Majaliwa: Michango maendeleo shuleni haijazuiwa
Dodoma. Serikali imesema michango yenye kupeleka maendeleo mashuleni haijazuiwa, isipokuwa inachangishwa chini ya wakuu wa wilaya au mtu atakayeteuliwa kwa niaba.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Juni Mosi, 2023 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kusini (CCM), Ally Kasinge.
Katika swali lake Mbunge huyo amehoji licha ya Sera ya elimu bure lakini kumekuwa na michango mingi akauliza kama serikali haioni haja ya kuwapunguzia wazazi mzigo wa michango hiyo.
Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutekeleza sera ya elimu bila malipo ambapo kila mwaka inapeleka fedha kwa walimu kwa ajili ya kulipia gharama ambazo zingeweza kuwafanya wazazi kutolipa michango.
“Natambua kuwa siyo maeneo yote yanapata fedha hasa chakula na eneo la ulinzi, kwa sasa tunashughulika na maboresho ya sera na kuona namna gani tutafanya katika jambo hilo kwani bado tunaendelea kuchakata ili tutoe huduma nzuri ya chakula,” amesema Majaliwa.
Ameomba wananchi kuendelea kuchangia michango ambayo itakuwa na tija ya kimaendeleo badala ya ile ya kusema walimu kusema njoo kesho na Sh200 ambayo ni kero.
Ametolea mfano wa michango ya maendeleo ni mfano wa ujenzi wa choo cha shule kama kimebomoka ambayo amesema haitazuiliwa kwani haliondoi maboresho kwa wazazi kusimamia elimu ya watoto wao.