Sita wahukumiwa kifo mlipuko Kanisa la Olasiti

Muktasari:

  • Mahakama Kuu yaawachia huru watatu kati ya tisa, ni tukio la mwaka 2013. Lilitokea mbele ya Balozi wa Papa nchini Tanzania.

Moshi/Arusha. Mahakama Kuu, imewahukumu adhabu ya kifo, watu sita kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya ugaidi, baada ya kuthibitika ndio waliorusha bomu ndani ya Kanisa Katoliki na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine kujeruhiwa.

Katika tukio hilo lililotokea Mei 5,2013, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi jijini Arusha, Balozi wa Papa hapa Tanzania, Askofu Francisco Padilla na Askofu Mkuu, Josephat Lebulu walinusurika.

Sherehe hizo zilikuwa zimehudhuriwa pia na mapadri na watawa kutoka mashirika mbalimbali ya Jimbo Kuu Katoliki la Arusha na waumini. Wakati Balozi wa Papa na Askofu Lebulu wamesimama kukata utepe ndipo bomu hilo lilirushwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha wakati huo, Liberatus Sabas alilielezea tukio hilo kuwa ni la kigaidi hasa kutokana na kumlenga Balozi wa Papa. Alisema aliyelirusha alitokea nyuma ya kanisa hilo la ghorofa na mlipuko huo ulisababisha  watu 60 kujeruhiwa.

Padri Moses Mwaniki aliyekuwa ameshika maji ya baraka yaliyotumika kubariki kanisa, alinukuliwa akisema kilichofanya bomu lisimfikie Balozi Padilla ni kwamba lilianguka mgongoni mwa mmoja wa waumini.

Kwa upande wake, msemaji wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Padri Festus Mangwangi amesema aliyerusha bomu hilo alishuhudiwa na mtoto mdogo aliyekuwa kanisani ambaye alieleza muhusika alikuwa amevaa kanzu nyeupe.

“Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto, huyo mtu alikuwa amevaa kanzu nyeupe na koti la mvua la rangi ya kahawia na alikimbia baada ya kulirusha katikati ya watu huku akiita mwizi, mwizi kama vile anamkimbiza mwizi,” alisema.

Kutokana na tukio hilo ambalo lilizua taharuki si kwa waumini tu wa Kanisa Katoliki nchini na duniani, lakini kwa Watanzania pia, vyombo vya ulinzi na usalama vilifanya uchunguzi na kukamatwa washukiwa kadhaa.

Hukumu ya kunyongwa

Kesi ya tukio hilo ambayo ilitumia miaka 10 kuanzia mwaka 2013 lilipotokea ilihitimishwa jana Desemba 11, 2023 na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, John Nkwabi ambaye amewahukumu adhabu ya kifo washtakiwa sita na kuwaachia huru watatu.

Ingawa haikuelezwa kama waliohukumiwa adhabu ya kifo ni masheikh, lakini taarifa zinazosambaa mitandaoni leo Desemba 13,2023  zinawataja kama ni masheikh na mmoja ni Jaafar Hashima Lema, aliyekuwa imamu mkuu wa Masjid Quba.

Wengine waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Abashari Hassan Omari, Yusuph Ally Huta, Kassim Idrisa, Abdul Hassan Juma na Ramadhan Hamad Waziri. Washtakiwa wana haki ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Walioachiwa huru ni Abdulrahman Jumanne, Abdul Mohamed Wagoba na Amani Mussa Pakasi, ambaye amerejeshwa mahabusu kwa maelezo anakabiliwa na kesi nyingine ya ugaidi ambayo hukumu yake inatarajiwa kutolewa Ijumaa Desemba 15,2023.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Nkwabi, amesema upande wa mashtaka umeleta  ushahidi wa kutosha kuthibitisha pasipo kuacha shaka yoyote dhidi ya washtakiwa hao sita kati ya tisa, kuwa ndio waliofanya tukio hilo la kigaidi.

Hii ni baada ya Mahakama kusikiliza ushahidi wa mashahidi 39 na kupokea vielelezo 37 vya upande wa mashtaka kuthibitisha makosa 47 yaliyokuwa yakiwakabiliwa, yakiwamo ya kula njama, ugaidi, kujaribu kuua na mauaji.

Kuhusu washtakiwa watatu waliochiwa, Jaji ameeleza kuwa amejiridhisha ushahidi wa Jamhuri haujathibitisha pasipo kuacha shaka makosa dhidi yao, hivyo Mahakama ikaona hawana hatia na kuwaachia huru.

Shauri hilo lilianza kusikilizwa mfululizo Oktoba 2,2023 hadi  Novemba kabla ya kuahirishwa kwa ajili ya hukumu iliyosomwa juzi na Jaji Nkwabi.

Katika utetezi, washtakiwa hao wakijitetea wenyewe bila kuwa na mashahidi wengine.