Mangula: Mafaili nayaacha kwa Kinana

Muktasari:
- Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Philip Mangula amekabidhi rasmi jina la mzee wa mafaili Kwa makamu mwenyekiti mpya Abdulrahman Kinana.
Dodoma. Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Mzee Philip Mangula amekabidhi rasmi jina la mzee wa mafaili Kwa makamu mwenyekiti mpya Abdulrahman Kinana.
Mangula amesema kuwa anakwenda kupumzika lakini kazi za chama zitaendelea hata baada ya kupumzika kwake kwenye nafasi hiyo.
Amesema kuwa kijiti anamkabidhi Kinana ambaye anakijua chama vizuri na kwamba mafaili hayo anayatambua kwa kuwa amewahi kuwa katibu wa kamati hiyo.
"Sasa nitaingia kwenye baraza la wazee ambalo huundwa na viongozi wakuu wastaafu wa chama, kwa hiyo mafaili bado yapo na ninayaacha yakiendelea,"amesema Mangula.
Kinana amechukua nafasi hiyo baada ya kupigiwa kura zote za ndiyo 1,875 bila kupoteza kura hata moja hivyo amepita kwa asilimia mia moja.
Akitoa neno la shukrani Kinana amesema atafanya kazi kwa moyo mmoja kwani imani huzaa imani na atajitahidi kutimiza matarajio ya mwenyekiti wao Rais Samia Suluhu Hassan.
Kinana ametoa ahadi ya kwanza kuwa anataka kukiimarisha CCM ili kiwe imara kinachokubalika kwa Watanzania.
Amesema lazima haki isimamiwe ili kufanya chama kiwe na demokrasia, kusiwepo mizengwe, upendeleo, rushwa wala umaarufu.
"Haki ya pili ni ya kutoa mawazo, lazima wanachama watoe mawazo, hakuna mwenye haki miliki ya mawazo, lazima tuhimize demokrasia, lazima kusimamia demokrasia," amesema Kinana.
Kinana amesema wanachama wakimchagua mtu kwa nini apingwe labla kama kuna sababu za msingi za kufanya hivyo.