Mamantilie, mteja wake wakutwa wamefariki dunia mgahawani wakiwa ‘watupu’
Mamantilie Swiga Mwakalobo (35) na mteja wake, Jacob Chang’a enzi za uhai wao.
Muktasari:
- Mamantilie na mteja wake, wamefariki dunia wakiwa ndani ya mgahawa katika maeneo ya Mkwawa, Manispaa ya Iringa.
Iringa. Mamantilie aliyekuwa anauza mgahawa katika eneo la Mkwawa, Manispaa ya Iringa, Swiga Mwakalobo (35) na mteja wake, Jacob Chang’a wamekutwa wakiwa wamefariki dunia ndani ya mgahawa huku wakiwa bila nguo.
Miili yao imekutwa jana Oktoba 6, 2023 asubuhi baada ya ndugu kumtafuta Swiga ambaye siku moja iliyopita hakurudi nyumbani.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya majirani wamesema baada ya kubomoa mlango, walikuta miili hiyo huku pembeni kukiwa na jiko la mkaa ambalo limebandikwa maharage.
"Hadi juzi usiku Swiga alikuwa akiendelea na shughuli zake za mgahawa kwa sababu huwa anachelewa kufunga kutokana na maandilizi ya chakula cha asubuhi, hatukuwa na hofu," amesema Hamza Hamisi ambaye ni ndugu yake Swiga.
Amesema kwa sabababu hadi kufikia jana asubuhi hawakumuona Swiga na ndipo majirani walianza kufanya juhudi za kumtafuta kwa kumpigia simu bila mafanikio.
"Ndipo tukaenda mgahawani kwake na kupiga simu na tukasikia inaitia ndani ya mgahawa na mlango ulikuwa umefungwa. Tulipochungulia tulikuta miili miwili iko ndani na hawakuvaa nguo," amesema Ibrahim Issa, mkazi wa Mkwawa.
Amesema walivunja mlango na kubaini kwamba watu hao walikuwa tayari wamefariki.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Imalanongwa A, Hamis Chananja amesema walipiga simu polisi ambao walifika eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha tukio hilo na kwamba wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi.