Majaliwa aonya rushwa uchaguzi wa Serikali za mitaa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwasha Mwenge wa Uhuru kwenye maadhimisho ya uzinduzi wa Mwenge huo, yaliyofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro Aprili 2, 2024. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu


Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa  amewataka wananchi kote kuwakataa na kuwapiga vita  viongozi wanaotoa rushwa ili wachaguliwe kwenye nafasi mbalimbali za uongozi

Moshi. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa  amewataka wananchi kuwakataa na kuwapiga vita  viongozi wanaotoa rushwa ili wachaguliwe kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.

Majaliwa amesema hayo leo Aprili 2 2024  wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa uliofanyika katika Viwanja vya chuo Kikuu cha Ushirika(MoCU), Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ikiwa na kauli mbiu:  "Tunza mazingira na  shiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa ujenzi wa taifa endelevu."

Amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa  kugombea nafasi za uongozi huku akiwataka wananchi kuwachagua viongozi waadilifu na wanaochapwa kazi.

"Kwa kuwa mwaka huu ni uchaguzi wa Serikali za mitaa wananchi wote epukeni kujihusisha na vitendo vya rushwa, kwa kiongozi anayetoa rushwa kuomba kuchaguliwa ili awe kiongozi, hafai na apigwe vita kwa tabia yake ya kutoa rushwa ili aweze kuchaguliwa,"amesema Majaliwa.

"Kila Mtanzania aepuke kushiriki kwenye vitendo vya rushwa na  atoe taarifa kuhusu viashiria au vitendo vya rushwa, kila Mtanzania anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa na wale ambao wanakusudia kufanya hivyo mwezi wa 10 ni fursa yao,  siku ya uchaguzi mjitokeze kwa wingi kushiriki kuchagua viongozi wetu ili kudumusha amani na utulivu."

Amewataka wananchi kwenda kuhakiki majina yao kwenye daftari la wapigakura kwenye maeneo yao  ili kupunguza malalamiko wakati wa kipindi cha uchaguzi.

 "Tunaposubiri kuelekea kwenye uchaguzi, zoezi la uandikishaji wa wapiga kura limeshaanza, nenda kahakiki kama jina lako liko sawasawa kwenye maeneo ulipo ili kuzuia malalamiko kipindi cha uchaguzi kwa kukosekana kwa jina lako," amesema Majaliwa.


 Neno kwa wakimbiza Mwenge wa Uhuru

Majaliwa amewataka wakimbiza Mwenge wa Uhuru kulitendea haki Taifa na kuhakikisha wanahakiki miradi yote na ile watakayoibaini kuwa mibovu, kuitolea taarifa ili  hatua ziweze kuchukuliwa haraka.

Pia, amewataka kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru, kuhamasisha ushiriki wa wananchi kwenye shughuli za maendeleo na kufichua vitendo vyote vya ubadhirifu bila woga.

"Mmeaminiwa na kupewa jukumu hili kubwa la kitaifa, nyeti na muhimu kwa Taifa letu, nendeni mkalitendee haki Taifa hili, kwa kufanya kazi mliyoaminiwa na kupewa, tunaamini tabia zenu njema na nidhamu ya kutosha mnayo. Lakini mkahakiki miradi yote, miradi mibovu yote isemeni na kuiandikia ripoti kama ilivyokuwa miaka yote, wapi kuna tatizo tuende tukachukue hatua, taifa hili linawategemea,”amesema Majaliwa.

"Ajenda zetu zote za kitaifa zisemeni kwa wananchi, hakikisheni wananchi wanaokuja wanaondoka na ujumbe uliokusudiwa."

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akmkabidhi Mwenge wa Uhuru  Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Godfrey Mzava kwenye maadhimisho ya uzinduzi wa Mwenge wa Uhuru, yaliyofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro Aprili 2, 2024. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu


Tatizo la lishe nchini

Waziri Mkuu amesema bado kuna tatizo la lishe nchini na kwamba ni kutokana na mtindo wa maisha watu wanayoishi.

Kwa mujibu wa takwimu ya mwaka 2022, taarifa zinaonyesha, hali ya lishe miongoni mwa Watanzania sio ya kuridhisha na kwamba asilimia 30 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanakabiliwa na tatizo la udumavu, asilimia 12 wana uzito pungufu na asilimia 3 wana ukondefu.

"Suala la lishe ni muhimu tunapofikia kwenye suala la msingi wa maendeleo na ustawi wa Taifa letu, Serikali imekuwa ikifanya jitihada nyingi kutokomeza aina zote za utapiamlo pamoja na kuweka mifumo katika mipango yote ili iweze kuwafikia wananchi wote na kuendelea kusisistiza kula  chakula chenye virutubisho vyote,"amesema.

Ameitaja mikoa inayongoza kwa kiwango kikubwa cha udumavu wa watoto kuwa ni mikio ya Iringa, Njombe, Rukwa, Geita, Ruvuma, Kagera, Simiyu, Tabora, Katavi Manyara,  Songwe na Mbeya huku Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa hauna changamoto hiyo kabisa.

"Tunayo asilimia 42 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa nao wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa damu, tatizo la  uzito uliozidi na viribatumbo, inaelekea kuwa  ni janga la Kitaifa lakini pia inakuwa nikisababishi kikubwa cha ongezoko la magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari,  saratani na magonjwa ya moyo,"amesema Majaliwa.

Amesema magonjwa yasiyoambukiza  yanasababishwa na mtindo wa maisha wa kuacha kufanya mazoezi.


 Uharibifu wa mazingira

Majaliwa amesema Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la uharibifu wa mazingira na kusema tatizo hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu.

"Mbio za Mwenge mwaka huu zinaendelea kusisitiza umuhimu wa kutunza mazingira kwa maendeleo endelevu kwa Taifa letu, kwa kupanda miti, uhifadhi wa vyanzo vya maji na ardhi oevu,"amesema Majaliwa.

"Kutokana na athari hizi, kila mmoja awe sehemu ya kuotesha miti na utunzaji wa mazingira, Serikali tayari imeshaweka mifumo imara ili kukabiliana na tatizo hili."

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),  Dk Selemani Jafo amesema Mwenge wa Uhuru unaleta faraja kubwa kwa nchi hasa katika suala zima la utunzaji wa mazingira na kwamba  ajenda ya mazingira ndio changamoto kubwa sana ya dunia hivi sasa.

"Mwenge wa Uhuru mwaka huu umeleta faraja kubwa katika utunzaji wa mazingira, binafsi niseme tunaposherehekea miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni faraja kubwa hasa katika sherehe za mwaka huu.

 "Kwa kuwa Mwenge huu utakimbizwa mikoa yote hapa nchini, ajenda hii na ujumbe huu utaweza kuwasaidia Watanzania kuelewa namna nzima ya utunzaji wa mazingira, imani yetu ni kwamba tutakapotunza mazingira tutapata faraja kubwa ya kuijenga nchi yetu, kwa sababu tunafahamu ajenda ya mazingira ndio changamoto kubwa sana ya dunia hivi Sasa,”amesema Dk Jafo.

Amesema Mwenge wa mwaka huu unaenda kujibu hoja za msingi hasa za kidunia ikiwa ni pamoja na wananchi kutunza mazingira yanayowazunguka katika jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kilomita 1,113 ndani ya mkoa huo ukizindua, kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 47 ambayo imegharimu zaidi ya Sh29 bilioni.

"Baada ya tukio hili la Mwenge kuzinduliwa leo, utakimbizwa katika halmashauri sa za mkoa huu, kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kukagua miradi mbalimbali, mbio hizo ni kichocheo kikubwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo hapa Mkoani kwetu,"amesema Babu.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu mkoa huo umepokea fedha Sh828 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji, barabarani, miundombinu ya umeme pamoja na sekta nyingine mbalimbali.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu), Protas Katambi amewataka wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuzingatia itifaki ya Mwenge pamoja na maagizo na maelekezo yatakayotolewa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na viongozi wa mbio za Mwenge.

"Viongozi wote, wakuu wa mikoa na wilaya wazingatie itifaki ya Mwenge lakini pia wazingatie maagizo na maelekezo yatakayotolewa kupitia ofisi ya Waziri Mkuu na viongozi wa mbio za Mwenge.”

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Mwita amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika mikoa 31 na halmashauri 195 na kwamba utakimbuzwa na vijana sita kutoka Bara na Zanzibar.

"Kazi hii itafanywa na vijana sita kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, vijana wameandaliwa kikamilifu kuhakikisha wanaendelea kufikisha kwa ufasaha ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu, kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwa umakini wa hali ya juu na kuhakikisha fedha zote zinazotolewa na Rais Samia kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania zimetumika ipasavyo."