Majaliwa awaasa madereva kuwafichia siri viongozi

Waziri Mkuu Kassim wakati alipohudhuria ufunguzi wa Kongamano la pili la Chama cha Madereva wa Serikali mkoani Morogoro.
Morogoro. Waziri mkuu Majaliwa Kasim Majaliwa amewaonya madereva wa Serikali kuacha tabia ya kutoa siri za viongozi wanaowaendesha kwani kufanya hivyo ni utovu wa nidhamu na maadili ya utumishi wa umma.
Majaliwa alitoa onyo hilo jana mjini hapa wakati akifungua kongamano la pili la Chama cha Madereva wa Serikali ambapo pamoja na kutunza siri lakini pia amewataka madereva hao kutambua mipaka na majukumu yao ya kazi kwa maslahi mapana ya nchi.
"Ukiwa dereva wa Serikali kuna vitu hupaswi kufanya hata kama unadhani ni haki huwezi kunywa au kucheza mziki mpaka saa tisa usiku hali ya kuwa asubuhi uko safarini, wapo madereva wengine wanadai wakinywa ndio wanakuwa vizuri barabarani, nawaambia hicho kitu hakipo," amesema Majaliwa.
Amewataka madereva wa Serikali kufuata sheria za nchi na sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali kwa kuwa uwepo wao Serikali hakuwafanyi wawe juu ya sheria.
Pia Majaliwa ameiitaka jeshi la polisi kutoa elimu Kwa madereva kuhusu matumizi ya ving'ora na 'vimulimuli' kwenye magari ya Serikali kwani amesema kuwa sasa hivi imeonekana magari mengi yanafungwa kiholela ving'ora na 'vimulimuli' bila kufuata sheria na kuongeza kuwa sio kila gari linaweza kuwekewa vitu hivyo.
Amekemea pia tabia ya baadhi ya madereva kuegesha magari kwenye nyumba za starehe na gereji bubu jambo ambalo ni hatari Kwa usalama wa magari wanayoendesha.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili madereva wa Serikali ya gharama za matengenenezo madogo madogo na usafi wa gari wanazotoa madereva kupitia fedha zao za mifukoni ambapo waziri mkuu aliagiza gharama hizo zitolewe na waajiri.
Amesema katika kutatua changamoto hizo Serikali muundo kwa kuondoa cheti Cha ufundi katika kupandisha madaraja madereva wa Serikali.
Katika hatua nyingine Waziri mkuu Majaliwa amewataka baadhi ya viongozi kuacha tabia ya kuchukua posho za madereva wao wanapokuwa safarini na kuwapangia matumizi madereva jambo ambalo amesema kuwa linanyima uhuru madereva wao.
"Nasisitiza posho za madereva wapewe madereva wenyewe tena ikiwezekana wapewe hata kabla ya safari ili waweze kujikimu na pia waweze kuachia familia zao," amesema Majaliwa.
Awali akitoa salamu za Wizara, waziri wa ujenzi Inocent Bashungwa ameahidi wizara kushirikiana na chama cha madereva wa Serikali ili kulifanya kongamano la mwakani liwe la kipekee.
Bashungwa amesema kuwa Wizara imeahidi kutekejeza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mazingira ya ufanyaji kazi wa madereva wa Serikali yanaboreshwa.
Amesema kuwa katika kuboresha kada hiyo ya madereva wa Serikali wizara imejipanga kuhakikisha chuo cha Taifa cha usafirishaji kinatoa mafunzo Bora Kwa kuwa jamii imekuwa ikiwanyooshea vidole baadhi ya madereva kwa kuvunja sheria za usalama barabarani.
Katika risala yao iliyosimwa na katibu wa chama hicho Castory Mvale madereva hao wameeleza changamoto nyingine zinazowakabili ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi kukaa kwenye nyumba za starehe hadi usiku huku wao wakiwasubiri na baadhi ya viongozi kupenda kusafiri usiku hata Kwa zile safari zisizokuwa za lazima.
Kuhusu ukuaji wa chama katibu huyo amesema kuwa chama hicho kilianzishwa kwaka 2013 na kupata usajili mwaka 2015 ambapo Kwa sasa kina jumla ya wanachama zaidi ya 550 kutoka kwenye wanachama 300 mwaka 2022.
Ametaja baadhi ya mada zitakazofundishwa katika kongamano hilo kuwa ni pamoja na maadili ya utumishi wa umma, Teknolojia ya matumizi ya magari ya kisasa yanayotukiwa na Serikali, afya ya akili, elimu kuhusu mifuko ya hifadhi ya jamii.
Akizungumza Kwa niaba ya madereva wenzake wanawake Habiba Msangi kutoka mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira jijini Mwanza ameishukuru Serikali kwa kuwaamini kuendesha viongozi japo kuwa baadhi ya taasisi zimekuwa bado hazina imani na madereva wanawake hasa pale yanapokija magari ya kisasa au mapya ambapo magari hayo wamekuwa wakipewa madereva wanaume.
Ametaja idadi ya madereva wanawake ambapo alisema katika taasisi hiyo ya mamalaka ya maji na usafi wa mazingira yupo dereva mwanamke peke yake na katika wizara wapo madereva wawili wakati nchi nzima wapo madereva wanaokadiliwa kuwa 42.