Mambo gani wanawake watarajie wanapokaribia kukoma hedhi

Mambo gani wanawake watarajie wanapokaribia kukoma hedhi

Muktasari:

  • Ukomo wa hedhi kitaalamu ‘menopause’, ni dalili kuwa umri wa mwanamke umekuwa mkubwa na kwa wakati huo hujiandaa kuingia katika umri ambao mwili wake husimama mzunguko wa uwezekano wa kupata ujauzito.

Ukomo wa hedhi kitaalamu ‘menopause’, ni dalili kuwa umri wa mwanamke umekuwa mkubwa na kwa wakati huo hujiandaa kuingia katika umri ambao mwili wake husimama mzunguko wa uwezekano wa kupata ujauzito.

Kukaribia kukoma hedhi huonekana katika dalili zake, nayo huja ili kumuonyesha mhusika kuwa sasa uwezo wa kuzaa umefikia mwisho.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Jane Muzo anasema mwanamke anaweza kuona dalili zinazoelekeza kuwa anafikia kukoma hedhi.

Anasema dalili hizo ni pamoja na vipindi vya hedhi kubadilika kila mara na kwa wanawake wengine huanza kuona dalili hizo wakiwa bado na umri wa miaka 30 na kuendelea.

“Kwa kawaida hali hii hujitokeza kwa wanawake wenye umri wa kati ya miaka 45 na 55, lakini pia hali hii huweza kusababishwa na upasuaji wa kuondoa ovari au kizazi (katika hysterectomy),” anasema.

Anasema wanawake wanaopitia katika hali hiyo hupata athari kadhaa ambazo huwafanya wawe tofauti na kipindi chao kingine walichowahi kupitia.

“Athari wanazozipata zipo nyingi, lakini kuna zile zinazowapata wengi ambazo ni pamoja na mzunguko wa hedhi kuvurugika, yaani hapa anakuwa hapati hedhi kama ilivyokuwa awali kwa siku zinazoeleweka na mtiririko wa kawaida,” anasema.

Dk Muzo anasema athari nyingine ni pamoja na kupoteza kumbukumbu, lakini pia wengine hupoteza hamu ya kufanya tendo la ndoa au kuwa na hisia za matamanio ya kimwili.

“Kutokuwa na hisia ya kufanya tendo la ndoa hapa wengi huanza kupuuzia baadhi ya mambo, hasa kwa wanandoa. Hii inakuwa ni tofauti na kipindi kingine.

“Baadhi yao hupata joto kali la mwili na wengine huanza kuwa na hasira na wengine huanza kutokufanya vitu alivyokuwa akipenda awali,” anasema.

Anasema wakati huo ubongo, ngozi, misuli na hisia huathiriwa kutokana na mabadiliko ya kichocheo cha oestrogen.

Dk Muzo anasema mwili huwa na mabadiliko ambayo husababisha pia matatizo kwenye kibofu na ukavu kwenye sehemu za uke ni miongoni mwa changamoto.

Anasema katika kipindi hicho mwanamke inabidi amuone daktari bingwa wa kinamama, afanyiwe uchunguzi ili kuthibitisha hana tatizo lingine na kwamba kuna dawa anaweza pewa ili hali hiyo isiwe na madhara zaidi kwake.


Ukomo wa hedhi

Dk Muzo anasema kwa kawaida katika mzunguko wa mwezi uzalishaji wa yai hufanyika kutoka kwenye ovari kila mwezi kwa ajili ya kurutubishwa na kwamba katika kipindi hicho, uwezo wa wanawake wa kuhifadhi mayai ukipungua, hedhi na uwezo wa kushika mimba hukoma.

Anasema katika kipindi hicho mwili nao huacha kuzalisha kichocheo cha oestrogen, ambacho hudhibiti mchakato wote.

“Hata hivyo, hali hii haijitokezi mara moja, huchukua miaka kadhaa kwa kichocheo hiki kupoteza uwezo wake, wakati ovari zikizalisha mayai machache wakati umri wa wanawake ukisogea, oestrogen kiasi kidogo huzalishwa mwilini,” anasema.

Mkuu wa Kitengo cha magonjwa ya kinamama na uzazi Muhimbili, Dk Nathanael Mtinangi anasema kwa kawaida mwanamke ana mayai 360 ambayo yanapokaribia kwisha kuna viashiria na kwamba wengine wanayo pungufu.

“Kisayansi mwanamke anatoa yai moja kwa mwezi, hivyo hutoa mayai 12 kwa mwaka, kwa kuwa uzao wake ni miaka 30 akianza kuzaa na miaka 15 mpaka anafikisha miaka 45 ni miaka 30 ukizidisha kwa miezi 12 unapata mayai 360, huku wengine wakiwa nayo zaidi na wengine pungufu,” anasema.

Dk Mtinangi anasema kwisha kwa mayai hayo ambayo huvunjika kila mwezi mimba isipotunga ndiyo kukoma hedhi na mwanamke hawezi kupata mimba.

Vyakula chanzo

Hata hivyo, utafiti uliofanyika nchini Uingereza umebaini ulaji wa tambi na wali kwa wingi husababisha ukomo wa hedhi mapema.

Ulaji wa tambi na wali kwa wingi kwa wanawake nchini Uingereza umesababisha kuwahi kukoma kwa hedhi mwaka mmoja na nusu mapema zaidi ya wastani wa umri wa miaka 51.

Utafiti mwingine uliofanywa na chuo kikuu cha Leeds kwa wanawake 914 nchini Uingereza pia umebaini kuwa mlo ulio na mafuta ya samaki kwa wingi na njegere na maharage, unaweza kuchelewesha ukomo wa hedhi kwa wanawake. Lakini wachambuzi wanasema kuna sababu nyingine, zikiwemo za kijenetiki.

Utafiti ulichapishwa kwenye jarida la Afya la Epidemiology & Community Health na wanawake waliulizwa mlo wao huwa una vyakula gani.

Mlo wenye mboga za jamii ya kunde kwa wingi, kama vile njegere, maharage, maharage membamba na dengu kwa wastani huchelewesha ukomo wa hedhi.

Sababu nyingine zilizoainishwa na watafiti ni pamoja na uzito wa mwanamke, historia ya uzazi na waliopata tiba za homoni, lakini hawakuangalia sababu za kijenetiki.

Janet Cade, mtaalamu wa lishe anasema, “umri ambao ukomo wa hedhi huanza unaweza kuleta madhara makubwa kwa baadhi ya wanawake.”