Mbowe asubiri hatima ya kesi yake

Mbowe asubiri hatima ya kesi yake

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kwa ajili ya kusikiliza uamuzi dhidi ya pingamizi waliwasilisha mahakamani hapo la kupinga kesi yao kusikilizwa na mahakama hiyo .

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kwa ajili ya kusikiliza uamuzi dhidi ya pingamizi walilowasilisha mahakamani hapo la kupinga kesi yao kusikilizwa na mahakama hiyo .

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo, leo Septemba Mosi, 2021 majira ya saa mbili asubuhi na kupelekwa mahabusu iliyopo mahakamani hapo.

Hata hivyo ilipofika  saa 2:45 asubuhi, walitolewa mahabusu na kupelekwa ndani ya ukumbi wa mahakama, kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa Jaji  Luvanda.

Jana Agosti 31, 2021 Mbowe na wenzake waliwasilisha pingamizi mahakamani hapo wakipinga mahakama hiyo kusikiliza kesi yao kwa mashtaka ya ugaidi na kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia Ugaidi kesi yao inapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu ya kawaida na si hiyo ambayo ni divisheni maalumu.

Baada ya washtakiwa hao kuwasilisha pingamizi hilo, Serikali imepinga hoja hizo ikidai kuwa kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 3 ya Mwaka 2016 Makosa yaliyoko   kwenye Sheria ya Ugaidi yaliwekwa kwenye Sheria ya Uhujumu Uchumi na kwamba kwa hali hiyo Mahakama ya Ufisadi ina mamlaka ya kusikiliza mashtaka yao.

Kutokana na hoja hizo,  Luvanda anayesikiliza shauri hilo, alipanga kutoa uamuzi leo.

Hata hivyo, ulinzi umeimarishwa katika mahakama hiyo kuanzia getini hadi ndani ya viunga vya mahakama na utaratibu wa kuingia katika mahakama hiyo kwa leo umekuwa tofauti ambapo kila anayeingia lango kuu la Mahakama hiyo, lazima aonyeshe kitambulisho na awe amevaa barakoa.

Hata hivyo ni watu wachache tu ndiyo wameruhusiwa kuingia katika ukumbi wa mahakama kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo, huku wengi wao wakisalia katika viwanja vya mahakama hiyo kutokana na tahadhari ya ugonjwa wa Uviko -19.

Katika kesi hiyo ya msingi namba 16/2021, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili pesa kwa ajili vitendo vya kigaidi.