Mahudhurio hafifu kidato cha kwanza yawaingiza viongozi mtaani

Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wakiwa darasani katika shule mpya ya  sekondari ya Makondeni iliyopo Wilaya ya Tandahimba Mkoani Mtwara . Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Tangu kuanza kwa muhula mpya wa masomo Januari 8, 2024 baadhi ya wanafunzi wanaopaswa kuanza kidato cha kwanza wamekuwa na mahudhurio hafifu katika baadhi ya mikoa nchini Tanzania, hivyo kuwalazimiu viongozi kuja na mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo

Dar/mikoani. Wiki ya kwanza tangu kufunguliwa shule za msingi na sekondari za umma kumeonekana kuwapo na mahudhurio hafifu ya wanafunzi wa kidato cha kwanza, hali iliyowafanya baadhi ya viongozi wa mikoa kuanza kuwasaka mitaani.

Hali hiyo inakuja wakati Serikali ikiendelea kutekeleza sera ya elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari.

Mwananchi imekusanya taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini zinazoonyesha juhudi za viongozi kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti shuleni.


Hali ilivyo Mtwara

Miongoni mwa maeneo yaliyotajwa kuwa na mahudhuri hafifu  ni mkoani Mtwara na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Lauteri Kanoni ametangaza kuendesha msako nyumba kwa nyumba kuwasaka wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni kuanzia Januari 15, 2024.

Tangazo hilo linakuja kufuatia Shule ya Sekondari Mpeta kuripoti wanafunzi saba pekee kati ya 89 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza shuleni hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Kanoni alisema  msako huo utawahusisha wazazi na walezi wa wanafunzi waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza katika shule mbalimbali za sekondari wilayani humo na hawajaripoti.

Amesema Serikali imekamilisha maandalizi yote muhimu kwa ajili ya wanafunzi wapya ikiwamo  kuongeza shule mpya katika maeneo ambayo watoto walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta elimu.

“Ikifika Januari 15, 2024 mtoto aliyepangiwa shule hajaenda kuanza masomo, tutafanya msako na kuwakamata, kuwafikisha mahali panapohusika,” amesisitiza Kanoni.

Kwa upande wake, ofisa elimu sekondari wa wilaya hiyo, Lusekelo Mkumbwa amesema katika shule nyingi mahudhurio ni hafifu.

“Shule ya Sekondari Metesa ambayo wameripoti wanafunzi 19 kati ya 64, Chikolopola waliopangiwa 163 wameripoti ni 20, Chikunja walipangiwa  100 wameripoti 25 pekee,” amesema Lusekolo.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, hali ni tofauti ambapo mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza ni ya kuridhisha.

Ofisa elimu sekondari wa halmashauri hiyo, Sostenes Luhende amesema, “Hii ni wiki ya kwanza na mwitikio ni mkubwa tunatarajia kupokea wanafunzi 5,500 katika shule zetu za sekondari, wanafunzi wengi wamesharipoti na tumepata shule mpya na zimepata usajili na wanafunzi wameanza kusoma.”

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude akiwahoji wanafunzi waliokamatwa mnadani katika msako wa kutafuta wanafunzi ambao hawajaripoti shule tangu zilipofunguliwa .Picha na Stella Ibengwe

Hali mbaya Bunda, Geita

Wanafunzi 4,601 waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari mwaka huu katika halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoani Mara hawajaripoti shuleni.

Wanafunzi 1,364 pekee  ndio wameripoti kuanza masomo ya sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kati ya wanafunzi 5,965 waliochaguliwa kujiunga na shule mbalimbali katika halmashauri hiyo mwaka huu.

Ofisa elimu sekondari wa halmashauri hiyo, Wandere Lwakatare ameiambia Mwananchi kuwa kati  ya hao wanafunzi walioripoti, 697 ni wasichana.

"Wavulana walioripoti hadi sasa ni 667 kati ya 2,999 waliopangiwa  shule za halmashauri ya wilaya ya Bunda wakati wasichana waliopangiwa ni 2,966 na wameripoti hadi sasa ni hao 697", amesema Lwakatare.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Salum Telela amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua wazazi watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shule.

Katika Shule ya Sekondari Mariwanda, wanafunzi 55 pekee ndio wameripoti shuleni hapo kati ya wanafunzi 196 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza.

"Hadi sasa wasichana ni 31 kati ya 100 wanaotakiwa kujiunga hapa na wavulana ni 24 kati ya 96 waliochaguliwa", amesema Mkuu wa shule hiyo, Kirika Mwambala.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mariwanda wamesema mazingira yasiyokuwa rafiki ni moja ya sababu inayofanya wanafunzi hao kuripoti kwa kusuasua.

"Mazingira ya kwenda shuleni si rafiki, hakuna walimu wala madawati ", amesema Suleiman Ndege.

Mzazi akiwa na mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika sekondari ya Kilelen akimsindikiza  shuleni kuanza masomo katika muhula mpya wa 2024 baada ya shule kufunguliwa. Picha na Rajabu Athumani.

Naye Pendo Joseph, amesema ubovu wa daraja na  barabara iendayo shuleni hapo ni sababu nyingine inayofanya mahudhurio ya wanafunzi kusuasua.

"Wewe mwenyewe umepita kwenye daraja na barabara ukajionea hali halisi, mbali na ubovu wa daraja lakini pia barabara ina tope jingi sana," amesema Pendo.

Iddi Warioba, amesema mvua zinazoendelea kunyesha ni kikwazo kwa wanafunzi hao kwenda shule, ingawa ana uhakika idadi hiyo itaongezeka hadi kufikia Jumatatu ijayo.

Hata hivyo, Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Wandere Lwakatare amewataka wazazi kuwapeleka watoto shule na kuacha visingizio.

"Wanadai madawati hayatoshi, lakini hadi sasa kuna madawati 50 na wanafunzi wapo 31, pia matengenezo yanaendelea kwenye karakana yetu hapo Hunyari na muda si mrefu madawati 80 yatakuwa tayari," amesema Lwakatare.

 Akizungumzia ubovu wa barabara iendayo shuleni hapo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), Michael Naingo amesema matengenzo ya dharura ya miundombinu iendayo shuleni hapo yataanza ndani ya wiki hii, huku ujenzi wa kudumu wa miundombinu hiyo ukitarajiwa kufanyika kwenye bajeti ijayo.

Mkoani Geita nako mahudhurio hafifu yameonekana, ambapo wanafunzi 995 sawa na asilimia 12 kati ya 8,292 waliopangwa kujiunga na kidato cha kwanza kwenye shule za sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Geita ndio wameripoti shule ndani ya wiki ya kwanza ya masomo.

Kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita wanafunzi 5,217  waliopaswa kuripoti kidato cha kwanza ni wanafunzi 1,200 pekee sawa na asilimia 23 ndio wameripoti.

Mkoani Shinyanga wanafunzi sita wa kidato cha kwanza kwenye Shule ya Sekondari Isoso wilayani Kishapu ndiyo wameripoti shule kati ya wanafunzi 138 waliopangiwa shule hiyo.

Mkuu wa shule hiyo, Anusiata Audax amesema mwitikio wa wazazi kupeleka watoto shule ni mdogo na kati ya sita walioripoti, idadi imeshuka na kubakia watatu.

Kufuatia changamoto ya wazazi kusuasua kupeleka watoto shule, juzi Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude juzi  amelazimika kufanya msako katika mnada wa Mhunze na kuwakamata wanafunzi 45 waliopaswa kuripoti shuleni, lakini wanazurura.

Akikagua  mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Isoso na kukuta wanafunzi watatu na Shule ya Sekondari Kishapu wameripoti 56 kati ya 256 waliochaguliwa kujiunga na shule hiyo.

Naye Ofisa elimu Mkoa wa Shinyanga, Dafroza Ndalichako amesema wanafunzi waliopangiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu ni 38, 963 na wanaendelea kufuatilia, ili kuhakikisha wote wanaripoti shuleni.

Kwa upande wa viongozi mkoani Arusha, akiwamo Mkuu wa mkoa huo  John Mongela na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera wamewahimiza wazazi kuwapeleka watoto shuleni.

Akizungumzia changamoto hiyo, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Ochola Wayoga amesema viongozi wa serikali za mitaa na vijiji wahusike katika kuwafuatilia wanafunzi hao, kubaini kama wamekwenda kwenye shule za binafsi au la.

“Serikali kupitia Tamisemi imekuwa ikituma ujumbe wa simu kukumbusha wazazi kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule, nguvu hii isiishie ngazi ya kitaifa ishuke huku chini kwa kuwa hao watoto wanafahamika,” amesema Wayoga.

Hata hivyo, juhudi za kuwatafuta Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Profesa Carolyne Nombo Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa na Naibu wake, Deo Ndejembi hazikuzaa matunda.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Adolfu Nduguru alipoulizwa kwa simu kuhusu hali hiyo, amejibu kuwa hawezi kuzungumzia hilo, kwani yupo  kwenye sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar.

Imeandikwa na Beldina Nyakeke (Mara), Elizabeth Edward (Dar), Rehema Matowo (Geita), Stella Ibengwe (Shinyanga), Florence Sanawa (Mtwara), Mussa Juma (Arusha) na Joseph Lyimo (Manyara)