PW 494: Mvuvi aliyefanikisha uokoaji kuajiriwa jeshini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpongeza na kumfariji kijana Jackson Majaliwa kwa ushujaa wake wa kuwahi katika eneo ilipotokea ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air na kuwaokoa abiria 24 waliokuwa wameshindwa kutoka ndani ya ndege hiyo.

What you need to know:

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza kijana Jackson Majaliwa, mvuvi wa Bukoba aliyefanikisha abiria 24 wa ndege ya Precision Air iliyopata ajali kuajiriwa kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Bukoba. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameagiza kijana Jackson Majaliwa, mvuvi wa Bukoba aliyefanikisha abiria 24 wa ndege ya Precision Air iliyopata ajali kuajiriwa kwenye Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Hilo limesemwa leo Jumatatu, Novemba 7, 2022 na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati wa ibada maalum ya kitaifa ya kutoa heshima za mwisho kwa miili 19 waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea jana Jumapili.

Majaliwa Jackson, mvuvi aliyefanikisha kuufungua mlango wa ndege na kufanikisha kuokolewa kwa abiria 24 waliokuwa ndani ya ndege ya Precision Air iliyotumbukia Ziwa Vickoria.

Majaliwa amesema pamoja na mambo mengine, kijana huyo atapewa mafunzo zaidi ya uokoaji na kujengewa ujasiri wa kushiriki shughuli mbalimbali za uokoaji.

"Rais Samia ameguswa na ujasiri wa kijana huyu na ameiagiza wizara ya mambo ya ndani kumwajiri katika Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa ajili ya mafunzo zaidi na kumjengea ujasiri.

Miili 19 ya waliofariki ajali ya ndege ikiagwa Kaitaba

“Nakuagiza waziri wa mambo ya ndani kutekeleza hilo haraka kwa kuchukua maelezo yote muhimu ya kijana huyu jasiri kwa hatua zingine," amesema Majaliwa

Pamoja na kijana huyo, Majaliwa amesema Serikali inatambua juhudi na jitihada za wavuvi wengine waliosaidia uokoaji huku akiahidi taratibu zitafanyika kuwawezesha.


Kijana Majaliwa Jackson tayari amekabidhiwa zawadi ya Sh1 milioni kama ishara ya kutambua juhudi na moyo wake wa kujitolea zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila.

Katika juhudi hizo, Majaliwa alijeruhiwa na mlango wa ndege na kukimbizwa hoaspitali ya rufaa mkoa wa Kagera kwa matibabu akiwa na majeruhi wengine 25 wa ajali hiyo wakiwemo abiria 24 na mfanyakazi wa uwanja wa ndege wa Bukoba aliyezimia kwa mshtuko.


Waziri Mkuu Majaliwa pia ametangaza kuwa Serikali itagharamia mazishi ya wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo na kuwaagiza wakuu wa mikoa kusimamia suala hilo.