Mama, babalishe kusajiliwa nchi nzima

Uzinduzi wa usajili wa Mama lishe na baba lishe Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Mbali na mama na baba lishe, shirika la Tiva linakusudia wajasiriamali zaidi ya 15 milioni katika kanzidata ya kidigitali ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za mikopo, bima na utatuzi wa kero zao.

Dar es Salaam. Ili kurasimisha biashara ya vyakula nchini, Chama cha Baba lishe na Mama Lishe Tanzania (Chabamata) kwa kushirikiana na Shirika la Tiva limeanza usajili wa wadau hao ili kukabiliana na changamoto zainazowakabili na kupata fursa zikiwemo mikopo na bima.

 Akizungumza jana jijini hapa leo October 14, Mwenyekiti wa Chamabata Taifa, Anastazia Lyakura amesema licha ya chama hicho kusajiliwa Februari 2022 Wizara ya Mambo ya Ndani, bado ukusanyaji wa kanzidata umekuwa changamoto, hivyo wanaanza kufanya usajili nchi nzima.

“Lengo la kuwaunganisha baba na mama lishe wote nchini ni kuzipata fursa za biashara na kukabiliana na changamoto. Kwa sasa tumeanza kusajili wanachama, kuanzia wiki ijayo tutaanza kuingia katika kila kata na wilaya kwa ajili ya kuwasajili hao wanachama,” amesema.

Kwa upande wake Katibu wa Chamamata Mkoa wa Dar es Salaam, Aziz Mussa amesema kumekuwa na changamoto nyingi zinazowakabili, hivyo kuna umuhimu wa kupata utambulisho rasmi.

“Adha tunazopitia ni pamoja na kusemwa vibaya na wateja tunapowahudumia, kucheleweshewa fedha baada ya kutoa huduma, kupandishiwa kodi za pango kiholela, kuhamishwa kwenye maeneo hayo. Sasa Chabamata imekuja kukabiliana na changamoto hizo,” amesema.

Naye Fadhili Makundi ambaye ni mwezeshaji wa Chabamata amesema chama hicho kinahusisha wadau wa chakula Tanzania nzima, wakiwamo wachuuzi wa samaki, wauza matunda, mbogamboga, nyama, wauza mchele, wauza vizi na wapishi.

“Lengo letu ni kuwaunganisha wadau wajue sera na wanachama wetu. Faida nyingine ni kupata mikopo ya bei nafuu, kupata mikopo ya mali kauli, kwa mfano muuzaji wa chakula anaweza kupata mchele, kuku au nyama kwa kupewa hizo bidhaa na akishauza anarudisha fedha jioni kwa mwenye duka na kubaki na faida yake,” amesema.

Amesema kwa kushirikiana na Tiva, wanachama wao watanunua vocha ya Sh1, 000 ili aingizwe katika mfumo wa kidigitali wa utambulisho.

Akizungumzia mfumo huo, Mkurugenzi mtendaji wa Tiva, Joshua Muhingo alisema itachukua miezi mitatu kusajili mama lishe pamoja na makundi mengineyo.

“Tuna makundi sita mpaka sansasa yenye wachanama wanaofikia 15 milioni, kwa hiyo tuna takeribani miezi mitatu ya kufanya usajili ndipo wanachama hao waweze kupata hizo huduma,” amesema.

Amesema kundi hilo ni muhimu katika huduma ya chakula na mapato kwa Serikali.

“Ulimwenguni, zaidi ya theluthi moja ya watu duniani wanashiriki chakula cha mitaani kila siku, na hivyo kufanya kuwa tegemeo kwa wakazi wengi wa mijini wenye kipato cha chini na kati, wakiwemo vijana, wanaume na hata wanawake. Hata hivyo, pamoja na umuhimu wao wa kiuchumi, kundi hili limesalia kuwa lisilo rasmi nchini Tanzania na hata nchi zingine za ulimwengu wa tatu.

“Serikali imefanya juhudi za kupongezwa kurasimisha na kutoa msaada kwa wachuuzi hawa wa mitaani. Hata hivyo, upungufu mkubwa umesalia katika uanzishwaji wa kanzi data ya kina na sahihi yenye taarifa zote muhimu zinazohitajika kuhusu wachuuzi wa chakula mitaani nchini Tanzania,” amesema.