Mahakama yatupa maombi kumshitaki DC Makilagi

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi

Muktasari:

  • Mchungaji Kitonka aliyekuwa anadai kuwa mmiliki halali wa jengo la kanisa linalogombaniwa, alikuwa anaiomba Mahakama kutoa amri ya kumruhusu yeye na waumini wake kuendelea kufanya ibada katika jengo hilo hadi shauri la msingi litakaposikilizwa na kuamuliwa.

Mwanza. Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali maombi madogo ya madai namba 68/2023, yaliyowasilishwa na Mchungaji wa Kanisa la Assemblied of God Gospel Church International (AGGCI), Benson Kitonka dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.

Kesi hiyo iliyotolewa hukumu katika shauri la msingi, mleta maombi mchungaji Kitonka alikuwa anaiomba Mahakama kulipa kanisa hilo haki ya kumiliki jengo la Kanisa lililoko eneo Bugando jijini Mwanza, ambalo kwa sasa linamilikiwa na Kanisa la Evangelical Assemblies of God in Tanzania (EAGT).

Kabla ya kujitenga na kuanzisha Kanisa jipya la AGGCI, mchungaji Kitonka na baadhi ya waumini wake walikuwa waumini wa Kanisa la EAGT na walikuwa wakifanya ibada zao katika jengo linalogombaniwa sasa.

Baada ya mgogoro na hatimaye wachungaji na baadhi ya waumini kujitenga kwa kuanzisha kanisa jipya, mali na fedha ziliamuliwa kubaki chini ya mamlaka na umiliki wa EAGT, uamuzi unaoungwa mkono na taasisi na ofisi za Serikali ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, msimamo unaopingwa na upande wa Kanisa la AGGCI kupitia kwa mchungaji Kitonka kwa kufungua shauri mahakamani.

Mchungaji Kitonka aliyekuwa anadai kuwa mmiliki halali wa jengo la kanisa linalogombaniwa alikuwa anaiomba Mahakama kutoa amri ya kumruhusu yeye na waumini wake kuendelea kufanya ibada katika jengo hilo hadi shauri la msingi litakaposikilizwa na kuamuliwa.

Desemba 20, 2023, Mahakama Kuu kupitia kwa Jaji Stanley Kamana ilitoa amri ya kuitaka Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana kutengua uamuzi wa kuwazuia waumini wa Kanisa la AGGCI kutumia jengo hilo.

Kutokana na amri ya awali kutotekelezwa, waleta maombi kupitia kwa Wakili Gibson Ishengoma walirejea mahakamani kuomba Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi atekeleze amri ya kutengua zuio dhidi ya waumini na viongozi wa Kanisa la AGGCI kutumia jengo la eneo la Bugando jijini Mwanza, tofauti na hivyo aitwe mahakamani kueleza kwa nini hajatekeleza amri halali ya mahakama.


Hata hivyo Januari 26, 2024, Wakili Merumbe aliwasilisha mapingamizi likiwemo la kudai mleta maombi anamshtaki mtu asiyetambulika (Amina Makilagi).

Pia amri ya kumuondoa mchungaji Kitonka na waumini wake katika kanisa hilo haukuwa utashi binafsi ya DC Makilagi bali wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.

Akisoma uamuzi huo leo Jumatatu, Februari 5, 2024, Jaji Wilbert Chuma, amesema kwa kuzingatia vigezo vya kisheria na hoja zilizowasilishwa na pande zote mahakamani hapo, mjibu maombi (Makilagi) hakustahili kushtakiwa kwani alikuwa akitekeleza maagizo kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Nyamagana.

Pia amesema mleta maombi kwenye hati ya maombi amemshtaki mtu asiyetambulika badala yake alitakiwa kukishtaki kituo cha Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana na si Amina Makilagi kama ilivyoandikwa katika hati ya maombi na kiapo cha mleta maombi.

“Mahakama hii inaona kwamba hoja ya kwanza; kuhusu kukosewa kwa majina ya anayeshtakiwa ingeweza kutosha kumaliza shauri lililopo mahakamani hapa bila kwenda hata katika pingamizi la pili la mjibu maombi.” 


“Mjibu maombi namba moja (Makilagi) kufanya vile alikuwa akitekeleza mamlaka yake kwa niaba ya Serikali kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama cheo kinachotambulika kwa mujibu wa Kifungu namba 15 cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1997. 

“Mahakama hii haiendelei na kuzungumzia maombi yaliyopo mahakamani kutokana na kukosewa hivyo maombi yamekuwa ‘struck out’. Mleta maombi kama hujaridhika unaweza kukata rufaa katika mahakama ya juu,” amesema jaji huyo.

Baada ya uamuzi huo kutolewa, Mchungaji Kitonga amesema hatokata rufaa badala yake ataandika barua kwa bodi ya wadhamini ya kanisa la EAGT kuomba akabidhiwe vitendea kazi ili aendelee kutoa huduma za kiroho katika eneo tofauti na kanisa hilo.

“Sisi wote (AGGCI na EAGT) ni watoto wa baba mmoja, kazi yetu ni kuhubiri injili, sioni tena haja ya kuendelea kumshitaki DC Makilagi, nimeamua kuachana na kesi zote na kanisa nimewaachia,” amesema Kitonka.