Maji sasa ni mateso kila kona Tanzania

Muktasari:

  • Wakati Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-25 ikiahidi upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 maeneo ya mijini, hali ya upatikanaji wa maji mijini hairidhishi, huku kukiwa na malalamiko ya wananchi kwa uhaba wa huduma hiyo.

Dar es Salaam. Unajua kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025, iliahidi upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 maeneo ya mijini?

Ni takribani miaka miwili imebaki kabla ya ilani hiyo kukoma, lakini hali ya upatikanaji wa maji siyo mijini tu, inasikitisha karibu maeneo mengi nchini.

Wananchi hawana maji, kilio chao ni maji na hii inakwenda kinyume na ahadi za sera ya maji ya mwaka 2002 na hata Katiba inayosisitiza Serikali kuimarisha ustawi wa wananchi.

Katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, wananchi wanalalamika kukosa huduma hiyo, licha ya kuunganishwa na miundombinu na wengine wakikosa kabisa hata kuunganishwa.

Sera ya Maji ya mwaka 2002 kifungu cha 4.1.2 inasema: “Kuwa na kipaumbele katika kugawa maji ili kuhakikisha kuwa shughuli za huduma za jamii, mazingira na uzalishaji zinapata mgawo wake kulingana na mahitaji kwa kuzingatia rasilimali zilizopo, na kuziwezesha kuongeza tija, na pia kuepusha migongano.”

Hata hivyo, katika hali inayoonyesha Serikali kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo kwa wananchi, ni malalamiko ya kukosa huduma ya maji, ambayo ni muhimu na inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Miongoni mwa maeneo yaliyokithiri kwa shida ya maji jijini humo ni Mbezi Msumi, ambako wananchi wanalazimika kutumia kati ya Sh500 hadi Sh1,300 kununua ndoo moja ya maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.

“Kukosekana kwa maji safi kunaniathiri sana kwenye biashara yangu, maji tunayotumia ni ya chumvi, hakuna wateja wanakubali nywele zao kuoshwa na maji hayo,” amesema Happiness Mushi, ambaye ni mmiliki wa saluni ya kike.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Charles Msigwa alisema upatikanaji wa maji umekuwa changamoto na badala yake wamekuwa wakitumia maji ya chumvi kutoka kwa wamiliki wa visima,  huku walio na hali za chini wakitumia  maji ya mifereji.

“Wanakwenda huko pembezoni wanafukua wanapata maji, wanatumia maji machafu, kwetu imekuwa ni changamoto sana, maji ya Dawasa wakileta maji wale wa maboza wanauza Sh15,000 hadi Sh17,000 kwa lita 1,000,” amesema Msigwa.

Mbali na Mbezi Msumi, Siwema Ngaya, mkazi wa Kimara Golani jijini Dar es Salaam amesema katika eneo hilo maji huwa yanatoka kwa siku tatu kwa wiki, yani Jumanne, Alhamisi na Jumapili.

Lakini kwa siku za hivi karibuni yanatoka siku ya Alhamisi pekee na kwa saa moja tu.

Hivyo huwalazimu kununua ambapo dumu la maji ya bomba hupatikana hadi kwa Sh600-700.

Mkazi wa Kisukuru Kwa Mkuwa, Hamida Seif amesema katika eneo hilo maji hayajatoka kwa takribani miezi miwili sasa.

“Kuanzia Januari hadi sasa Februari maji hayajawahi kutoka kabisa, nikisema hayajatoka namaanisha hata yale kidogo hakuna, tunatumia maji ya visima ya kununua na gharama yake ni kubwa, siyo chini ya Sh20,000 kwa kuletewa mpira na wenye visima ujaze kwenye tanki,” amesema Hamida.

Aliyewahi kuwa Diwani wa Kibamba, Ernest Mgawe amesema tatizo la maji katika Wilaya ya Kibamba ni la muda mrefu na bado hakujawa na suluhisho la kudumu.

“Kuna maeneo ambayo hayajaunganishwa na maji kabisa, kama Mbezi Msigani, Msumi na Makabe, huko wanategemea tu maji ya kununua na kuchimba mifereji," amesema.

Katika eneo la Kariakoo nako kuna malalamiko, ambapo Mariam Muhidin, amesema changamoto ya maji katika eneo hilo ni tangu Desemba mwaka jana na hakuna taarifa yoyote kuhusu ukosefu wa maji hayo.

Mkazi huyo kutoka Mtaa wa Mkunguni amesema hawajui sababu ya kukosa maji ni nini, kwa sababu kama visima vya Serikali vilichimbwa, kwa nini maji hakuna.

Mariam amesema maji wanayotumia ni ya visima vilivyochimbwa na watu ambao wameachana na huduma ya Dawasa.

“Unajua kuna watu wana visima wala hawatumii maji ambayo sisi tunalalamika kuyakosa kila siku, huko ndipo tunapochota maji,” amesema Mariam.

Hata hivyo, alisema kwa zaidi ya miezi miwili hakuna huduma ya maji ya kawaida na yakitoka labda baada ya wiki mbili yanatoka mara moja, tena ni kidogo sana na hayachukui zaidi ya nusu saa yanakatika, hata jaba ya ndoo sita halijai.

“Lakini cha kushangaza bili ya maji ilivyokuja ya katikati ya mwezi huu wa Februari ilikuwa hatari, yaani inaonyesha tumetumia uniti zaidi ya 20, wakati maji hakuna, sijui tatizo ni nini. Maji hayatoki kama inavyotakiwa lakini bili inakuwa kubwa,” amelalamika Mariam.

Naye Felix Mwakalinga anayeishi Majohe Dar es Salaam, amesema wamekuwa wakipata mgawo wa umeme mara mbili hadi tatu kwa wiki, ila huduma ya maji wanaweza kuikosa wiki mbili hadi tatu.

Maji sasa ni mateso kila kona Tanzania

“Nimeshazoea kulipa uniti 8 hadi 12 kwa mwezi kwa matumizi yangu ya maji nyumbani, lakini sasa ni mwezi wa tatu Dawasa wamekuwa wakinitumia meseji ya kunidai unit 1, ikimaanisha wananipa mateso makubwa ya huduma yao,” amesema.

Kauli ya Serikali

Juhudi za kumpata Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Naibu wake, Maryprisca Mahundi hazikufanikiwa baada ya simu zao kuita bila kupokelewa.

Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano wa Dawasa, Everlasting Lyaro alipoulizwa kuhusu kero hiyo, alimtaka mwandishi kusikiliza mahojiano yaliyofanywa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Kiula Makalla Kingu Februari 19, 2024.

Kaimu Mtendaji mkuu Dawasa, Kiula Kingu

Katika mahojiano hayo, Kingu amekiri kuwepo kwa changamoto za upatikanaji wa maji, akisema ni kutokana na mvua za El-Nino zilizoanza Oktoba mwaka jana hadi Januari.

“Kwa jumla kilomita 35 ya miundombinu yetu ambayo ni sehemu zaidi ya 55 zilichukuliwa na maji. Kwa hiyo tumeendelea na juhudi kurudisha maeneo ambayo miundombinu imeondolewa na huduma ya maji imeanza kurejea,” amesema.

Hata hivyo, Mwananchi Digital inatambua kuwa kero ya maji imekuwepo kabla hata ya mvua za El-Nino, ambapo maeneo mbalimbali nchini yamekuwa katika hali ngumu ya upatikanaji wa maji.

Hali ilivyo kwingineko Tanzania

Mkoani Kilimanjaro nako kumekuwa na kero hiyo, ambapo baadhi ya wananchi wa kijiji cha Singa, kata ya Kibosho Mashariki, wilaya ya Moshi, wamelazimika kunywa maji machafu yanayotoka katika Mto Karanga kutokana na uhaba wa maji.

Wakizungumza jana Februari 21, wananchi hao wamesema licha ya kila mwananchi kuunganishiwa maji kwa gharama ya Sh162, 000 mwaka 2018 changamoto ya maji imeendelea kuwepo katika kitongoji hicho, hali ambayo imekuwa ikisababisha kero kwa wananchi.

Yasinta Mushi, mkazi wa kitongoji cha Singa kati, wilayani hapa, amewatupia lawama viongozi wanaosimamia miradi ya maji katika kijiji hicho na kusema kwamba changamoto hiyo ya maji inasababishwa na wao baada ya kuanza kusimamia miradi ya maji katika kijiji hicho.

Alipotafutwa meneja anayesimamia mradi wa maji kijijini hapo, kutoka taasisi ya SIKIKA, Mwita Juma amekiri uwepo wa changamoto ya maji katika baadhi ya maeneo katika kijiji hicho, na kwamba jitihada zinafanyika kuhakikisha wananchi wanapata maji.

Katika Jiji la Mwanza, mkazi Mtaa wa Ng'washi Kata ya Buhongwa, Esther Muyenjwa amelalamikia tatizo la ukosefu wa maji katika eneo lao, huku akidai kuchoshwa na ahadi zinazotolewa na Serikali kukabiliana na changamoto hiyo.

"Mpaka sasa maji hata kudondoka tu hakuna, hao Mwauwasa wanazidi kutudanganya kwamba tatizo wanalishughulikia mbona mpaka sasa hivi maji hakuna? Ni bora wawe wanasema ukweli kama maji hayatoki tununue wanatukwaza sana wateja wao," amesema Muyenjwa 

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Ofisi ya Mawasiliano Mwauwasa Mkoa wa Mwanza, imeeleza kuwepo mgawo na kukosekana kwa huduma hiyo katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo, jambo linalotajwa kusababishwa na uwepo wa mgawo wa umeme jijini humo.

Katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilayani humo, Ismail Ismail amekiri kuwepo kwa upungufu wa maji, akisema wanatarajia kuchimba visima 20 vya maji katika vijiji 20 vya wilaya ya Mbozi.

Hali ilivyo makao makuu ya nchi Dodoma

Makao makuu ya  nchi Dodoma pia yameendelea kukumbwa na uhaba wa maji, hali inayosababisha watu kupata huduma hiyo kwa mgao wa mara mbili kwa wiki na katika maeneo mengine wanapata mara moja.

Hata hivyo, wakati mwingine hali inakuwa tofauti kwani mgao haufuatwi kama ilivyo kwenye ratiba, kutokana na siku za kupata maji kutofautiana na hivyo kusababisha kero kwa wananchi.

Joel Mjengi,  mkazi wa Mnada mpya jijini Dodoma amesema kuwa japo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa) hutoa ratiba ya mgao wa maji kila siku, lakini utekelezaji wake ni mdogo kutokana na maji kutotoka  siku husika.

Imeandikwa na Elias Msuya, Aurea Simtowe (Dar), Mgongo Kaitira, Anania Kajuni, Daniel Makaka (Mwanza), Rachel Chibwete (Dodoma), Janeth Joseph (Kilimanjaro).