Mbio za mwenge Chunya zafikia miradi ya Sh2.9 bilioni

Kiongozi wa Mbio za mwenge kitaifa, Abdallah Shaibu (kulia) ni mwekezaji Saimon Shinsh akizindua maabara ya upimaji sampuli za madini ya dhahabu uliogharimu fedha za Kitanzania zaidi ya  Tsh.900 milioni ambao unamilikiwa na wekezeji wazawa ambao Endew Shinsh na Simon Shinsh. Picha Mery Mwaisenye

Chunya. Mwenge wa uhuru umemaliza mbio zake wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya ambapo umetembelea tarafa mbili na Kata 12, huku ukiifikia miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya Sh2.9 bilioni.

Akitoa ujumbe wa Mwenge mwaka 2023 kwenye vijiji tofauti, Katika mbio hizo, Kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Abdallah Shaib Kaim, amewataka wakandarasi wanaosimamia miradi ya maendeleo kuhakikisha wanasimamia miradi vyema ili kuhakikisha Serikali haipati hasara.

Aidha, amewataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara, kupinga rushwa, kutoa elimu ya madawa ya kulevya na kuhakikisha wanazingatia utunzaji wa mazingira ili kuepukana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Kama kauli mbiu ya mwenge inavyosema, ‘Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na kwa Uchumi wa Taifa,’ tuhakikishe tunazingatia sana suala zima la utunzaji mazingira kwa maslahi yetu na taifa kwa ujmla,” amesema.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Lupa, Masache Kasaka, akitoa salama kwa wananchi, ametumia nafasi hiyo kufikisha ombi la wananchi hao, la kuijenga kwa kiwango cha lami, barabara inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Tabora.

Kasaka amesema barabara hiyo ikijengwa kwa kiwango cha lami itarahisisha mawasiliano na mikoa jirani.

"...naomba utufikishie kilio chetu wananchi wa Chunya, kuhusu ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mamlaka ya Mji Mdogo Chunya, kwenya Tabora kwani kujengwa kwa barabara hiyo kutarahisisha usafiri kwa mikoa jirani,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka, yeye aliukabidhi mwenge huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ili aukabidhi kwa mwenzie wa Tabora, huku akimhakikishia juu ya utekelezwaji wa maelekezo waliyopewa na kiongozi wa mbio hizo.