Arusha na Manyara waanza kufuatilia watoto watoro shuleni

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera (kulia) akizungumza baada ya kufanya ziara ya kukagua shule za msingi na sekondarI. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Mikoa Arusha na Manyara ina  ya wafugaji ambao wamekuwa hawapendi watoto wao kusoma badala yake wachunge mifugo na watoto wa kike kuolewa

Arusha/ Manyara. Viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali Arusha na Manyara,wameanza kufatilia wanafunzi  waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ambao bado hawajaripoti shuleni.

Mikoa Arusha na Manyara ina  ya wafugaji ambao wamekuwa hawapendi watoto wao kusoma badala yake wachunge mifugo na watoto wa kike kuolewa.

Mkuu wa Mkoa Arusha,John Mongela ametaka wazazi kuhakikisha watoto wote waliofaulu kidato cha kwanza wanakwenda shule.

Mongela ambaye anaendelea na ziara kukagua miundombinu ya shule Wilaya ya Longido baada ya kukamilisha ziara Arusha ameonya wazazi ambao hawatapeleka watoto shule watachukuliwa hatua za kisheria.

"Rais wetu  Samia Suluhu Hassan  ametoa fedha nyingi kwa ajili ya elimu Mkoa wa Arusha ikiwamo kuhakikisha kuna madarasa ya kutosha, madawati na walimu, hivyo Serikali haitegemei kuona watoto wanabaki nyumbani,"amesema.

Mongela ameeleza kuridhishwa na ujenzi wa shule na uwepo wa madawati katika shule nyingi za Arusha.

Wakati huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera amewaagiza maofisa watendaji wa kata  kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaripoti shule.

Dk Serera amesema hayo Leo January 11,2024,baada ya kutembelea shule za msingi na sekondari kukagua mahudhurio ya wanafunzi ikiwa ni baada ya shule hizo kufunguliwa.

"Mtendaji wa kata ya shule husika kama mwanafunzi wa kata nyingine hajafika mpe taarifa ofisa tarafa husika ili afuatilie na kuhakikisha anahudhuria masomo," amesema.

Hata hivyo, amewasisitiza wazazi hasa jamii ya kifugaji kuendelea kupeleka watoto wao katika shule walizopangiwa na kuepuka kuchunga mifugo.

Ametembelea shule mpya ya Lengijape iliyopo Kijiji cha Namalulu, Kata ya Naberera yenye mikondo miwili, madarasa 14 ya shule ya msingi, madarasa mawili ya awali, nyumba za walimu na matundu 24 ya vyoo, ambayo Serikali imeijenga kwa Sh638 milioni.