Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yasimamisha kwa muda ujenzi wa MK-ICC Arusha

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imezuia kwa muda shughuli za ujenzi wa mradi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mount Kilimanjaro (MK-ICC) unaotekelezwa katika eneo la Kijenge, Arusha kufuatia sehemu ya eneo hilo lenye ukubwa wa ekari mbili, kuwa na mgogoro kati ya Andrew Mollel na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), hadi kesi ya ardhi kuhusu eneo hilo itakapoamuliwa.

Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha imeamuru kusitishwa kwa muda shughuli zote za ujenzi wa mradi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mount Kilimanjaro (MK-ICC), unaotekelezwa kwa katika eneo la Kijenge, Arusha.

Mahakama imefikia uamuzi huo kutokana na sehemu ya ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) kwa kushirikiana na PSSSF, yenye ukubwa wa ekari mbili, kuwa kwenye mgogoro, hadi kesi ya msingi kuhusu eneo hilo itakapomaliza kusikilizwa na kuamuliwa.

Uamuzi huo ulitolewa Juni 15, 2026 na Jaji Frank Mahimbali katika maombi yaliyowasilishwa na Andrew Titus Mollel dhidi ya AICC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika shauri hilo, Mollel aliomba Mahakama itoe amri ya muda ya kuwazuia wadaiwa kuendelea kuingia, kujenga, kuweka uzio, kugawa au kufanya shughuli zozote katika eneo hilo wakati kesi ya msingi ya ardhi namba 29450/ 2025 ikiendelea mahakamani.

Mahakama ilikubaliana na maombi hayo baada ya kubaini kuwa kuna masuala mazito ya kisheria kuhusu mmiliki wa eneo hilo, yanayohitaji kusikilizwa kikamilifu kabla ya hatua zozote zaidi kuchukuliwa kwenye eneo linalobishaniwa.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Mollel anadai kuwa ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo baada ya kununuliwa na Christine Marealle Juni 28, 1990 kwa Alfred Lotuno, wakati yeye akiwa mdogo.

Ombi hilo liliungwa mkono na hati ya kiapo ya Christine Marealle huku likipingwa na hati ya kiapo ya Mkurugenzi wa AICC, Christine Mwakatobe (kwa niaba ya mjibu maombi wa kwanza).

Pia, alieleza kuwa mwaka 2006 ardhi hiyo ilivamiwa na mtu aliyefahamika kwa jina la Mashaka Sambweti, jambo lililosababisha kufunguliwa kwa shauri katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya.

Mollel alidai kuwa katika shauri hilo yeye alitangazwa kuwa mmiliki halali wa ardhi husika na baadaye ushindi huo ulithibitishwa na Mahakama Kuu kupitia Rufaa ya ardhi namba 35/2018.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, taratibu za utekelezaji wa hukumu zilifanyika na umiliki wa eneo hilo ulirejeshwa kwake rasmi Aprili 2024.

Hata hivyo, alidai kuwa Machi 2025 maofisa na mawakala wa AICC waliingia katika eneo hilo, wakabomoa nyumba ya mlinzi, wakaondoa uzio na kuanza shughuli za ujenzi bila ridhaa yake.

Aidha, aliiambia Mahakama kuwa utafiti wa mipaka uliofanywa na kampuni ya Precise Surveys and Mapping Ltd unaonyesha kuwa eneo lake halimo ndani ya eneo la Kijenge Site "E" ambalo AICC inadai kuwa sehemu ya mali yake.

Kwa upande wake, AICC ilipinga madai hayo na kueleza kuwa ardhi inayogombaniwa ni mali ya umma iliyokabidhiwa kwa taasisi hiyo kwa mujibu wa Notisi ya Serikali namba 115 ya mwaka 1978.

AICC ilieleza kuwa eneo hilo lipo ndani ya Kijenge Site "E" na umiliki wake tayari umeamuliwa na Mahakama Kuu katika kesi za ardhi jumuishi namba 12 na 16 za mwaka 2015 ambapo waliambatanisha nakala ya hukumu iliyotolewa Septemba 29,2017.

Kwa mujibu wa AICC, hatua zilizolalamikiwa na Mollel zilifanyika kwa kufuata amri halali za utekelezaji zilizotolewa na Mahakama Julai 15, 2025 dhidi ya watu waliokuwa wamevamia ardhi hiyo ambapo Mahakama iliidhinisha urejeshaji wa umiliki wa ardhi kutoka kwa wavamizi.


Uamuzi wa Mahakama

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mahimbali amesema Mahakama haiwezi katika hatua ya maombi ya muda kuamua moja kwa moja nani mmiliki wa eneo hilo kwa kuwa kuna maswali mengi yanayohitaji ushahidi wa kina.

Miongoni mwa maswali hayo ni kutambua eneo halisi la ardhi inayobishaniwa, kama ardhi ya Mollel ipo ndani au nje ya Kijenge Site "E", pamoja na kubaini kama hukumu zilizotolewa katika kesi za awali zinaihusu ardhi hiyo hiyo.

Nyingine ni kama hukumu katika kesi za ardhi jumuishi namba 12 na 16 za 2015 inaathiri haki zinazodaiwa na mwombaji na kama amri ya utekelezaji ya Julai 15 mwaka jana ilitekelezwa dhidi ya ardhi ya mwombaji au lah.

Mahakama ilieleza kuwa masuala hayo hayawezi kuamuliwa kwa kutumia hati za kiapo pekee bali yanahitaji ushahidi wa wataalamu wa ardhi, nyaraka za umiliki, ramani na ushahidi wa mashahidi wakati wa usikilizwaji wa kesi kuu.

Katika uamuzi wake, Mahakama ilitumia kanuni zilizowekwa katika mashauri mbalimbali ambayo yanaweka masharti matatu ya kutoa amri za muda.

Masharti hayo ni kuwepo kwa suala zito la kusikilizwa, uwezekano wa kutokea kwa madhara yasiyoweza kurekebishwa kwa urahisi na uwiano wa masilahi kuwa upande wa mwombaji.

Jaji Mahimbali amesema sharti la kwanza limetimia kwa kuwa pande zote zimewasilisha nyaraka na hoja zinazozua mgogoro mkubwa wa umiliki unaohitaji kuamuliwa na Mahakama.

Kuhusu madhara yanayoweza kutokea, Mahakama ilibaini kuwa ujenzi unaoendelea katika eneo hilo unaweza kubadilisha kabisa hali ya ardhi kabla ya kesi kuamuliwa.

Jaji amesema ikiwa Mollel atashinda kesi baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maendeleo katika eneo hilo, utekelezaji wa hukumu unaweza kuwa mgumu au hata kutowezekana kwa vitendo.

Kwa mujibu wa Mahakama, uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya kudumu kama hoteli, majengo ya mikutano, barabara na huduma nyingine unaweza kufanya urejeshwaji wa ardhi katika hali yake ya awali kuwa mgumu sana.

Jaji Mahimbali amesema ingawa AICC imeeleza kuwa mradi huo una masilahi ya umma, Mahakama ina wajibu wa kuhakikisha haki za wadai wote zinalindwa hadi mgogoro wa msingi utakapopatiwa uamuzi wa mwisho.

"Masilahi ya umma yanapaswa kwenda sambamba na kulinda haki za watu wanaodai umiliki wa mali inayobishaniwa.

"Ushahidi uliopo mbele ya Mahakama unaonyesha kwamba sehemu inayobishaniswa ni sehemu ya mradi mkubwa wa maendeleo unaohusisha ujenzi wa MK-ICC ambapo wakandarasi tayari wamekabidhiwa eneo la Mraei Desemba 22, 2025," amesema Jaji Mahimbali katika sehemu ya uamuzi wake.

Jaji amesema jambo lingine mahakama imelizingatia ni kwamba ujenzi unaendelea na fedha za umma zimewekezwa katika mradi huo hata hivyo ni muhimu kutambua umiliki wa sehemu halisi inayodaiwa na mwombaji unabaki kuwa suala linalosubiri uamuzi katika kesi ya msingi.

"Ikiwa ujenzi hautasitishwa na mwombaji akafanikiwa, Mahakama inaweza kukabiliwa na jambo lililobadilishwa na hukumu ambayo itakuwa ngumu kutekeleza, madhumuni ya usitishaji wa muda kusubiri uamuzi ni muhimu," amesema.

Kutokana na sababu hizo, Mahakama ilikubali maombi ya Mollel na kuamuru pande zote kudumisha hali ilivyo katika eneo lenye mgogoro.

Mahakama pia imezuia AICC, watumishi wake, mawakala, wakandarasi na mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba yake kuendelea na ujenzi, maendeleo, ugawaji, uhamisho au shughuli yoyote itakayobadilisha hali ya eneo hilo.

Aidha, pande zote zimeagizwa kutoharibu au kuingilia ushahidi wowote unaohusiana na mipaka, utambulisho na umiliki wa ardhi inayobishaniwa.

Mahakama imeagiza pia kesi kuu ya Ardhi namba 29450/ 2025 kupewa kipaumbele na kusikilizwa kwa haraka ili mgogoro huo upate ufumbuzi mapema.

Kuhusu gharama za maombi hayo zitaamuliwa kulingana na matokeo ya kesi kuu.