Majeruhi wawili ajali ya Somanga wahamishiwa Muhimbili kwa matibabu

Gari ndogo ainaya Mazda iliyogongana uso kwa uso na lori la mafuta na kusababisha watu 13 kufariki na 6 kujeruhiwa jana.Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Gari dogo la abiria aina ya Mazda lililokuwa likitokea Somanga kuelekea Nangurukuru, jana liligongana uso kwa uso na lori la mafuta katika barabara kuu ya Lindi – Kibiti na kusababisha vifo vya watu 13 na majeruhi 6.

Lindi. Majeruhi wanne kati ya sita wa ajali iliyotokea jana Jumatatu Aprili 22, 2024 eneo la Somanga, wameruhusiwa kutoka hospitalini walikokuwa wakitibiwa.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa majeruhi wengine wawili walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Ajali hiyo iliyoua watu 13, ilihusisha gari dogo la abiria aina ya Mazda na lori la mafuta ambayo yaligongana uso kwa uso.

Akizungumza leo Jumanne Aprili 23 ,2024 Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Sokoine Mkoani Lindi, Alexander Makalla amesema majeruhi mmoja aliyefikishwa hospitalini hapo na kupokelewa katika kitengo cha dharura, alipatiwa matibabu na kuruhusiwa jana ileile.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kinyonga walikopelekwa majeruhi baada ya ajali hiyo, Dk Manda Shabani amesema wagonjwa wanne ambao mmoja alilazwa hospitali ya Tingi na watatu aliyelazwa Kinyonga na baadaye Hospitali ya Sokoine wote walisharuhusiwa, lakini wagonjwa wawili walipelekwa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Dk Shabani amewataja majeruhi waliopelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwa ni Ingawaje Mnola (30) na Kassim Saidi (30).

Jana akizungumza baada ya kutokea ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, John Imori alisema ilitokea Saa 1:30 asubuhi.

Alisema gari dogo la abiria aina ya Mazda lililokuwa likitokea Somanga kuelekea Nangurukuru, liligongana uso kwa uso na lori la mafuta katika barabara kuu ya Lindi – Kibiti.

"Huyu dereva wa lori alihama upande wake na kulifuata gari la abiria bila kuwa na tahadhari yoyote na kusababisha vifo vya watu 13,” alisema Kamanda Imori.

Alifafanua kuwa madereva wa magari hayo wanashikiliwa na  Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.