Maji yaweka rehani kibarua cha makamu wa Rais

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi wa Usanifu na Usimamizi wa Miradi ya Maji wa Wizara ya Maji, Mhandisi Abbas Muslim wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe  alipotembelea chanzo cha mradi huo eneo la la Nyumba ya Mungu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro leo Machi 21, 2024. Picha na OMR

Muktasari:

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema kila mtu atimize wajibu wake kwa kuwa kurudi kwa Rais kusema maji hayatoki, ataacha kazi

Mwanga. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema endapo maji hayatawafikia wananchi kama ilivyokusudiwa na Serikali katika mradi wa Same - Mwanga -Korogwe  ifikapo Juni, mwaka huu, ataacha kazi.

Dk Mpango ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Machi 21, 2024  alipotembelea mradi huo ambao chanzo chake ni Bwawa la Nyumba ya Mungu, ambao upo katika Kata ya Kirya, Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro.

"Amri ya Rais (Samia Suluhu Hassan) ni kwamba maji yatoke Mwanga na  Same  ifikapo Juni mwaka huu, nataka  nirudie tena, mjipange vizuri, wasimamieni makandarasi na wataalamu, bahati nzuri wana uwezo, usiku na mchana maji yatoke. Mradi huu umekuwa kero kwa wananchi wa maeneo haya, ni takribani miaka 19 imepita tangu umeahidiwa na kuanza kutekelezwa 2014,"amesema Dk Mpango.

"Kila mtu atimize wajibu wake, kurudi kwa Rais  kwamba maji hayotoki…mimi nitaacha kazi, kama maji hayatoki hapa, mimi nikiacha kazi, hao wengine sijui, Katibu Mkuu na waziri wake mimi sijui, kwa hiyo tuelewane vizuri."

Hivyo, amewataka watendaji wa Wizara ya Maji  kutimiza wajibu wao  ikiwamo  kuwasimamia makandarasi na wataalamu wanaotekeleza mradi huo pamoja na kuweka kambi  kusudi kazi ifanyike usiku na mchana.

Makamu huyo wa Rais amesema ametoa maagizo hayo ili wananchi wa wilaya za Mwanga, Same na Korogwe wapate maji kama walivyoahidiwa na Serikali.

Historia inaonyesha mradi huo wa maji ulitolewa ahadi na  Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwaka 2005 wakati akiomba kura kuingia madarakani kwa kipindi cha kwanza.

Ulianza kutekelezwa mwaka 2014 na unatarajiwa kugharimu Sh262 bilioni hadi kukamilika kwake, huku ukitarajiwa kunufaisha wakazi 438,000.

Dk Mpango amesema wananchi wameusubiri mradi huo kwa muda mrefu huku wakiwa na kiu ya kuondokana na changamoto ya maji katika maeneo yao.

Kutokana na kusuasua kwake, Dk Mpango amewaagiza wataalamu kutoka Wizara ya Maji kuweka kambi kwenye eneo hilo la mradi na wahakikishe unatekelezwa na kukamilika kama ilivyopangwa.

"Wananchi wamesubiri sana kwa muda mrefu,  sasa imefikia mahali hawa wananchi tuwapatie maji, narudia tena kama kuna kituo ambacho napenda muwe mnakuja mara nyingi na mpangiane zamu usiku na mchana, ni hapa," amesema Dk Mpango. 

"Waziri wa Maji na wasaidizi wako wote muweke kambi hapa, Amiri Jeshi Mkuu (Rais Samia) alishatoa amri ni lazima mhakikishe maji yanatoka, mimi nitakuja kabla yake hapa  ili kuhakikisha  hili limetimia.

“Pale mnapohisi pana changamoto mjipange kuzitatua, hatuwezi kurudi tena kuwatazama wananchi wa Same na Mwanga," amesisitiza Dk Mpango.

Amesema matumaini ya wananchi wengi wa maeneo hayo yanapaswa kutimia sasa.

“Unajua inaumiza kweli, ukikuta watu wanakunywa maji ambayo hayafai, hospitali zetu zinajaa kinamama wanapata tabu, wenye punda wabebe maji ni shida tupu , miaka 19 wanaahidiwa maji alafu wakichungulia pale wanaona hapo kwenye bwawa haikubaliki," amesema.

Pia, amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kwa kushirikiana na wakuu wake wa wilaya wasimamie rasilimali za maji na kuhakikisha vyanzo vyote vya maji vinalindwa.

 Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2014 na sasa wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha ifikapo Juni, 2024, unakamilika.

"Mradi huu kama unavyouona kwa sasa tuko asilimia 85.7  na miradi ya maji mara nyingi ikifikia asilimia 92.93 maji huwa yanaanza kutoka, tunakuhakikishia mheshimiwa makamu wa Rais, tutajitahidi kama Wizara ya Maji na timu yangu kuhakikisha zile kazi muhimu zote ambazo zimebaki ili maji yafike maeneo yanayotakiwa, tutazifanya,"amesema Katibu Mkuu.



Wakizungumza baadhi ya wananchi wa eneo la Kirya wilayani Mwanga, wamesema hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo ni mbaya hali ambayo huwafanya kutumia maji ya mito na bwawa ambayo si safi na salama.

Anitha Mkiramweni, mkazi wa Mwanga amesema kwa sasa wanatumia maji si salama na katika maeneo ya mito wanakochota ni hatarishi kwa kuwa hukutana na mamba.

"Tunaomba Serikali isimamie mradi huu ukamilike kwa wakati uliopangwa ili tuweze kupata huduma hii muhimu, kwa sasa tunatumia maji ya mito," amesema Anitha.

Monica Samuel, mkazi wa Kirya amesema mradi huo ukikamilika wataweza kufanya shughuli nyingine za maendekeo kwa kuwa kwa sasa wanapoteza muda mwingi kuzunguka kutafuta maji.

"Serikali ituangalie na kukamilisha mradi huu wa maji, tumeshapewa ahadi mara nyingi lakini bado haujakamilika, sasa ifike mwisho, mradi ukamilike ili tuondokane na adha tunayopitia kwa sasa,” amesema Monica.