Majaliwa abaini ‘upigaji’ mamilioni, wagawana kama ndizi Serengeti

Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa akizungumza na wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Sokoine vilivyopo Mugumu leo Februari 27. Majaliwa yupo mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku tano. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Muktasari:

  • Majaliwa ameeleza namna watumishi na madiwani wanavyotumia mbinu kuiba fedha za umma.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase amkamate Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Saad Ishabailu akituhumiwa kwa kosa la kuhamisha zaidi ya Sh213.748 milioni kwa awamu nne kwa njia ya uhamisho wa ndani kwa kushirikiana na watumishi wa Ofisi ya Rais (Tamisemi) na kuzitumia kwa matumizi binafsi.

“Mkamate huyo bwana sasa hivi aende polisi akafunguliwe mashtaka, huyu ni wa kupeleka mahakamani moja kwa moja. DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) aelezwe afungue jalada la mashtaka. Wale wenzake tumewapeleka mahakamani tayari sababu tulibaini walihusika na wizi kama huu kwenye Manispaa ya Kigoma mwaka jana,” amesema.

Ametoa agizo hilo leo Jumanne, Februari 27, 2024 alipozungumza na madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwenye kikao kilichofanyika kwenye halmashauri hiyo, mkoani Mara.

Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu imesema Majaliwa amefikia hatua hiyo baada ya kuwaeleza watumishi na madiwani mbinu wanazotumia watumishi wachache wa baadhi ya halmashauri ambao walikuwa wanashirikiana na watumishi watatu wa kitengo cha Treasury Single Account (TSA) kuiba fedha za umma.

Akitoa mfano wa mbinu zinazotumiwa na wachache hao, amesema Juni 10, 2023 walitumia mwanya wa kuombea kibali fedha za bakaa kwa barua iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Chatta Luleka, kwenda Hazina.

“Ilipofika Juni 30, walikuwa wamemaliza kutumia fedha hizo na ikabakia Sh9 milioni lakini kwa kuwa walishaandika barua ya kuomba kibali, bado fedha hizo zilihamishwa na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri Juni 19, 2023 na aliyejua alikuwa Ishabailu peke yake. Hakutoa taarifa kwa mkurugenzi, mwenyekiti wala wakuu wa idara,” amesema na kuongeza:

“Nilituma timu yangu hapa ije kufanya uchunguzi, ikawahoji baadhi ya watumishi akiwemo ofisa mipango wa halmashauri, Wilfred Mwita ambaye amesema hajui uwepo wa hizo fedha wala hawakuwa na mpango wala bajeti inayohitaji fedha hizo. Mkurugenzi wa sasa, Furaha alipoulizwa naye amesema hajui uwepo wa fedha hizo, kwani alianza kazi Agosti, mwaka jana.”

Amedai Juni 21, 2023 Ishabailu alianza kufanya matumizi ya fedha hizo kwa kushirikiana na mfanyabiashara mmoja wa  Mugumu, kupitia kwenye akaunti zake za NMB na CRDB kwa kupitia miamala minne ya Sh76.3 milioni, Sh57.7 milioni, Sh47 milioni, na Sh32.5 milioni.

Amesema alipoulizwa na timu ya uchunguzi mfanyabiashara huyo (jina tunalo) alikiri kuwa haidai fedha yoyote Halmashauri ya Serengeti isipokuwa Mweka Hazina aliomba apitishie fedha zake kwenye akaunti zake kwa sababu zinahitajika haraka kwa matumizi ya ofisi.  “Aliambiwa atoe Sh189 milioni akamkabidhi zote Ishabailu na zilizobakia (Sh24 milioni) akaambiwa abaki nazo,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema” “Baada ya kupokea fedha hizo, Ishabailu alipanda basi kutoka Serengeti hadi kituo cha mabasi cha Nyegezi, Mwanza na kumkabidhi Zablo Mponzi ambaye alisema zinatakiwa haraka na wakubwa Dodoma, bila kuwataja wakubwa hao ni kina nani. Yeye pia alikabidhi Sh150 milioni kwa huyo Zablo, ina maana alibakia na Sh39 milioni.”

Amewasisitiza madiwani na watumishi wawe makini na matumizi ya fedha za umma kwani Rais Samia Suluhu Hassan anapotafuta fedha na kupeleka kwenye halmashauri, anataka ziende kutatua kero za wananchi walio wengi.

Katika hatua nyingine, Majaliwa amekemea tabia aliyosema imeanza kusambaa ya baadhi ya watumishi wa halmashauri kubana fedha za miradi na kuzitumia kinyume cha mipango.

"Jana nilikuwa Bunda na leo hapa Butiama nimekuta huu mchezo ambao halmashauri yenu inatumika kama kichaka. Wachache wenye mamlaka humu ndani wanatumia mwanya wa mwisho wa mwaka wa fedha na kuhamisha fedha zilizoletwa kutoka Serikali Kuu ili ziendeshe miradi," amesema na kuongeza: 

''Hii tabia imeanza kusambaa, hawa wanamhujumu mkuu wa nchi ambaye anatafuta fedha za maendeleo usiku na mchana, pia wanaihujumu halmashauri na wananchi wa wilaya ya Butiama sababu hii ni kodi yao."