Majibu mshirika wa Mdee yaliyoibua kicheko mahakamani
Muktasari:
- Shahidi wa pili upande wa walalamikaji katika kesi ya wabunge 19 wa viti maalim waliofukuzwa uanachama wa Chadema amemjibu Wakili wa Chadema kuwa ndiye alipaswa kumsaidia kufungua kesi kupinga Katiba ya Chadema
Dar es Salaam. Shahidi wa pili katika kesi ya wabunge wa viti maalumu 19 waliofukuzwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Hawa Mwaifunga, ameieleza Mahakama Kuu kuwa kiongozi wa jopo la mawakili wa Chadema, Peter Kibatala ndio alipaswa kumsaidia kufungua kesi kupinga katiba ya chama hicho.
Hawa ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema(Bawacha) amemtiwisha jukumu hilo Wakili Kibatala wakati akijibu maswali yake alipokuwa anamhoji kuhusiana na ushahidi wake kwenye kiapo chake alichokiwasilisha mahakamani.
Katika maswali hayo ya dodoso leo Alhamisi, Oktoba 13, 2022, Wakili Kibatala amemuuliza Mwaifunga kama anatambua katiba ya Chadema inaruhusu Kamati Kuu kuchukua hatua za dharura na kutoa uamuzi dhidi ya mwanachama hata bila yeye kusikilizwa.
Mwaifunga amejibu anatambua kuwa katiba hiyo ya Chadema inaruhusu Kamati Kuu kufanya hivyo lakini akasema lakini katika misingi ya haki kama ameitwa lazima ahojiwe.
Hivyo Wakili Kibatala akimuuliza iwapo aliwahi kufungua kesi kulalamimia katiba ya Chadema kuwa ina tatizo?
"Mimi sio mwanasheria, ningewezaje kufungua ndio wanasheria lakini hukunisaidia,"alijibu Mwaifunga na kuamsha vicheko kwa wasikilizaji wa kesi hiyo.
Katika mahojiano hayo Mwaifunga amedai licha ya kukata rufaa rufaa Baraza Kuu na kuwasikisha hoja zake zarufaa, lakini akupewa nafasi ya kusikili badala yake Baraza Kuu lilimsikiliza aliyekuwa anamlalamikia (Kamati Kuu ya Chadema) na si yeye aliyeshtaki.
Wabunge hao akiwemo Halima Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), wamefungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu, wakipinga kufukuzwa uanachama, kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama.
Hata hivyo jopo la mawakili wa Chadema linaloongozwa na Peter Kibatala liliomba mahakama na ikaridhia na kuwaamuru wabunge hao wanane kati yao akiwemo Mdee wafike mahakamani kwa ajili ya kuwafanyia mahojiano kuhusiana na ushahidi wao yaani malalamiko yao waliyoyato kwenye viapo vyao.
Mbali na Mwaifunga wengine walioitwa kuhojiwa ni Halima Mdee, Grace Tendega ambaye ndiye alikuwa Shahidi wa kwanza kuhojiwa, Nusrati Hanje, Ester Matiko, Ester Bulaya, Jesca Kishoa, na Cecila Pareso.
Shauri hilo namba 36 la mwaka 2022 lilianza kusikilizwa rasmi Ijumaa iliyopita, ambapo Tendega alifungua pazia kwa kuwa wa kwanza kupanda kizimbani na kuwekwa katika kikaango cha maswali kutoka kwa wakili Kibatala.
Katika kesi hiyo wanapinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema wa Mei 11, 2022, kutupilia mbali rufaa zao za kupinga uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 27, 2020 kuwafukuza uanachama kwa tuhuma za kuapishwa kuwa wabunge bila ridhaa ya Chama.
Hivyo wanaiomba mahakama itengue mchakato na uamuzi huo, iamuru Chadema kutimiza wajibu wake kisheria, yaani kuwapa haki ya kuwasikiliza na itoe zuio kwa Spika na Nec kuchukulia hatua yoyote mpaka malalamiko yao yatakapoamuriwa.
Mbali na Chadema kupitia Bodi yake ya Wadhamini, wadaiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye pia anasimama kwa niaba ya Bunge la Tanzania; na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).