Majaliwa aagiza hatua mpya makutano ya barabara, reli Tanzania

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Muktasari:
- Kutokana na matukio ya ajali mara kwa mara, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha inafunga taa za tahadhari au kifaa kinachoruhusu na kuzuia magari kwa mfumo wa kidigitali katika kila makutano ya reli na barabara ili kunusuru maisha ya Watanzania.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha inafunga taa za tahadhari au kifaa kinachoruhusu na kuzuia magari kwa mfumo wa kidigitali katika kila makutano ya reli na barabara ili kunusuru maisha ya Watanzania.
Majaliwa amesema Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) washirikiane na Shirika la Reli Tanzania (TRC) uimarisha mifumo katika maeneo hayo ili kudhibiti matukio ya ajali za mara kwa mara zinazohusisha vyombo hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumamosi Desemba 2, 2023, Majaliwa alitoa maagizo hayo wakati akizungumza na wadau mbalimbali kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani katika ukumbi wa Halmashauri ya Dodoma Jiji uliopo Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma.
“Kutokana na umuhimu wa miundombinu rafiki, Tarura na Tanroads wahakikishe wanazingatia mahitaji ya jamii ya watu wenye ulemavu kwa kuweka miundombinu rafiki pamoja na alama mahsusi kwa usalama wa watu wenye ulemavu,” alisema Majaliwa.
Maagizo hyo anayatoa kipindi ambacho kumeshuhudia ajali ya basi la Kampuni ya Ally’s Star lililokuwa linatoka jijini Dar es Salaam kwenda Mwanza kupata ajali eneo Manyoni, Mkoa wa Singida na kusababisha vifo vya watu 13 na majeruhi zaidi ya 30.
Ajali hiyo ilitokea alfajiri ya Jumatano ya Novemba 29, 2023.
Katika tukio hilo, Majaliwa alizindua Mfumo wa Kielektroniki wa Taarifa na Kanzidata kwa Watu wenye Ulemavu unaorahisisha kazi ya kuwatambua watu wenye ulemavu nchini.
Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alisema maadhimisho hayo ya kila mwaka yanalenga kutambua mchango wao katika jamii, kubaini changamoto zao na kuangalia namna bora ya kutatua changamoto hizo.
“Namshukuru Rais Samia kwa namna Serikali imekuwa ikithamini watu wenye ulemavu na kufanyia kazi changamoto zao,” alisema.
Mwakilishi Msaidizi wa UNFPA nchini, Dk Majaliwa Marwa alisema kwa mujibu wa sensa ya Taifa asilimia 9.3 ya Watanzania ni watu wenye ulemavu licha ya namba hiyo inaweza kuongezeka kwani wenye matatizo akili na mtindio wa ubongo huwa wanafichwa majumbani.
“Tunatakiwa tutambue nguvu, uwezo na mchango wa kila mtu mwenye ulemavu katika jamii jhapa nchini na kwa maano hiyo kuwepo kwa mfumo rasmi, kutrasaidia kutambua watu wenye ulemavu nchini na kubainisha vipawa vyao na michango yao,” alisema.