Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa: Tanzania itajifunza Cuba kuvutia watalii, ampa maagizo Polepole

Muktasari:

  • Tanzania imeahidi kuendeleza ushirikiano baina yake na Cuba katika nyanja mbalimbali za elimu na utalii.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali za Tanzania na Cuba zitaendelea kushirikiana katika sekta za elimu, afya, kilimo, utalii na masuala ya teknolojia. 

Ameeleza hayo baada ya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Cuba, Salvador Valdes Mesa yaliyofanyika Revolutionary Square, Havana nchini Cuba, jana Jumanne, Agosti 13, 2024.

Majaliwa ambaye yuko nchini Cuba kwa ziara maalumu ya siku mbili kwa ajili ya kuboresha mahusiano baina ya Tanzania na Cuba, amesema Wizara za Elimu za Tanzania na Cuba zinaendelea kutekeleza makubaliano ya muda mrefu ambapo Watanzania wengi wamesoma na wanaendelea kusomea udaktari nchini humo. 

Aidha, ameeleza kuwa Wizara ya Afya Tanzania imekuwa ikiwaalika madaktari bingwa kutoka Cuba kuja Tanzania kushirikiana na madaktari wa Kitanzania kutoa huduma ya matibabu ya kibingwa kwa katika maeneo mbalimbali nchini. 

“Tumeshuhudia mara kadhaa madaktari kutoka Cuba wakija Tanzania kufanya kazi katika hospitali kama vile Muhimbili, Mloganzila, Bugando, KCMC na Dodoma na wakati wote wamefanya kazi zao kwa bidii na uzalendo. Nimemuhakikishia Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa tuendelee kuuenzi ushirikiano huo wa kidugu,” amesema. 

Kuhusu sekta ya utalii, Majaliwa amesema Tanzania inayo mengi ya kujifunza kutoka Cuba kwani nchi hiyo imefanikiwa sana kukuza utalii wa fukwe baada ya kuwa imejenga hoteli za kitalii, miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na kuwa na utaratibu mzuri wa magari ya kubeba watalii.

“WaCuba wanapokea watalii wengi sana, upo umuhimu mkubwa kwetu kujifunza mbinu wanazotumia kuwavutia kutoka sehemu mbalimbali duniani.”

Vilevile katika kikao hicho, suala la kukuza lugha ya Kiswahili lilijadiliwa ambapo ubalozi wa Tanzania nchini Cuba ukiongozwa na Balozi Humphrey Polepole, umejitwika jukumu la kusimamia mchakato mzima wa kufundisha na kuifanya lugha hiyo  izungumzwe na kusambaa nchini humo na katika nchi za Latin Amerika. 

“Hivi sasa Kiswahili kinafundishwa katika vyuo vikuu nchini Cuba na wanachuo wengi wanajitokeza kujifunza,” amesema.

Balozi  Polepole amesema ziara ya Waziri Mkuu nchini Cuba imekusudia kukuza uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kibayoteknolojia na katika maeneo ya taaluma kwa faida ya nchi mbili hizo. 

Kuhusu Kiswahili, Balozi Polepole amesema Majaliwa ameuelekeza ubalozi wa Tanzania uendelee na maandalizi ya Kongamano la Kimataifa la Kiswahili linalotarajiwa kufanyika Havana nchini Cuba Novemba 7-9, 2024. Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.