Makarani Arusha, Katavi waporwa vishikwambi

Muktasari:

Makarani wawili wa mikoa ya Arusha na Katavi wameporwa vifaa vyao vya kukusanyia takwimu maarufu kama vishikwambi, huku Polisi wakifanikiwa kumpata mtuhumiwa mmoja.

Arusha. Wakati sense ya Watu na Makazi ikiendelea nchini, makarani wawili wamejikuta katika wakati mgumu baada kuporwa vifaa vyao vya kukusanyia taarifa maarufu kama vishikwambi na vibaka.

Tukio la kwanza limetokea jijini Arusha ambapo karani aliyetambuliwa kwa jina la Saraphia Kiwango ameporwa kishikwambi chake alipokuwa akielekea kuanza kuhesabu makundi maalum katika Kata ya Unga Ltd jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 23, Diwani wa Unga Ltd, Mahmoud Said amesema alipokea taarifa usiku wa kuamkia Agosti 23, kuwa kuna karani ameibiwa kishikwambi na mumewe kujeruhiwa kichwani na bodaboda hao wawili.

"Jana usiku hawa makarani wa Sensa waliitwa kwa mtendaji wakati wanakwenda huko ndiyo wakakutana na vibaka waliokuwa kwenye bodaboda wakamjeruhi mumewe na kumpora kishikwambi kisha kutoweka kusikojulikana," amesema.

Mtendaji wa Kata hiyo, Sophia Laizer amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa karani huyo baada ya kuibiwa kishkwambi hicho na kuwa alivamiwa na vijana hao akiwa njiani kuelekea kuhesabu makundi maalum.

"Ni kweli tukio hilo lilitokea jana usiku lakini ameshapewa kishkwambi kingine na anaendelea na kazi," amesema

Naye Mratibu wa sensa wilaya ya Arusha, Maneno Maziku amekiri kutokea kwa tukio hilo ila kitu kiko sawa na kuwa aliyejeruhiwa anaendelea vizuri na kuwa kayika maeneo mengine zoezi linaenda vizuri.

"Ni kweli aliporwa kishikwambi na mume wake kujeruhiwa kichwani lakini ameshapewa kishikwambi kingine anaendelea na kazi lakini pia majeruhi hali yake inaendelea vizuri," amesema bila kuwataja majina yao.

Hata hivyo, akizungumzia kazi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Said Mtanda amesema hali ni shwari katika maeneo mengine na kuwa watakaotaka kuvuruga sensa.

"Hali ni shwari ila jana usiku kuna karani mmoja wahuni walitaka kumshambulia kwa sababu tuliweka mgambo na polisi walidhibitiwa," amesema.

Kibaka aliyepora kishikwambi adakwa

Katika halmashauri ya Mpimbwe kata ya Majimoto mkoani Katavi, karani aliyetajwa kwa jina la Kenani Kasekwa amevamiwa na mtu asiyejulikana na kumwibia kishikwambi na fedha taslimu Sh760,000.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Catherine Mashala akizungumza kwa simu karani huyo wa kata ya Majimoto alivamiwa baada ya kitasa cha mlango wake kuvunjwa na mwizi huyo kupora vitu hivyo.

“Mwizi aliingia chumbani akaiba vitu hivyo na vingine, inavyoonekana alipuliza dawa ili walale usingizi fofo akapata mwanya wa kuiba pia redio aina ya subwoofer na simu,” amesema Mashala.

Amesema baada ya kutokea tukio hilo karani huyo alitoa taarifa kituo cha polisi Majimoto, polisi walifanya msako kisha kumkamata mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ally Makame alipotafuwa na Mwananchi ili kuthibitisha tukio hilo simu yake iliita pasipo kupokelewa.

Hali shwari Karatu

Kwa upande wake Mratibu wa sensa wilaya ya Karatu, Rose Mipango amesema sensa inaendelea vizuri na kwamba zoezi hilo lilianza kwa kuhesabu makundi maalum wakiwemo wageni waliolala hotelini, watoto wanaoishi mazingira hatarishi na madereva wa malori.

Ametaja kundi lingine kuwa ni jamii ya wafugaji ya wadzabe waliopo Kata ya Baray, ambao wamechinjiwa na kugaiwa nyumbu wawili na pundamilia wawili pamoja na ndizi ili waweze kuhesabiwa.

"Wamegawiwa pundamilia wawili na nyumbu wawili kama kitoweo kwani hilo ni kundi maalum na chakula chao kikuu ni nyamapori na matunda hivyo tumeweka utaratibu maalum ili washiriki zoezi hili muhimu," amesema.

Aidha katika baadhi ya maeneo ikiwemo barabara za Uhuru na Makongoro zilizopo katikati ya jiji la Arusha maduka mengi ya biashara yalikuwa yamefungwa.