Mahakama yataifisha gari iliyokutwa na dawa za kulevya

Muktasari:
- Llicha ya Mahakama kuwaachia huru washtakiwa watano walioshtakiwa kwa usafirishaji wa dawa za kulevya, imetaifisha gari iliyokutwa na dawa hizo.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewaachia huru wafanyabiashara watano wakiwemo raia wa Nigeria waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka manne ya kusafirisha dawa za kulevya aina heroine, cocaine na bangi huku ikilitaifisha gari iliyotumika kusafirisha dawa hizo.
Washtakiwa hao wameachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.
Walioachiwa ni raia wa Tanzania, Ruth Kabezi na wanaume wanne raia wa Nigeria ambao ni Kayode Alonge, Aron Ejeh, Nwauba Obinna na Darlington Nwauba.
Licha ya Mahakama kuwaachia huru washtakiwa hao, imeamuru gari aina ya Toyota Mark X iliyokutwa na dawa hizo itaifishwe na kuwa mali ya Serikali.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Desemba 28, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.
Amesema washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 197/2019 walipofikishwa mahakamani walikuwa sita, lakini baadaye mshtakiwa mmoja, Bisola Adeyemi alifariki dunia wakati kesi ikiwa hatua ya usikilizwaji.
Amesema washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka manne ya kusafirisha dawa za kulevya, tukio wanalodaiwa kulitenda Februari 17, 2018 eneo la Masaki, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Wanadaiwa siku hiyo walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya cocaine zenye uzito wa gramu 13.53, heroin zenye uzito wa gramu 10 na bangi gramu 247.24.
Akipitia ushahidi wa upande wa mashtaka, Kabate amesema Serikali iliwasilisha mashahidi tisa kuthibitisha mashtaka yao, huku upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi watano ambao ni washtakiwa wenyewe.
Hakimu Kabate amesema amejielekeza katika hoja mbili ambazo kama washtakiwa walisafirisha dawa hizo na iwapo walikutwa nazo.
Amesema ushahidi wa upande wa mashitaka ulidai walikutwa na dawa hizo ndani ya nyumba namba 706, iliyopo Masaki, eneo la Slip Way, aliyokuwa amepanga mshtakiwa Ruth na ndiye aliyewafungulia mlango polisi walipokwenda kufanya upekuzi.
"Hati ya upekuzi ambayo ni kielelezo cha nne cha upande wa mashtaka, kinaonyesha ilijazwa kwa jina la Ruth K. ambalo ni jina tofauti na lililo katika hati ya mashtaka, kwani hati ya mashtaka linasomeka kama Ruth Kabezi( mshtakiwa wa kwanza) na si Ruth K" amesema Hakimu Kabate.
Pia ameeleza hakuna uthibitisho kwamba Ruth K ndiye huyo huyo, Ruth Kabezi, hivyo upande wa mashtaka wameshindwa kuithibitishia Mahakama ni yupi hasa mmiliki wa nyumba hiyo (Apartment).
Pia imeelezwa Adeyemi ambaye ameshafariki ndiye alikuwa akilipia kodi nyumba hiyo waliokuwa pia wakiishi washtakiwa wenzake.
"Upande wa mashtaka umeshindwa kuleta mkataba wa nyumba kuthibitisha hilo au hati ya kusafiria ya Ruth kuthibitisha majina yake, ukiondoka ushahidi huo hakuna ushahidi mwingine unaothibitisha kuwa nyumba hiyo ilikuwa ikimilikiwa na mshtakiwa huyo," imeelezwa.
Akiendea kupitia ushahidi huo, Kabate amesema dawa nyingine zilipatikana katika gari aina ya Toyota Mark X inaodaiwa kumilikiwa na mshtakiwa Nwauba.
"Naamuru gari hili litaifishwe kuwa mali ya Serikali kwa kuwa lilikutwa na dawa za kulevya ndani yake, lakini mshtakiwa huyu (Nwauba) Mahakama hii inakuachia huru kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kama gari hilo lilikuwa lako au la kwa sababu shahidi kutoka TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) alivyokuja kutoa ushahidi alitueleza jina lililosajiliwa katika mfumo wa magari ni tofauti na jina aliloshtakiwa nalo mshtakiwa," amesema na kuongeza:
"Kwa kuwa hakuna ushahidi wa kuwaunganisha na mashtaka yaliyokuwa yanawakabili washtakiwa hawa, Mahakama hii inawachia huru washtakiwa wote" amesema Hakimu Kabate.
Baada ya maelezo hayo, ameamuru dawa hizo ziteketezwe chini ya usimamizi wa Kamisha wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA).
Pia ameelekeza washtakiwa warudishiwe hati zao za kusafiria, simu pamoja na kompyuta.