Mahakama ya Rufani yabariki Waziri kulipwa fidia Sh1.2 bilioni

New Content Item (1)

Muktasari:

  • Waziri Hamad Masauni na wenzake waliishtaki Kampuni ya Wings na wakurugenzi wake kwa kukiuka makubaliano ya ununuzi wa hisa za Kampuni ya Alliance Cargo.

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imebariki uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuitaka Kampuni ya Wings Flight Services Limited, kuilipa fidia ya Dola 500,000 za Marekani (Sh1.27 bilioni) Kampuni ya Alliance Cargo Handling Limited inayomilikiwa na  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na wenzake wawili.

Mahakama Kuu imeiamuru Kampuni ya Wings Flight kuilipa fidia Kampuni yab Alliance Cargo Handling Limited ya Waziri Masauni na wenzake Arthur Mosha na Juma Mabakila kwa kukiuka mkataba wa makubaliano ya ubia na ununuzi wa hisa za kampuni yao.

Mahakama ya Rufani imeibariki hukumu hiyo ya Mahakama Kuu, katika hukumu yake ya rufaa iliyoikata Wings Flight mahakamani hapo kupinga hukumu na amri za Mahakama Kuu, baada ya kukataa hoja za warufani waliowakilishwa mawakili Deogratius Kiritta na Reginald Martin.

Badala yake imekubaliana na hoja za wajibu Rufani, Masauni na wenzake kupitia wakili wao Alex Mgongolwa.

Hukumu hiyo ya Februari 26, 2024 iliyotolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo Jacobs Mwambegele (kiongozi wa jopo) Issa Maige na Gerson Mdemu, tayari imechapishwa katika tovuti ya Mahakama ya Tanzania.


Chanzo cha mgogoro

Septemba 16, 2009 Masauni na wenzake walisajili kampuni yao ya Alliance Cargo Handling  na

Februari 7, 2011 waliingia mikataba ya makubaliano na Kampuni ya Paradise Group Co. Limited chini ya wakurugenzi wake Mohamed Abdillah Nur na Ummul Kheri Mohamed ya ubia na ununuzi wa hisa.

Paradise ilinunua hisa 3,200,000 za Alliance Cargo Handling  sawa na asilimia 65.

Katika mikataba hiyo ya makubaliano, Paradise Group Co. Limited ilipaswa iweke Dola 4 milioni za Marekani (Sh10.2 bilioni) katika akaunti ya pamoja ya kampuni hizo, kwa ajili ya hisa hizo.

Hivyo katika muundo huo, Masauni na wenzake wakawa wanahisa wadogo ndani ya Alliance Cargo Handling  baada ya kubakiwa na hisa asilimia 35 tu.

Wakati mchakato huo ukiendelea, wakurugenzi hao wa Paradise Group Co. Limited, bila kina Masauni kuwa na taarifa, walitangaza kuwa Wings Flight Services Limited ni muungano na Paradise na Alliance Cargo Handling, iliyobadilishwa baadaye na kuwa Africa Flight Services.

Kesi ya msingi

Mwaka 2021, Masauni na wenzake walifungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, dhidi ya Nur na Mohamed (wakurugenzi wa Wings), Kampuni ya Wings na Africa baada ya kupata kibali cha Mahakama.

Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 33/2021, Masauni na wenzake waliwalalamikia wadaiwa hao (Nur, Mohamed na Wings) kuwa walifanya vitendo vilivyokiuka mkataba wa makubaliano.

Vitendo hivyo ni pamoja na kudhibiti masuala ya Africa Fligh kwa kubadili jina la kampuni kutoka Alliance Cargo kuwa Africa Flight na kukopa pesa benki Dola 3 milioni za Marekani.

Pia waliwalalamikia wadaiwa kutokuwapatia gawio na kutokuwahusisha katika mambo yote ya Africa Flight.

Wadaiwa katika majibu yao walipinga kukiuka mikataba hiyo ya makubaliano, wakadai kuwa kila walichokifanya walizingatia mikataba hiyo, sheria ya kampuni na sheria kwa jumla na hawakufanya jambo lolote lenye madhara kwa kampuni ya ubia, Africa Flight.

Jaji Stephen Magoiga katika uamuzi wake wa Julai 8, 2022, alikubaliana na madai na hoja za kina Masauni kuwa alithibitisha madai yao baada ya kubaini kuwa mdaiwa wa tatu (Wings) alikiuka makubaliano.

Jaji Magoiga alisema Kampuni ya Wings Flight chini ya uongozi wake, Nur na Mohamed, ilikiuka makubaliano ya muungano wa ununuzi wa hisa kwa kushindwa kuweka kwenye akaunti Dola 4 milioni za Marekani kama walivyokubaliana.

Hivyo, alisema kushindwa kutekeleza takwa hilo kulisababisha makubaliano hayo kuwa batili tangu mwanzo kwa kutokuweka kiasi hicho cha pesa kwenye akaunti ya pamoja.

Jaji Magoiga aliiamuru Kampuni ya Wings kurejesha hisa zote asilimia 65 ilizojipatia katika kampuni ya Africa Flight (awali Alliance Cargo) na zigawanywe kwa wanahisa wadogo (Masauni na wenzake) kwa uwiano sawa.

Pia, Jaji Magoiga aliamuru wadaiwa wailipe fidia ya Dola 500,000 za Marekani Kampuni ya Africa Flight (Alliance Cargo).

Pia, alisema jina la Kampuni ya Alliance Cargo Handling Limited lilibadilishwa kuwa Africa Flight Services isivyo halali.

Hivyo, alitoa amri kwa wadaiwa hao ikiwaelekeza kuwasilisha amri hiyo ya mahakama kwa Msajili wa Kampuni, ikimuelekeza huyo msajili wa kampuni kulifuta jina la Africa Flight Services na kurejesha jina la awali la Alliance Cargo Handling Company Limited na wadaiwa kulipa gharama za kesi hiyo.

Wadaiwa hao hawakuridhika na uamuzi huo wa Mahakama, hivyo walikata rufaa Mahakama ya Rufani lakini Mahakama hiyo katika hukumu yake imetupilia mbali sababu zote za rufaa hiyo ikieleza hazina msingi, badala yake imekubaliana na hoja za wakili wa kina Masauni, kuwa Mahakama Kuu ilikuwa sahihi katika uamuzi wake na amri zote ilizozitoa zilizingatia sheria.

“Kama tulivyodokeza, hata mabadiliko ya jina la kampuni yalifanywa bila wajibu rufani kuhusishwa, nini kingine zaidi tunahitaji zaidi ya huu ushahidi?” imehoji Mahakama ya Rufani baada ya kujadili hoja za pande zote na kuhitimisha

 “Kwa kusema hayo yote, ni mtizamo wetu imara kwamba rufaa hii haina ustahilifu. Hivyo, uamuzi na amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara unakubaliwa. Matokeo yake rufaa inakataliwa kwa gharama.”