Maisha ya Malkia Elizabeth II

Muktasari:

  • Kumbukumbu za Uingereza zinamtaja Malkia Elizabeth wa pili kama mtawala aliyeongoza Taifa lililounganisha visiwa mbalimbali kwa muda mrefu zaidi ikilinganishwa na watangulizi wake wa awali.

Dar es salaam. Kumbukumbu za Uingereza zinamtaja Malkia Elizabeth wa pili kama mtawala aliyeongoza Taifa lililounganisha visiwa mbalimbali kwa muda mrefu zaidi ikilinganishwa na watangulizi wake wa awali.

Kiongozi huyo wa kimila amefariki jana Alhamisi, Septemba 8, 2022 akiwa na miaka 96 huku akishikilia rekodi ya kuliongoza Taifa hilo kwa muda wa miongo saba.

Elizabeth alianza kuliongoza taifa hilo akiwa na miaka 25 tu mwaka 1952.

Utawala wake wa muda mrefu ulipitia changamoto mbalimbali ambazo mara kadhaa zilisababishwa na mabadiliko ya dunia ambayo iliilazimu Uingereza kutoka kwenye utawala wa kifalme uliojikita haswa kwenye masuala ya kivita hadi kuwa Taifa la kisasa la kitamaduni ambalo liliheshimu uongozi wa kimila lakini maamuzi mengi yakikabidhiwa mikononi mwa waziri mkuu ambaye alitokana na vyama vya siasa.

Mwananchi imekuandalia kumbukumbu za picha za nyakati tofauti ambazo malkia Elizabeth alizipitia kabla na baada ya kupata wadhifa huo mkubwa wa kiuongozi nchini humo.

Malkia Elizabeth aliyezaliwa Aprili 21, 1926, akiwa amebebwa na mama yake, Elizabeth na Baba yake Mfalme George VI.

Malkia Elizabeth alipokuwa na miaka 14 (kulia) akiwa na dada yake kwa ajili ya matangazo ya redio Oktoba 13, 1940.

Novemba 20, 1947, Malkia Elizabeth alifunga ndoa na Mwanamfalme Philip aliyekuwa luteni kwenye Jeshi la Wanamaji la Uingereza ambaye alikuwa amezaliwa katika familia za kifalme za Ugiriki na Denmark.

Alimuoa baada ya kuukana uraia wake wa awali na kuwa raia wa Uingereza.

Malkia Elizabeth II akiwa kwenye ufunguzi wa Bunge la Uingereza Aprili 1966.

Malkia Elizabeth II akiwa na mtoto wake, Prince Charles, 1969. Charles ndiye anayefuata kuwa kiongozi wa kimila wa Taifa hilo (Mfalme).

Malkia akimkaribisha Boris Johnson katika kasri la Buckingham, ambako alimwalika rasmi baada ya  kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Julai 2019.

Johnson alishinda kinyang’anyiro hicho kwa tiketi ya Chama cha Conservative cha Uingereza na kuchukua nafasi ya Theresa May aliyejiuzulu.

Malkia akiwa amekaa peke yake kwenye mazishi ya mumewe    Aprili 2021.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na watu 30 tu kutokana na vizuizi vya Uviko-19