Mahakama yatupilia mbali pingamizi la Mbowe, Kibatala awasilisha pingamizi lingine

Mahakama yatupilia mbali pingamizi la Mbowe, Kibatala awasilisha pingamizi lingine

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, imetupilia mbali pingamizi ililowasilisha na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu la kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi zenye mashtaka ya Ugaidi.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, imetupilia mbali pingamizi ililowasilisha na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu la kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi zenye mashtaka ya Ugaidi.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Septemba Mosi, 2021 na Jaji Elinazer Luvanda, baada ya kupitia hoja za pande mbili.

Jaji Luvanda amesema mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ugaidi na kwamba pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi halina mashiko na hakubaliani nalo.

"Kwa maoni yangu, sitaweza kukubaliana na hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi," amesema Jaji Luvanda na kuongeza

"Baada ya kupitia hoja za pande zote, mahakama hii inayo mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ugaidi na hoja zilizowasilishwa na upande wa utetezi hazina mashiko," amesema Jaji Luvanda.

Jana Agosti 31, 2021 Mbowe na wenzake waliwasilisha pingamizi mahakamani hapo wakipinga mahakama hiyo kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao kwa mashtaka ya ugaidi na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Ugaidi kesi yao inapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu ya kawaida na si hiyo ambayo ni Divisheni Maalum.

Baada ya washtakiwa hao kuwasilisha pingamizi hilo, Serikali imepinga hoja hizo ikidai kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba 3 ya mwaka 2016 makosa yaliyoko   kwenye Sheria ya Ugaidi yaliwekwa kwenye Sheria ya Uhujumu Uchumi na kwamba kwa hali hiyo mahakama hiyo ya ufisadi ina mamlaka ya kusikiliza mashtaka yao.

Baada ya Jaji Luvanda kutoa uamuzi huo, upande wa mashtaka waliomba kuwasomea maelezo ya awali (PH) washtakiwa hao.

Hata hivyo kabla ya kuwasomea maelezo kufanya, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando anayewasilisha jopo la mawakili watano wa upande wa mashtaka, ameniomba mahakama hiyo, kufanya marekebisho katika hati ya mashtaka kwa kuieleza mahakama hiyo kuwa Hoteli  ya Aishi ipo wilayani Hai na sio wilayani Moshi kama ilivyoandika katika hati ya mahstaka.

Wakili Kadando baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Peter Kibatala amewasilisha pingamizi mahakamani hapo akipinga hati ya mashtaka ina makosa.

Kutokana na hali hiyo, Jaji Luvanda aliahirisha kesi hiyo kwa dakika 15 ili upande wa utetezi uweze kuja kuwasilisha hoja kuhusu pingamizi hilo huku upande wa mashtaka nao watatakiwa kujibu hoja hizo.