Mahari ya kuoa mwanamke wa Kiafrika yatajwa chanzo cha ukatili kwenye ndoa, familia

Muktasari:

  • Diwani wa Matumbulu, Emmanuel Chibago amesema mipango na mikakati inapaswa kuelekezwa kwenye kutoifanya mahari kuwa ya lazima, badala yake iwe sehemu ya zawadi.

Dodoma. Mahari inayotolewa kwa wazazi wa mwanamke kabla ya kuolewa imetajwa ndiyo chanzo cha manyanyaso na mateso katika familia nyingi.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili, Desemba 10, 2023 na Diwani wa Matumbulu, Emmanuel Chibago wakati akizungumza na wananchi wa Kata za Matumbulu na Mpunguzi kwenye kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Wananchi wa kata hizo walikutanishwa pamoja kwa uratibu wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) na Ushirika wa Wakulima wa Zabibu na Masoko (Uwazamam) chini ya ufadhili wa Shirika la We Effect.

Chibago amesema mila za utoaji wa mahari kwa wanandoa zimeacha ombwe na maumivu kwa wanawake hata maisha yao kwenye nyumba wanazoishi baadhi yao yamekuwa kama Jehanamu.

Diwani huyo aliyewahi kuwa naibu meya amesema wanaume wamebebeshwa ufalme mkubwa lakini ndani ya familia ukweli unabaki kuwa mwanamke ndiye kila kitu.

"Haya mambo ya mahari ni tatizo, ndiyo chanzo kikuu cha magomvi na migogoro inayowaumiza zaidi wanawake na mama zetu, tunafanya ukatili usiokuwa na aibu hadi kwenye daladala," amesema Chibago.

Hata hivyo, amesema ukatili kwa wakati huu upo hata dhidi ya wanaume, japo ni sehemu ndogo, lakini hawajitokezi hadharani na mara nyingi huenda kufanya udikteta kwa kulipa kisasi.

Mkazi wa Mpunguzi, Victoria Mushi amesema matukio mengi yapo maeneo ya vijijini ambako sehemu kubwa hawajapata elimu ya ukatili na hawajui mahari pa kukimbilia au kupeleka matatizo yao.

Victoria amesema kwa siku za hivi karibuni vijana wanapooa huwalazimisha wenza wao kufanya nao mapenzi kinyume na maumbile na mabinti wakigoma basi hutafutiwa sababu.

Hata hivyo, amesema mambo mengi yanaishia ngazi ya chini kwa maana ya kumalizana bila kufika kwenye vyombo vya maamuzi.

Amesema suala la vipigo ni kawaida kusikia kila uchao na wengi hupata ulemavu na hata vifo kwa mambo ambayo kama yangefikishwa kwa wahusika, huenda yangepatiwa ufumbuzi na suluhu ya kudumu.

Mjumbe wa Bodi ya Tawla, Fortunata Matinde amesema wamepeleka ujumbe huo kijijini kwa lengo la kuwakumbusha na kuwataka wawe mashujaa wa kuripoti matukio bila kuchukua sheria mkononi.

Matinde amesema kwenye kusanyiko hilo, pamoja na kuwapa elimu ya kutambua ukatili, wameshirikiana na taasisi inayojihusisha na masuala ya ardhi ili kutoa elimu kwenye masuala ya migogoro ya ardhi na haki za umiliki.