MAHUBIRI: Kukabiliana na nguvu kinzani kwa njia za maombi
Bwana Yesu asifiwe! Ninakukaribisha katika mahubiri ya leo, Jumapili, tukiwa tumepewa somo; “Kukabiliana na nguvu za upinzani kwa njia ya maombi.” Sote tunatambua kuwa maisha ya mwanadamu mara nyingi hukutana na nguvu za upinzani zinazolenga kuzuia maendeleo, mafanikio na utimilifu wa kusudi la Mungu.
Hata hivyo, kupitia neno la Mungu tunapata uhakika kwamba hakuna silaha itakayofanyika juu yetu itakayofanikiwa, kwa sababu Mungu ameahidi kuwa pamoja nasi katika kila vita tunavyopitia.
Biblia Takatifu inatufundisha kwamba zipo nguvu za upinzani zinazoonekana na zisizoonekana, lakini njia kuu ya kushinda ni kwa njia ya maombi. Tunapomuita Mungu kwa imani, yeye hufunua yaliyojificha, huondoa vikwazo na kutufungulia njia ya ushindi katika kila eneo la maisha yetu.
Isaya 54:17 anasema: “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa.”
Upinzani maana yake nini?
Ni ile hali ya kuzuiwa usitembee kwenye viwango vya aina fulani.
Kupingwa usifanye jambo kwa mafanikio ya aina fulani.
Kuzuiwa usiwe na matokeo kwenye mipango uliyo nayo. Kupingwa usitimize malengo fulani. Kuwekewa vikwazo vitakavyosababisha usiwe na ufanisi. Kuwekewa zuio juu ya maono na malengo uliyojiwekea.
Aina mbili kuu za upinzani
Upinzani dhahiri uliofunuliwa
Huu huwa ni upinzani unaoonekana. Aina hii ya upinzani unakuwa unaweza kumuona anayekupinga, au waliokuwa wanakupinga kwa siri Mungu anawaweka wazi, na vitu vya sirini kuonekana katika uhalisia wake.
Ayubu 12:22 anasema: “Huvumbua mambo ya siri tokea gizani, na hicho kilicho giza tupu huleta mwangani.”
Upinzani wa rohoni, ule usioonekana
Huu huwa ni upinzani uliofichwa katika namna ya rohoni. Aina hii ya upinzani unakuwa hauelewi kinachoendelea, lakini mambo hayako sawa, mambo hayaendi unavyopanga, hayaendi unavyotaka. Ni mpaka utakapopata ufunuo wa kujua cha kufanya au vitu kuwekwa wazi mbele yako. Sasa njia pekee ya kuyafunua yaliyofichwa huwa ni njia ya maombi.
Yeremia 33:3 anasema: “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.”
Kukabiliana na upinzani (vikwazo)
Isaya 57:14 anasema: “Naye atasema, Tutieni, tutieni, (jengeni, jengeni), itengenezeni njia, kiondoeni kila kikwazacho katika njia ya watu wangu.” Ukisoma kwenye tafsiri ya Kiingereza utaona lile neno “kiondoeni kila kikwazacho” ametumia neno “Remove the obstacles,” akiwa na maana ya kuondoa vikwazo katika njia ya watu wangu.
Unapoanza kuomba juu ya jambo ambalo halisogei, haliendi au halipo unavyotaka, maombi huwa na nguvu ya kwenda katika ulimwengu wa roho na kuondoa kila kinachozuia (obstacles). Lakini pia, maombi huwa na nguvu ya kulifunua jambo lililositilika na kuliweka wazi ili liweze kushughulikiwa.
Luka 8:17 anasema: “Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi.”
Maeneo mengi tulipoanza kuomba juu ya upinzani uliokuwepo, Mungu aliondoa vikwazo, na maeneo mengine Mungu alilifunua tatizo na ikawa rahisi kushughulika nalo.
Maeneo ambayo watu hukabiliwa na upinzani
Upinzani unaolenga mtu asifanikiwe kiuchumi, asiwe na kibali ofisini, asifanikiwe kiutawala.
Pia, upinzani wa mtu asifanikiwe kimaisha, kielimu, kisiasa, asiwe na mahusiano yenye tija, asiolewe, asioe, asifikie malengo, asiwe na amani kwenye ndoa, asiwe na afya njema, awe mtu wa kuhangaika hospitalini, kukosa furaha, na siku zote awe mtu wa huzuni.
Eneo jingine ni upinzani unaolenga mtu asione faida kwenye biashara, siku zote awe mtu wa hasara, asizae watoto, tumbo la uzazi lifungwe, asiwe na uhuru wa kifedha, siku zote awe mtu wa madeni yasiyoisha, na asikubalike, awe mtu wa kuchukiwa na watu.
Ahadi ya Mungu juu ya maisha yako
Yeremia 1:19 anasema: “Nao watapigana nawe, lakini hawatakushinda.” Pata nafasi ya kuomba ukimuamini Mungu juu ya ahadi hii, kuwa upinzani unaweza ukaja, lakini Bwana amekusudia kukushindia kwa kuwa unamwamini na kumtegemea.
Yoshua 1:5 anasema: “Hapatakuwa na mtu yeyote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako, kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe. Sitakupungukia wala sitakuacha.” Maana yake ni kuwa hapatakuwa na upinzani utakaokuweza, japokuwa ni pale utakapokuwa na muda wa kutafuta madhabahu ya Mungu kwa maombi.
Ufunuo 12:11 anasema: “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wao.” Jitamkie ushindi katika jina la Yesu. Achilia damu ya Yesu kwa maombi.
Ninakutakia neema ya ushindi katika kila eneo lenye upinzani katika jina la Yesu.
Mungu hajakusudia uishi chini ya vifungo, huzuni na kushindwa, bali amekusudia ushinde na kutembea katika neema yake. Hivyo basi, usikate tamaa unapokutana na upinzani, bali simama katika maombi ukiamini kuwa Bwana atakupigania na hakuna adui atakayekushinda.
Tunaposhikilia ahadi za Mungu na kutumia silaha ya maombi, kila kikwazo kitaondolewa na ushindi utakuwa sehemu ya maisha yetu. Bwana akupe neema ya kushinda kila nguvu ya upinzani inayoonekana na isiyoonekana katika jina la Yesu Kristo. Amina.
Kwa maombi na ushauri, Mwalimu Tuntufye Mwakyembe anapatikana jijini Arusha kwa simu 0767629562.