Mahindi yaliyozuiwa Zambia ruksa kuingia nchini

Muktasari:

  • Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dk Francis Michael Mei 31 mwaka huu ametembelea mpaka wa Tunduma na kuzungumza na wafanyabiashara wa kitanzania ambao walipiga kambi mpakani hapo wakiendelea na jitihada mbalimbali za kukomboa shehena hiyo.

Songwe. Hatimaye shehena ya mahindi iliyokuwa imekwama nchini Zambia, yaruhusiwa kuingizwa nchini baada ya Serikali ya Tanzania na Zambia kutatua changamoto hiyo kidipromasia ili kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael Mei 31 mwaka huu ametembelea mpaka wa Tunduma na kuzungumza na wafanyabiashara wa Kitanzania ambao waliweka kambi mpakani hapo wakiendelea na jitihada mbalimbali za kukomboa shehena hiyo.

Dk Michael amesema kuwa zaidi ya malori 30 ambayo ni sawa na Tani 1000 za mahindi yalikwama katika mji wa Nakonde Zambia, lakini sasa yameruhusiwa kuvuka ikiwa ni hatua za awali za kuruhusu mahindi yote yaliyokwama nchini humo kuruhusiwa.

Inadaiwa kuwa mahindi hayo yalinunuliwa na wafanyabiashara hao kwa kusudi la kuyaingiza nchini miezi sita iliyopita, kwa kuzingatia taratibu zote za nchi hiyo, lakini baadaye kutokana na nchi hiyo kuona inakabiliwa na upungufu wa chakula mwaka huu, ilifunga mpaka na hivyo kuzuia mazao ya nafaka kutoka nje.

"Tuliiomba Serikali ya Tanzania  kupitia Mkuu wa Mkoa kuzungumza na Serikali ya Zambia ili tuweze kuruhusiwa kuvuka mpaka baada ya kuzuiwa kwa takribani miezi 6 bila sababu za msingi huku tukiwa na nyaraka zote za ununuzi na usafirishaji," amesema Salome Mwampeta mmoja wa wafanyabiashara ambao shehena yao ilikuwa imezuiliwa.

Mwampeta amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kufanikisha mzigo wao kuvuka na kuwa kitendo hicho ni cha ukombozi kwao kwani walishaanza kukata tamaa wakidhani wamepoteza na hawakujua watapata wapi fedha zingine Ili walipe mikopo waliyokopa.