Mahakama yaitupa kesi ya waumini EAGT wanaogombea mali

Muktasari:

Mahakama yasema kesi haikufunguliwa sawasawa mahakamani.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya mgogoro wa umiliki wa mali za Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) baina ya makundi mawili ya waumini wanaovutana.

 Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa kesi hiyo haikufunguliwa sawasawa mahakamani hapo kutokana na kufunguliwa kama kesi ya uwakilishi (wachache kuwawakilisha walio wengi) bila kibali cha Mahakama.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Butamo Phillip, Aprili 12, 2024 kutokana na hoja iliyoibuliwa na Mahakama yenyewe, iwapo kesi hiyo ilikuwa imekidhi kuwa kesi ya uwakilishi na uhalali wake kuwepo mahakamani.

Jaji Phillip katika uamuzi wake amekubaliana na wakili wa wadaiwa Andrew Miraa, kwa kuwa kesi ilifunguliwa kama kesi ya uwakilishi bila kuwa na kibali cha Mahakama imekiuka Amri ya 1, Kanuni ya 8 ya Kanuni za Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC).

“Msimamo wa kisheria ni kwamba upande unaokusudia kufungua kesi ya uwakilishi lazima uombe na upate kibali cha Mahakama na ni majina machache tu ya wadaiwa ndiyo yatakayoonekana kwenye hati ya madai na kusaini sehemu ya uthibitisho wa madai,” amemesema Jaji Phillip na kuamuru:

“Kwa kuwa Wakili Kachenje (wa wadai) amekiri hoja iliyoibuliwa na Mahakama hii, kuwa kesi hii iko mahakamani isivyo sawasawa, hivyo haina ustahilifu, ninakubaliana na wakili Miraa (wa wadaiwa) kuwa kesi hii inapaswa kutupiliwa mbali. Hivyo ninaitupilia mbali kesi.”

Jaji Phillip amesema kwa kuwa kesi imetupiliwa mbali kutokana na hoja iliyoibuliwa na Mahakama, haitoi amri ya gharama za kesi kwa upande wa wadai (kuwalipa wadaiwa) bali kila upande utabeba gharama zake.

Kesi hiyo ilitokana na mgogoro wa waumini wa kanisa hilo ulioibuka mwaka 2016 kutokana na tofauti na kutokuelewana miongoni mwao, hatimaye kugawanyika katika makundi mawili ambayo awali yalikuwa yakiabudu kwa pamoja ndani ya kanisa hilo lililosajiliwa na Msajili wa Jumuiya.

Baadaye kuliibuka ugomvi kuhusu matumizi na umiliki wa mali.

Hatua mbalimbali zilichukuliwa kusuluhisha mgogoro huo, ukiwemo mkutano ulioitishwa na Msajili wa Jumuiya, lakini hazikuzaa matunda.

Julai 13, 2022, wadaiwa waliwaandikia barua wadai wakiwatishia na kuwapa muda wa miezi mitatu kuanzia tarehe ya barua hiyo hadi Oktoba 20, 2022 ama waombe radhi kwa Askofu Mwakipesile na kuendelea kufanya kazi chini yake au wajiondoe kutoka ndani ya kanisa hilo.

Wadai walifungua kesi ya madai dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa EAGT, mdaiwa wa kwanza na Askofu Brown Mwakipesile, mdaiwa wa pili.

Kesi hiyo ya madai namba 208 ya mwaka 2023 ilifunguliwa na kundi la waumini 72, John Mathias Chambi na Andondile Kaliboti na wenzao wengine 70 wakiwakilishwa na wakili Johanes Kachenje.

Kwa mujibu wa hati ya madai waliomba nafuu mbalimbali ikiwemo Mahakama kutamka kuwa mdaiwa wa pili, Askofu Mwakipesile au ofisa yeyote hakuwa na mamlaka ya kutoa barua ya Julai 13, 2022.

Pia walidai kundi la upande wa wadaiwa linajaribu kujitwalia isivyo halali makanisa yaliyoko chini ya himaya yao.

Wadaiwa kupiti wakili Miraa katika maelezo yao ya utetezi wa maandishi dhidi ya madai hayo, walipinga madai yote ya wadai.

Pia waliibua pingamizi la awali la kisheria wakiiomba Mahakama isiwasikilize, wakidai hawana haki kisheria kufungua kesi hiyo na kudai masilahi katika mali za kanisa hilo.

Mahakama ilipodurusu hati ya madai ilibaini nyaraka hizo zilikuwa zimesainiwa na kuthibitishwa na wadai wawili tu; Chambi, ambaye ni mdai wa kwanza na Kaliboti, mdaiwa wa pili.

Hati ya madai ilionyesha wadai hao wawili waliosaini hati hiyo wamesaini kwa niaba ya wengine jambo linaloonyesha ni kesi ya uwakilishi.

Jaji Phillip kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo aliibua hoja iwapo kesi hiyo imefunguliwa kwa mfumo wa uwakilishi (kwamba mdai wa kwanza Chambi na wa pili, Kaliboti) ni wawakilishi wa wadai wengine 70, kwa kuzingatia taratibu za kufungua shauri la uwakilishi.

Wakili wa wadai, Kachenje alikiri kutokana na sehemu ya uthibitisho wa madai katika hati ya madai kusainiwa na wadaiwa wawili pekee wakati hapakuwa na kibali kilichoombwa na kutolewa na Mahakama kwa wadai kufungua kesi ya uwakilishi.

Hata hivyo, aliiomba Mahakama iamuru wafanye marekebisho katika hati ya madai, kurekebisha kasoro hiyo ili kesi iendelee kusikilizwa.

Wakili Miraa, alipinga maombi ya wadai kuruhusiwa kurekebisha kasoro hiyo akidai sheria inazuia kuchukua hatua kama hiyo wakati tayari pingamizi la awali likiwa limeshaibuliwa na upande kinzani.