Mwenge watua Mbeya, kupitia miradi ya Sh36.4 bilioni

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Francis Michael akimkabidhi mwenge wa uhuru mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera

Muktasari:

  • Jumla ya miradi 45 yenye thamani ya zaidi Sh36.4 bilioni mkoani Mbeya inatarajiwa kukaguliwa, kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi na wakati wa mbio za mwenge wa uhuru, zilizoanza leo Septamba 7, 2023; mkoani hapa.

Mbeya. Jumla ya miradi 45 yenye thamani ya zaidi Sh36.4 bilioni mkoani Mbeya inatarajiwa kukaguliwa, kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi na wakati wa mbio za mwenge wa uhuru, zilizoanza leo Septamba 7, 2023; mkoani hapa.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya mwenge huo kutoka mkoani Songwe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa, amesema mwenge huo ukiwa mkoani humo utakagua na kuwekewa mawe ya msingi katika halmashauri zote.

"Nakiri kuupokea mwenge ukiwaka, matarajio yangu ni kuhakikisha miradi 45 yenye thamani ya Sh36.4 bilioni ikikakaguliwa, kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa," amesema Malisa.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio hizo kitaifa, Shaibu Kaimu, ameomba ushirikiano toka kwa Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jafari Haniu, ambako ndiko mbio hizo zimeanzia, kwa kuandaa taarifa za miradi, uwepo wa wataalamu na wakuu wa miradi katika kila eneo ambako mwenge utafika.

Ameongeza kuwa lengo la uwepo wa mwenge katika halmashauri nchini ni kuhamasisha maendeleo na kutetea amani, na kwamba matarajio ya wakimbiza mwenge huo, ni kukamilisha shughuli hizo za ujenzi wa taifa.

"Tunapokuwa katika mradi wowote, naomba uwepo wa wakuu wa idara, vifaa vya kupimia, wataalamu, taarifa za miradi na ushirikiano wenu, lengo kubwa la mwenge ni kutetea amani na kuchochea maendeleo,” amesema Kaimu.

Kwa upande wake, DC Haniu amesema kuwa kwa muda wote ambao mwenge utakuwa katika Halmashauri yake ya Rungwe, atahakikisha shughuli zote zinaenda vizuri.

"Na kwa leo tunaanzia katika mradi wa maji Ikuti, ambao utawekwa jiwe la msingi, mradi huu unagharimu Sh2 bilioni na niwahakikishie shughuli hii katika halmashauri hii zitaenda vizuri," amesema Haniu.