ya sherehe za kanisa zikidaiwa kutolewa na Japhari.
Upande wa mashtaka ulitegemea zaidi maelezo ya onyo ya washtakiwa ambayo yalifutwa wakati wa kesi ya msingi, ushahidi wa mashahidi, vielelezo vya uchunguzi na ushahidi wa kitabibu kuthibitisha mashitaka hayo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mahakama Kuu iliwatia hatiani warufani kwa makosa ya mauaji, kutenda makosa ya ugaidi, kutumia mali kwa kutenda vitendo vya ugaidi na kula njama ya kutenda ugaidi na kosa la mauaji, ambapo walihukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Sababu za rufaa
Wakiwa hawajaridhishwa na hukumu hiyo,watu hao walikata rufaa wakiwa na sababu sita, wakiiomba Mahakama ya Rufani ibatilishe hukumu na adhabu zilizotolewa na Mahakama Kuu wakidai kuwa zilitokana na makosa ya kisheria na kiutaratibu.
Sababu hizo ni pamoja na Mahakama Kuu ilikosea kisheria kuwatia hatiani na kuwahukumu wakati upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi yao bila kuacha shaka yoyote ya msingi, Mahakama haikufanya tathimini ya kina ya ushahidi uliowasilishwa na pande zote kabla ya kuwatia hatiani.
Nyingine ni Mahakama ilikosea kuwatia hatiani na kuwahukumu kwa msingi wa kesi ya mashtaka iliyojaa makosa ya kiutaratibu, Mahakama Kuu ilikosea kuwahukumu bila kuzingatia ushahidi wa upande wa utetezi.
Walidai kuwa Mahakama ilikosea kuwatia hatiani na kuwahukumu kwa msingi wa vielelezo visivyokubalika kisheria na ilikosea kuwahukumu kwa msingi wa maelezo ya ungamo ambayo yalikataliwa na kufutwa.
Katika sababu ya saba, walidai Mahakama ilikosea kwa kuwatia hatiani kwa wakati mmoja kwa kosa la kula njama ya kutenda vitendo vya ugaidi na kosa la kutenda vitendo hivyo, wakisema kisheria makosa hayo hayawezi kusimama pamoja pale ambapo kosa la msingi tayari limethibitika.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, warufani hao waliwakilishwa na mawakili tisa huku upande wa mjibu rufaa ukiwakilishwa na mawakili wa Serikali waandamizi watano.