Mwenge kuwashwa Kilimanjaro 2024

Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa kiongozi wa Mbio hizo, Abdallah Shaibu Kaimu wakati wa Maadhimisho ya Kilele cha mbio hizo katika uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara leo Oktoba 14, 2023.

Muktasari:

  • Kwa mwaka huu 2023 mwenge wa uhuru uliwashwa Mkoani Mtwara na kilele chake kufanyika Mkoani Manyara.

Babati. Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024, zitaanzia Mkoa wa Kilimanjaro ambako utawasha, huku sherhe za kuhitimisha mbio hizo zikifanyika mkoani Mwanza.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (KaziVijanaAjira na Wenye Ulemavu), Prof Joyce Ndalichako ameyasema hayo leo Jumamosi Oktoba 14, 2023; mjini Babati, Mkoa wa Manyara, kwenye sherehe za kilele cha mbio hizo.

“Kilimanjaro kutafanyika uzinduzi kule baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipowasha Mwenge na kilele chake kitafanyika jijini Mwanza, kikienda sambamba na kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa na wiki ya vijana kitaifa,” amesema Prof Ndalichako.

Kiongozi wa mbio hizo kitaifa kwa mwaka huu, Abdalah Shaibu Kaim amesema miradi saba pekee yenye thamani ya Sh1.9 bilioni ndiyo ambayo haikukubaliwa.

Kaimu amesema miradi hiyo ni asilimia 0.5 ya miradi yote ya maendeleo nchini na kwamba wameikabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia imewapatia Sh535 bilioni za kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.

Sendiga amesema fedha hizo zimefanikisha miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara.

Amesema mbio hizo zimewapatia uwanja mzuri wa michezo uitwao Tazanite Kwaraa uliopo mjini Babati ambapo ndipo maadhimisho hayo yalipofanyika.

"Madini ya Tanzanite yanapatika Manyara pekee hapa duniani na tunaendelea na ujenzi wa soko la madini hayo ambalo lipo kwenye hatua ya ukamilishaji ili kuongeza mnyororo wake wa thamani," amesema Sendiga.