Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yaamuru OC-CID, DAS kumlipa raia Sh10 milioni

Katibu Tawala Wilaya ya Babati, Mkoani Manyara, Halfan Matipula

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, John Kahyoza  haoni ushiriki wa Serikali katika matendo hayo (yaliyofanywa na mkuu wa upelelezi na katibu tawala wilaya) kwa kuwa kiongozi anapovunja sheria anakuwa amejitoa katika kutekeleza majukumu ya Serikali bali ni utashi binafsi

Babati. Mahakama Kuu Tanzania, imemhukumu mkuu wa upelelezi (OC-CID) Wilaya ya Babati, Richard Mwaisemba na Katibu Tawala (DAS) wa wilaya hiyo, Halfan Matipula, kumlipa raia mwema Sh10 milioni kwa kumweka mahabusu bila uhalali.

 Katika kesi yake ya madai namba 16 ya mwaka  2023, Lawrence Tara aliyesimama mwenyewe kortini alifungua kesi dhidi ya Mwaisemba na Matipula pamoja na kumuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiwadai wote fidia ya Sh50 milioni.

Hata hivyo, katika hukumu yake iliyopatikana Juni 11,2024 katika mtandao wa Mahakama, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, John Kahyoza amewaamuru Mwaisemba na Matipula  kumlipa mwananchi huyo, Sh5 milioni kila mmoja.

Jaji alisema haoni kwa namna yoyote ushiriki wa Serikali katika matendo hayo ( yaliyofanywa na mkuu wa upelelezi na katibu tawala wilaya) kwa kuwa kiongozi anapovunja sheria anakuwa amejitoa katika kutekeleza majukumu ya Serikali bali ni utashi binafsi.

Hukumu hiyo inaongeza orodha ya wateule wa Rais ambao Mahakama iliwaamuru kulipa fidia kutokana na kutoa amri zilizosababisha wananchi kukamatwa na kuwekwa mahabusu.

Januari 2023, Jaji Lameck Mlacha wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, aliamuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu kumlipa Marry Otaru (70) fidia ya Sh10 milioni na Serikali kulipa Sh90 milioni, kwa kumweka mahabusu bila uhalali.

Hii ni baada ya Jaji Mlacha kutamka kuwa amri ya Buswelu kumweka mahabusu kwa siku tano, Marry Otaru bila kumfungulia mashitaka yoyote ilikuwa ni haramu.

Desemba 2022, Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora ilimwamuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini, Komanya Kitwala kumlipa Alexander Ntonge, fidia ya Sh80 milioni kwa kutoa amri ya kukamatwa kwake na kudhalilishwa na polisi.


Nini walichofanya mkuu wa upelelezi, katibu tawala wilaya

Kwa mujibu wa hukumu ya Jaji Kahyoza, maelezo ambayo hayabishaniwi ni kuwa Tara alikamatwa na polisi Juni 13,2020 na kuwekwa mahabusu kwa siku tisa hadi Juni 22 alipoachiwa kwa dhamana na hakufunguliwa mashitaka yoyote.

Katika ushahidi wake mbele ya Mahakama, Tara alieleza kuwa Juni 12,2020, alipigiwa simu na mdaiwa wa kwanza (mkuu wa upelelezi) akitakiwa kufika ofisini kwake siku inayofuata na alikwenda saa 7:00 mchana akiwa na Wakili Lister Tadei.

Mkuu wa upelelezi alimjulisha kuwa anatuhumiwa kutenda kosa la uchochezi hivyo anatakiwa kuwekwa mahabusu, lakini mwananchi huyo akataka apewe maelezo ya kosa alilolitenda na kupewa dhamana, lakini hakupewa na akawekwa mahabusu.

Licha ya wakili wake kufanya jitihada za mara kwa mara kuomba mteja wake apewe dhamana haikuwezekana, Juni 15,2022 makachero walitaka kumchukua maelezo mbele ya wakili wake mwingine, John Mwita ila nalo halikuwezekana.

Juni 17 2022  Mkuu wa upelelezi huyo akamtaka mwananchi huyo apelekwe ofisini kwake na alimjulisha kuwa anafanya utaratibu ili aweze kudhaminiwa kwa masharti kama ataacha kuongea ongea, masharti ambayo mwananchi huyo aliyagomea.

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Babati. Picha na Joseph Lyimo

Wakati mpelelezi akikamilisha dhamana ofisini kwake, mkuu wa upelelezi aliingia katika ofisi hiyo na kumwamuru mpelelezi huyo amrudishe Tara mahabusu na kumtaka mpelelezi waongozane kwenda ofisini kwa mkuu wa mkoa wa Manyara.

Siku hiyo hiyo ya Juni 17,2022 kwenye saa 9:30 mchana, ofisa mmoja wa polisi aliyetajwa kwa jina moja tu la Said, alitoa maelekezo Tara apelekwe ofisi ya mkuu wa upelelezi kwa mahojiano na mbele ya wakili Mwita, alipewa kwanza barua aisome.

Barua hiyo kwa mujibu wa ushahidi uliochambuliwa na Jaji, ilikuwa imeandikwa na Christna Martin ambaye alikuwa shahidi wa nne wa Tara, kwenda kwa Rais, akilalamikia kukamatwa mara kwa mara kwa mumewe kunakofanywa na mkuu wa upelelezi.

Katika barua hiyo, alilalamikia amri ya mkuu wa mkoa kuzuia kufanyika kwa mnada wa kuuza shamba, ulioamriwa na Mahakama na kutaka shamba hilo lirejeshwe kwa mmiliki wa awali, jambo ambalo lilikuwa ni kukiuka amri ya Mahakama.

Tara katika mahojiano hayo alijibu kuwa hakumbuki kama yeye ndio aliandaa (draft) barua hiyo na kwamba hata kama ni yeye aliyeiandika, haikuwa ni kosa kwa kuwa ufahamu wake, mkuu wa mkoa ndiye anakiuka sheria kutokana na maagizo yake.

Baada ya hapo, aliamriwa arejeshwe mahabusu lakini wakati anarudishwa mahabusu alifanikiwa kuonyeshwa kitabu cha kumbukumbu kituoni hapo na ndipo alipobaini kuwa kumbe mlalamikaji katika kesi hiyo alikuwa ni Matipula.

Katika madai yake, katibu tawala wilaya anadaiwa kueleza kuwa Tara alikuwa akiwachochea wananchi wagomee amri ya halali ya mkuu wa Mkoa wa  Manyara na Juni 19 2022 saa 3:00 asubuhi, alitolewa mahakamani pamoja na watuhumiwa wa kesi nyingine.

Kwa mshangao wake, hakufikishwa mbele ya hakimu yeyote na kusomewa mashitaka na ilipofika saa 8:00 mchana, maofisa wa polisi walimchukua pamoja na washitakiwa wengine hadi Gereza la Babati, akarudishwa tena mahabusu polisi.

Juni 22 2022, alipomuuliza mkuu wa kituo cha polisi (OCS) Babati kwa nini anashikiliwa mahabusu kwa siku 9 mfululizo, alimjibu kuwa hayo yalikuwa ni maagizo ya mkuu wa upelelezi, hapo ndipo mkuu huyo wa kituo cha polisi  alipompigia simu (mkuu wa upelelezi), Mwaisemba kumjulisha malalamiko hayo ya Tara.

Jibu la Mwaisemba lilikuwa ni kwamba ataachiliwa kwa dhamana siku hiyo na kweli aliachiwa na kutakiwa kuripoti mara moja kwa mwezi na baadaye aliambiwa aendelee na shughuli zake na endapo kutakuwa na jambo atapigiwa kuitwa.


Utetezi wao ulivyokuwa

Katika utetezi wake kortini, Mwaisemba aliyekuwa mdaiwa wa kwanza, alikanusha kuahidi kumpa dhamana Tara endapo atafunga mdomo na pia akakana kuagiza apewe dhamana, bali alipewa baada ya kwenda kumuona mkuu wa kituo.

Hata hivyo alikiri kufahamu barua kwenda kwa Rais ambayo mdai aliirejea na kwamba aliiona kwa mara ya kwanza Jijini Arusha alipokwenda mbele ya Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo shahidi wa 4 alikuwa anamlalamikia mkuu wa mkoa.

Katika malalamiko yake, shahidi Christna Martin alikuwa amelalamika mbele ya Tume kuhusiana na matumizi mabaya ya mkuu wa mkoa wa kati huo na pia alilalamika kuwa hajatajwa lakini alikuwa akitumia polisi kumnyanyasa mumewe.

Alijitetea kuwa yeye alipokea malalamiko kutoka kwa katibu tawala Wilaya ya Babati na kuyawasilisha Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) ambao waliwaelekeza wafanye uchunguzi kwa vile wakati huo kwa ushahidi uliokusanywa, ulikuwa hautengenezi kosa lolote.

Alikanusha pia kutoa maneno kuwa Tara alikamatwa na kuwekwa mahabusu kutokana na maelekezo kutoka juu na kuiomba Mahakama ipuuze madai hayo na kwamba mdai anafahamu fika nani alikuwa nyuma ya kukamatwa kwake.

Kwa upande wake, katibu tawala  wilaya Matipula alijitetea kuwa yeye kama mtu binafsi, hakumlalamikia mdai na wala hafahamu kama aliwekwa mahabusu polisi kinyume cha sheria ama la na kwamba kulikuwa hakuna namna ya kufahamu hilo.


Alichokisema Jaji Kahyoza

 Jaji alisema ni jambo lisilobishaniwa kuwa Juni 12,2022, mdaiwa wa kwanza (mkuu wa upelelezi) alimwita mdai ofisini kwake na kwamba alipofika siku iliyofuatwa alikamatwa na kuwekwa mahabusu hadi Juni 22, 2022 alipoachiwa kwa dhamana ya polisi.

Kuhusu kama kuwekwa kwake mahabusu kulikuwa ni halali, Jaji alisema imethibitishwa kuwa alikuwa mahabusu kwa siku 9 na kwamba haoni sababu ni kwanini alikamatwa kwani tuhuma alizokamatwa zilikuwa hazitengenezi kosa.

“Moja, kuandika barua ya malalamiko kwenda kwa Rais haikuwa ndio kupinga maagizo ya RC (mkuu wa mkoa), pili hakuna ushahidi wowote kama mdai ndiye aliyeandika barua kwa kuwa haina Saini yake au kushawishi watu kuandamana,”alisema Jaji.

Katika sababu ya tatu, Jaji akasema hata kama Mahakama ingeamini kuwa Tara aliandika barua kwenda kwa Rais kwa niaba ya Christina Martin, hilo haliwezi kuwa kosa la jinai la kusababisha mtu akamatwe kwa tuhuma za jinai.

Jaji alisema sheria iko wazi kuwa kumkamata au kumuita mshukiwa kwa mahojiano inaruhusiwa na sheria na kungekuwa hakuna tatizo lolote kama mkuu wa upelelzi angemuita mdai, kumhoji na kumchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa jaji, ingawa mdaiwa wa tatu (katibu tawala wilaya) alikuwa na wajibu wa kutoa taarifa polisi kuhusiana na kutendeka kwa kosa la jinai, lakini katika kesi hiyo kulikuwa hakuna kosa lolote lililotendeka wala kuwepo dhamira ya kutenda kosa.

“Ninamuona mdaiwa wa tatu ambaye ndio alianzisha mchakato huu na mdaiwa wa kwanza ambaye baada ya kumkamata mdai alimweka mahabusu kwa siku tisa kuwa walimkamata na kumweka mahabusu kinyume cha sheria,”alisema Jaji.

Kutokana na msimamo huo na katika hukumu yake aliyoitoa Mei 9, 2024, Jaji amewaamuru mkuu wa upelelezi na katibu tawala kila mmoja kumlipa mdai fidia ya Sh5 milioni na gharama za kesi hiyo.