Majaliwa apokewa jeshini, kuanza mafunzo Handeni

Kijana shujaa katika ajali ya ndege ya Precision Air, Majaliwa Jackson akiwa ofisi ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kagera akipokelewa na Kamanda wa Mkoa kamishna msaidizi mwandamizi, Zablon Muhumha. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Kijana shujaa katika ajali ya ndege ya Precision Air, Jackson Majaliwa amepokewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na anatarajiwa kupata mafunzo katika chuo cha Chogo kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga.

Dar es Salaam. Kijana shujaa katika ajali ya ndege ya Precision Air, Jackson Majaliwa amepokewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na anatarajiwa kupata mafunzo katika chuo cha Chogo kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga.

Katika ajali hiyo iliyotokea Novemba 6, 2022, Majaliwa ambaye ni kuuza dagaa katika mwalo wa Nyamkazi uliopo katika manispaa ya Bukoba, alionyesha ujasiri wa kwenda ndege iliyoanguka haraka na kufanikiwa kuvunja mlango wa ndege na kuwezesha abiria 24 kutoka wakiwa wazima.

Wakati wa kuaga miili ya watu 19 waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametaka kijana huyo akabidhiwe kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ili aingizwe kwenye Jeshi la Zimamoto kwa ajili ya kupatiwa mafunzo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Novemba 7, 2022, na Msemaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Puyo Nzalayaimisi, tayari kijana huyo amepokewa na jeshi hilo na atapewa mafunzo rasmi ya zimamoto, uokoaji na uaskari.

“Mkuu wa Jeshi wa Zimamoto na Uokoaji, Kamishna Jenerali John Masunga anaujulisha umma kuwa Majaliwa Jackson Samweli, ameshapokelewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Hivyo, maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, yameshatekelezwa.

“Majaliwa anatarajiwa kuanza mafunzo ya zimamoto na uokoaji pamoja nay a uaskari katika Chuo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilichopo Chogo, wilaya ya Handeni mkoani Tanga,” inaeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba Kamishna Jenerali anatoa shukrani kwa vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi wa mkoa wa Kagera kwa ushirikiano mkubwa waliotoa wakati wa uokoaji katika ajali hiyo.

“Kamishna Jenerali anatoa pole kwa wafiwa wote na kumwombea faraja katika kipindi hiki kigumu wanachopitia, anawatakia majeruhi wote afya njema. Anawasihi wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Zimamoto katika kuokoa maisha ya watu na mali dhidi ya majanga mbalimbali,” amesema Nzalayaimisi katika taarifa yake kwa umma