Mahakama yataka upelelezi kesi ya Loliondo uharakishwe

Watu saba wafikishwa kortini wakidaiwa kujipatia Sh 428milioni mali ya Tanesco

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imetaka Jamhuri kuharakisha upelelezi kesi ya mauaji askari Loliondo.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, imeutaka upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya askari polisi inayowakabili watuhumiwa 27, kutoka eneo la Loliondo, wilayani Ngorongoro, kuharakisha upelelezi.

Agizo hilo limetolewa leo Julai 14, 2022 na Hakimu Mkazi Herieth Mhenga, wakati shauri hilo la mauaji namba 11/2022 lilipotajwa mahakamani hapo.

Miongoni mwa wanaokabiliwa na shauri hilo, ni madiwani 10, Mwenyekiti wa CCM wilayani Ngorongoro, Ndirango Laizer pamoja na wanafunzi wawili.

Hakimu Mhenga ameutaka upande huo wa Jamhuri kukamilisha upelelezi huo ili wanaofunzi waliomo warudi shule na washitakiwa wengine wawili wanaoumwa wakatibiwe.

Awali Wakili wa utetezi Jeremiah Mtobesya aliomba kuharakishwa kwa upelelezi kutokana na watuhumiwa hao wanne kutakiwa kwenda masomoni na wengine kupata matibabu.

Wakili Mtobesya amedai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa wa tatu, Simeli Parmwati ni mwanafunzi anayepaswa kujiunga na masomo ya kidato cha tano huku mshitakiwa wa 23, Fred Victor alipaswa kuwasilisha maandiko yake ya kitaaluma kwa ajili ya kuendelea na masomo nchini Marekani ambapo anachukua shahada ya uzamivu (PhD).

Amedai mahakamani hapo kuwa Parmwati anapaswa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu ambapo wanafunzi wengine wameshaanza masomo huku Victor, akidaiwa kuwa akichelewesha mawasilisho hayo atafutiwa usajili hivyo atakuwa amepoteza haki yake ya kupata elimu na atapata hasara.

Kuhusu wagonjwa, alidai kuwa mshitakiwa wa 19 anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari huku mshitakiwa wa 22, Lukerenga Koyee akiwa na tatizo la figo.

Washitakiwa wengine ni Molongo Paschal, Albert Selembo, Lekayoko Parmwati,Sapati Parmwati, Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti, Morijoi Parmati, Morongeti Meeki, Kambatai Lulu Moloimet Yohana na Joel Clemes Lessonu.

Wengine ni Simon Orosikiria,Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu,Luka Kursas,  Taleng'o Leshoko, Kijoolu Kakeya, Shengena Killel,Kelvin Shaso Nairoti, Lekerenga Koyee, Wilsom  Kiling, James Taki, Simon Saitoti na Joseph Lukumay.

Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 28, 2022 ambapo atatolea uamuzi mdogo hoja nyingine zilizowasilishwa na mawakili wa panze zote.