Majaliwa amtembelea Lowasa hospitalini Afrika Kusini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na mke wa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, Regina Lowassa, (wa tatu kushoto) na Fredrick Lowassa (kulia) alipoenda kumjulia hali Lowassa anayepata matibabu jijini Johannesburg, Afrika ya Kusini. Wa pili kushoto mke wa Majaliwa, Mary Majaliwa na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Jumatano Desemba 28, 2022 amemtembelea Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowasa anayepatiwa matibabu nchini Afrika ya Kusini.

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo Jumatano Desemba 28, 2022 amemtembelea Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowasa anayepatiwa matibabu nchini Afrika ya Kusini.

  

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha Habari inasema Majaliwa alikwenda Johannesburg, Afrika Kusini kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.


Akiwa hospitalini hapo Majaliwa amezungumza na familia ya Lowasa na kuwaambia Rais Samia yupo pamoja na familia hiyo na wanamuombea uponyaji mstaafu huyo.


"Rais anafuatilia kwa kila hatua kuhusu hali ya mheshimiwa Lowasa na anamuombea uponyaji wa haraka," inanukuliwa sehemu ya taarifa hiyo.


Mama Regina, mke wa Lowasa ametoa pongezi kwa Serikali na Rais kwa namna ambavyo wamekuwa karibu na familia hiyo katika kumuuguza kiongozi huyo wa zamani.


Amemuomba Majaliwa kufikisha shukrani zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan na kuomba Watanzania waendelee kumuombea Lowasa.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtoto mkubwa wa Lowasa ambaye ni mbunge wa Monduli, Fredrick Lowasa amewashukuru Watanzania kwamba wamekuwa wakimuombea Mzee wao uponyaji lakini akaomba waendelee hivyo.

Lowasa alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika Serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete na alihudumu kwa miaka miwili na nusu kabla ya kujihuzulu mwaka 2008 kutokana na kashfa ya Richmond.